2016-10-10 15:30:00

Familia ya Mungu nchini Mauritius inahamasishwa kuwa ni shuhuda!


Kardinali mteule Maurice  E. Piat, Askofu mkuu wa Jimbo kuu Port- Louis, nchini Mauritius anasema, anamshukuru Mwenyezi Mungu kwa kumwezesha Baba Mtakatifu Francisko kumteuwa kuwa Kardinali, hasa wakati huu Mama Kanisa anapoadhimisha Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu. Kwa uteuzi huu, Baba Mtakatifu anapenda kuliimarisha Kanisa nchini Mauritius ili kweli liweze kuwa ni chombo na shuhuda wa huruma ya Mungu kwa waja wake. Iwe ni fursa kwa familia ya Mungu nchini Mauritius kutenda kwa unyenyekevu, kutubu na kuongoka, tayari kuambata huruma ya Mungu katika safari ya maisha ya kila siku!

Kardinali mteule anamshukuru Baba Mtakatifu Francisko kwa kumwona na hatimaye, kumteuwa kuwa ni Kardinali, tayari kumsaidia katika utekelezaji wa dhamana na majukumu yake kama Khalifa wa Mtakatifu Petro. Hii ni heshima kubwa inayobeba dhamana kubwa katika Kanisa la kiulimwengu, kama msaidizi wa karibu wa Khalifa wa Mtakatifu Petro na hatimaye, kushiriki pia kwa wakati muafaka uchaguzi wa Khalifa wa Mtakatifu Petro. Kutokana na dhamana na changamoto zote hizi zilizoko mbele yake, Kardinali mteule Maurice E. Piat anawaalika waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema kumsindikiza katika safari hii, anapojiandaa kusimikwa rasmi kama Kardinali hapo tarehe 19 Novemba 2016 kama sehemu ya kufunga maadhimisho ya Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu.

Itakumbukwa kwamba, Baba Mtakatifu Francisko ametoa upendeleo wa pekee kwa Maaskofu wakuu wanaotoka katika Nchi za Kimissionari. Kutoka Barani Afrika kuna: Askofu mkuu Dieudonnè Nzapailanga wa Jimbo kuu la Bangui, Jamhuri ya Afrika ya Kati. Hapa ndipo mahali ambapo Baba Mtakatifu Francisko kwa mara ya kwanza katika historia ya Kanisa alipozindua maadhimisho ya Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu, ukawa ni mwanzo wa mchakato wa haki, amani, umoja na mshikamano wa kitaifa.

Askofu mkuu mstaafu Mohale’s Hoek kutoka Lesotho; Askofu mstaafu Anthony Soter Fernandes wa Jimbo kuu la Kuala Lumpur, Malaysia pamoja na Askofu mkuu mstaafu Sebastian Koto Khoarai ni kati ya Makardinali wapya kutoka katika nchi za kimissionari! Hawa wamejipambanua kwa katika utume na ushuhuda wa maisha ya Kikristo, ndiyo maana Baba Mtakatifu Francisko anapenda kuwashirikisha maisha na utume wa Khalifa wa Mtakatifu Petro kama washauri wake wa karibu!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.