2016-10-10 08:32:00

Makardinali wateule 17! Watatu kutoka Barani Afrika: Nzapalainga na Mohale's


Baba Mtakatifu Francisko amefunga rasmi maadhimisho ya Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu kwa vyama vya kitume vyenye Ibada kwa Bikira Maria, Jumapili tarehe 9 Oktoba 2016 kwa kutangaza majina ya Makardinali wateule 17, kutoka katika nchi 11 na kati yao kuna Makardinali 4 ambao hawana haki tena ya kupiga au kupigiwa kura wakati wa uchaguzi wa Khalifa wa Mtakatifu Petro. Makardinali wapya watasimikwa rasmi hapo tarehe 19 Novemba 2016 katika mkesha wa kufunga rasmi maadhimisho ya Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu sanjari na Sherehe ya Kristo Mfalme wa Ulimwengu.

Uteuzi wa Makardinali hawa wapya unazingatia ukatoliki na kwamba, hiki ni kielelezo cha huruma ya Mungu. Kanisa bado linatumwa kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu inayojika katika huruma ya Mungu sehemu mbali mbali za dunia. Ushiriki wa Makardinali wapya katika maisha na utume wa Kanisa mjini Roma ni kielelezo makini cha umoja na mshikamano kati ya Khalifa wa Mtakatifu Petro na Makanisa mahalia yaliyotawanyika kila pembe ya dunia.

Makardinali wapya wataadhimisha pamoja na Baba Mtakatifu Francisko Ibada ya kufunga Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu hapo tarehe 20 Novemba 2016 huku wakiungana na Wakleri pamoja na familia ya Mungu kutoka sehemu mbali mbali za dunia. Makardinali wapya ni kama ifuatavyo:

Askofu mkuu Mario Zenari, Balozi wa Vatican nchini Syria, ataendelea na utume wake nchini humo hasa katika kipindi hiki kigumu cha machafuko ya kisiasa na maafa makubwa kutokana na vita ambayo imedumu sasa kwa takribani miaka mitano. Anasema, amepokea wadhifa huu kwa heshima ya watu wa Syria wanaoendelea kuteseka kwa ajili ya vita.

Askofu mkuu Dieudonnè Nzapalainga, Jimbo kuu la Bangui, Jamhuri ya Watu wa Afrika ya Kati anakumbukwa kwa mchango wake katika mchakato wa haki, amani na maridhiano nchini mwake. Askofu mkuu Kevin Joseph Farrel, Mwenyekiti wa Baraza la Kipapa la walei, familia na maisha kutoka USA.

Wengine ni Askofu mkuu Carlos Osoro Sierra wa Jimbo kuu la Madrid, Hispania. Askofu mkuu Sèrgio do Rocha wa Jimbo kuu la Brasilia, Brazil. Askofu mkuu Blase J. Cupich, Jimbo kuu la Chicago, USA. Askofu mkuu Patrick D’Rozario, Jimbo kuu la Dhaka, Bangaladesh.

Makardinali wateule wengine ni pamoja na: Askofu mkuu Baltazar Enrique Porras Cardozo, Jimbo kuu la Mèrida, Venezuela; Askofu mkuu Jozef De Kesel wa Jimbo kuu la Manilnes, Brusselles, Ubelgiji. Askofu mkuu Maurice Piat, Jimbo kuu la Port Louis, Mauritius. Askofu mkuu Carlos Aguiar Retes, Jimbo kuu la Tlalnepantla, Mexico, Askofu mkuu John Ribar, Jimbo kuu la Port Moresby, Papua New Guinea. Askofu mkuu Joseph William Tobin, Jimbo kuu la Indianapolis, USA.

Baba Mtakatifu Francisko ametambua mchango mkubwa na ushuhuda wa maisha ya Kikuhani na Kikristo uliotolewa na: Askofu mkuu mstaafu Anthony Soter Fernandez, Jimbo kuu la Kuala Lumpur, Malaysia. Askofu mkuu mstaafu Renato Corti, Jimbo kuu la Novala, Italia. Askofu mkuu mstaafu Mohale’s Hoek kutoka Lesotho, Afrika. Mwishoni katika orodha ya Makardinali wateule ni Mheshimiwa Padre Ernest Simoni wa Jimbo kuu la Shkodrè-Put, Scutari, Albania.

Mwishoni, Baba Mtakatifu Francisko amewaalika waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema kusali na kuwaombea Makardinali wateule, ili waweze kumsaidia katika utekelezaji wa dhamana na utume wake kama Khalifa wa Mtakatifu Petro, kielelezo makini cha: umoja katika imani pamoja na mshikamano kwa kumwambata Kristo Yesu, Kuhani mkuu, mwingi wa huruma na mwaminifu.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.