2016-10-10 08:18:00

Mshikamano na wananchi wa Haiti waliokumbwa na maafa!


Baba Mtakatifu Francisko wakati wa Sala ya Malaika wa Bwana, baada ya maadhimisho ya Jubilei ya Bikira Maria, maalum kwa ajili ya vyama vya kitume vyenye ibada kwa Bikira Maria Mama wa Mungu na Kanisa, Jumapili tarehe 9 Oktoba 2016 kwa masikitiko makubwa aliungana na wananchi wote walioguswa na kutikiswa kwa tufani ya Mathew iliyovikumba Visiwa vya Caribbiani, lakini kwa namna ya pekee, nchi ya Haiti.

Tufani hii imesababisha maafa makubwa kwa watu na mali zao. Baba Mtakatifu anapenda kuonesha uwepo wake wa karibu na matumaini makubwa kwa mshikamano unaoneshwa na Jumuiya ya Kimataifa, Taasisi za Kanisa pamoja na watu wote wenye mapenzi mema. Baba Mtakatifu anawaalika waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema kuungana pamoja naye katika sala kwa ajili ya watu hawa ambao wameathirika kwa kiasi kikubwa.

Wakati wa Sala ya Malaika wa Bwana, Baba Mtakatifu pia amemkumbuka Padre Gennaro Fueyo Castanon na waamini walei watatu waliotangazwa kuwa Wenyeheri huko Oviedo, Hispania, Jumamosi tarehe 8 Oktoba 2016. Baba Mtakatifu amemshukuru Mungu kwa mashuhuda hawa wa imani wanaoungana sasa na umati mkubwa Mashahidi wa imani walioyamimina maisha yao kwa ajili ya Kristo na Kanisa lake! Baba Mtakatifu aliwashukuru waamini wote walioshiriki kikamilifu katika maadhimisho ya Jubilei ya Maria sanjari na kujikabidhi chini ya ulinzi na tunza ya Bikira Maria.

Waamini wamemwomba Bikira Maria awasaidie binadamu kuutengeneza ulimwengu ili uweze kuwa kweli bustani inayopendeza kwa kuchagua zawadi ya uhai; kwa kupokea na kumwilisha Injili ya Kristo Mkombozi wa ulimwengu badala ya kuugeuza ulimwengu kuwa kama tambara bovu!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.