2016-10-11 14:32:00

Washughulikieni wala rushwa na mafisadi kwa kuzingatia Katiba na Sheria!


Idara ya Usalama wa Taifa nchini Nigeria imewatia mbaroni Majaji 7 na wengine 15 kuwaweka chini ya uchunguzi mkali pamoja na kutaifisha mali yenye thamani za dolla za kimarekani 800, 000 zilizokuwa zimehifadhiwa kwenye nyumba za Majaji hawa wanaotuhumiwa kujihusisha na vitendo vya rushwa na ufisadi.

Akizungumzia kuhusu sakata hili, Kardinali John Onaiyekan, Askofu mkuu wa Jimbo kuu la Abuja, Nigeria, ameitaka Serikali kuendesha kesi hii kwa kuzingatia haki, haki, ukweli na uwazi ili kuondoa mawazo kwamba, Serikali inataka kuwafumba midomo Majaji, ili washindwe kutekeleza wajibu wao barabara, hali ambayo inaonesha hali ya wasi wasi na mfumo wa sheria na mahakama nchini Nigeria. Kardinali Onaiyekan anaendelea kufafanua kwamba, kumekuwepo na mjadala mkali kuhusu nafasi ya Majaji ndani ya Katiba ya Nigeria na utekelezaji wake na kwamba, baadhi ya watuhumiwa ni Majaji kutoka katika Mahakama kuu ya Nigeria. Kutokana na shutuma hizi, hali ya kisiasa nchini Nigeria kwa sasa ni tete sana anakaza kusema Kardinali Onaiyekan.

Baraza la Majaji nchini Nigeria pamoja na watetezi wa haki za binadamu wanasema uchunguzi unaofanywa dhidi ya Majaji hawa ni kinyume cha sheria na kwamba, Serikali inataka kuwatisha Majaji ili wasitekeleze azma yao ya kupambana na wala rushwa na mafisadi wakuu nchini Nigeria. Ili haki iweze kutendeka, kuna haja kwanza kabisa Serikali kuhakikisha kwamba, Majaji wala rushwa wanaondolewa kwenye mfumo wa haki na kufikishwa Mahakamani ili sheria iweze kushika mkondo wake. Majaji waaminifu, waadilifu na wachapakazi wapewe nafasi ya kutekeleza vyema kazi yao kadiri ya Katiba na sheria za nchi.

Kardinali John Onaiyekan anaendelea kufafanua kwamba, Rais Muhammadu Buhari alipoamua kulivalia njuga sakata la rushwa na ufisadi nchini Nigeria, Baraza la Maaskofu Katoliki Nigeria lilimuunga mkono. Hapa jambo la msingi ni kuhakikisha kwamba, vyombo vya ulinzi na usalama havina budi kuhakikisha kwamba, Katiba na sheria za nchi zinatekelezwa kikamilifu bila upendeleo. Watuhumiwa wapewe nafasi ya kujitetea mbele ya sheria, ili kweli haki iweze kutendeka badala ya kulitumbukiza taifa katika mpasuko wa Kikatiba na kisheria, jambo ambalo ni hatari kwa haki, amani, usalama na mafungamano ya kijamii!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.