Jumatatu 26 Septemba, Rais wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC)Joseph Kabila Kabange, alitembela Vatican na kukutana na Papa Francisko na kisha alikutana na Askofu Mkuu Paulo Gallagher , Katibu wa Vatican kwa ajili ya mahusiano na nchi zingine.
Mazungumzo yao yalifanyika katika hali ya kirafiki, yakionyesha uhusiano mzuri uliopo kati ya Jimbo Takatifu na DRC. Kwa namna ya kipekee walitazama uhusiano wa Kanisa Katoliki katika maisha ya kijamii , kupitia kazi zinazofanywa na taasisi za Kanisa, kumwendeleza mwananchi kielimu, kiafya na kiuchumi hasa juhudi za kufukuza umaskini miongoni mwa jamii ya Congo. Pande zote mbili zilionyesha kuridhika na makubaliano yaliyotiwa sahihi Mei 2016, kati ya Jimbo Takatifu na DRC.
Aidha jimbo la Papa bila kuchelea , lilirejea kwa umakini zaidi hali ya kisiasa inavyosuasua katika taifa hilo, kama ilivyokuwa katika machafuko ya hivi karibuni katika mji mkuu wa Kinshasa. Kwa upande huo , Jimbo la Papa limehimiza umuhimu wa serikali kujenga ushirikiano thabiti na watendaji wengine wakuu wa kisiasa na wawakilishi wa vyama vya kiraia na jumuiya za kidini, kwa ajili ya ustawishaji wa mazuri kwa jamii nzima ya DRC, kupitia njia ya kuheshimu majadiliano na makubaliano yanayofikiwa kwa ajili ya uwepo wa utulivu na amani ya taifa.
Mwisho walizama zaidi hali ya machafuko inavyotendea eneo la Kaskazini Mashariki mwa DRC, na kuona haja ya ushirikiano zaidi kitaifa na kimataifa kwa ajili ya utoaji wa msaada unaohitaji kurejesha amani na utulivu katika eneo hilo.
All the contents on this site are copyrighted ©. |