2016-09-12 13:28:00

Papa ; Yesu hutufundisha jinsi Mungu alivyo na huruma kwa watu wote


Baba Mtakatifu Francisko Jumapili katika tafakari yake fupi kabla ya sala ya Malaika wa Bwana,  alieleza kuwa,  ujumbe wa  liturujia ya Neno kwa Jumapili iliyopita, unatuonyesha wazi kwamba, kwa huruma yake Mungu , tunasamehewa kila aina ya dhambi tunayoweza mkosea  Mungu. Tunatakaswa dhidi ya dhambi zote kama  mtu binafsi, kwa sababu Mungu daima yu upande wetu na  daima hututakia mema hata wakati tunapomwasi.

  Papa alieleza  na kuomba msaada wa  Mama  Bikira Maria, kimbilio la Wenye dhambi, aiwezeshe mioyo yetu kuwa na  imani kama ile iliyowaka ndani ya moyo wa mwana Mpotevu, aliyejisemea moyoni mwake baada ya taabu na dhiki nyingi za maisha: "Nitaondoka, nitakwenda kwa baba yangu na kusema: Baba, nimekosa" (Lk 15:18).. Papa alisema kuwa aya hiyo inakuwa ni sababu kwetu sote kufurahi kwa sababu Mungu yu tayari kutupokea na kufurahi pamoja nasi. Furaha ya Mungu inakuwa ni furaha yetu pia. 

Ni tafakari ya Papa Francisko mbele ya mahujaji na wageni waliokusanyika katika Uwanja wa Kanisa Kuu la Takatifu Petro, Siku ya Jumapili iliyopita, akitafakati Liturujia ya Neno , Injili ya Luka  sura ya 15 , ambamo mna sura ya Huruma , inayoonekana katika mifano mitatu iliyotolewa na Yesu kama kujibu manug’uniko ya waandishi na Mafarisayo. Mfano wa Kondoo aliyepotea, mfano wa sarafu iliyopotea na mfano wa mwana mpotevu.

Aliendelea kufafanua kwamba , Mafarisayo na waandishi walikuwa wamkinung’unikia  Yesu kwamba, anakaa na wadhambi na kula pamoja nao.  Na hivyo Yesu kwa mifano hiyo mitatu alipenda waeleza kwamba Mungu ni Baba mwenye huruma, anayewaelekea watu wote hata wenye dhambi na kuwapokea kwa huruma. Na kwamba, katika mfano wa kwanza, Mungu anajiwasilisha kama Mchungaji mwema anayewaacha wale  tisini na tisa na kwenda kumtafuta mmoja aliyepotea.  Mfano wa pili, Mungu anajifanisha na mwanamke maskini anayepoteza  sarafu  yake na kuitafuata hadi kuiona, na kisha kuwaita marafiki zake kufurahia pamoja nae kwa kuwa ameiopata sarafu yake iliyokuwa imepotea. . Na katika mfano wa tatu Mungu anajionyesha kama  baba ambaye anamkaribisha mtoto wake aliyeasi na kwenda mbali , lakini baada ya maisha kumshinda huko, sasa anarudi kwa baba akiomba msamaha. Huu unaonyesha jinsi Mungu alivyo na huruma.Huruma iliyoletwa na Yesu  duniani.

Papa aliendelea kutoa maelezo juu ya mifano hii mitatu akisema , inatuonyesha wazi,  sisi kwamba , mikono ya Mungu ni wazi kwa wakati wote tunapomwendea hata kama tumechafuka kwa dhambi. Mungu ni mwenye huruma. Cha msingi,  tunapaswa kutambua ni kwamba,  Mungu anatupenda na wakti wote hutukumbatia kama baba, kila tunaporejea baada ya kuasi, kama ilivyokuwa katika mfano wamwana mpotevu. Maovu  ya kidunia,  hutuwekwa mbali na Mungu Baba .Cha Msingi Papa alisisitiza, tunapolemewa na mizigo ya dunia , tukiwa mbali na Mungu, na tunatambue makosa yetu na kujisemea "Nitaondoka, nitakwenda kwa baba yangu" (mstari 18)..na kusema nisamehe nimekosa. Ni kurudi nyuma katika njia ya kuelekea nyumbani, yaani katika njia ya matumaini na maisha mapya.

Papa alieleza na kutoa wito kwa kila mmoja kwamba , Mungu anatusubiri tumrudie. Tuyaweke matumaini  yetu mapya kwa Bwana, Yeye yupo anatusubiri kwa uvumilivu, na huona nia zetu tangu kukiwa bado mbali , hutukimbilia  na kutusamehe makosa yetu.  Msamaha wake HUafuta yote ya nyuma  na kutufanya upya kwa upendo wake . Mwenye dhambi huongolewa na kuwa na matarajio mapya.  

 Baada ya sala ya Malaika wa Bwana, Papa kwa namna ya pekee alitolea maombi  maalum kwa taifa la Gabon , ambalo kwa wakati huu linapita katika kipind kigumu cha Kisiasa. Aliiwakabidhi walioathirika wa mgogoro wa kisasa  katika mikono ya Bwana. Na aliungana na  Maaskofu wa nchi kukataa dhuluma zote, akiwataka wote watembee katika njia ya maisha ya haki na amani, kwa manufaa ya wote . Aliomba wote wawe wajenzi wa amani, kupitia njia ya mazungumzo na mshikamano wa kidugu. Nao  Maaskofu Katoliki wa Gabon, katika ujumbe wao kwa Taifa ,  waliomba  mpatanishi wa kimataifa, atakayeweza kuondoa mtafaruko wa kisiasa uliojitokeza baada ya uchaguzi wa tarehe 27 Augost, kama zinenavyo hekima za  Kiafrika," ndugu wawili wakigombana basi ni muhimu kumhusisha mtu wa tatu kama mpatanishi".  Ujumbe wa Maaskofu ulitiwa saini na Askofu Mkuu Basil Mve Engone wa Libreville. 








All the contents on this site are copyrighted ©.