2016-09-05 09:06:00

Papa: Mtakatifu Mama Tereza ni mwanga unaomulikia wengi walio gizani


Jumapili 4 Septemba 2016 , Papa Francisko alimtangaza Mama Tereza wa Calcutta,  kuwa Mtakatifu , anayemulikia wengi walio katika giza la maisha,  wengi  waliokata tamaa, na waliopoteza matumaini ya kuondokana na hali ya umasikni na mateso. Na  kwa sifa zake za upole , huruma  na utakatifu aliyokuwa nao , na wingi wa matunda ya kiroho aliyozalisha, inawia vigumu kumwita tu Mtakatifu Tereza,  lakini  inakuja bila hata kufikiria kuendelea kutumia jina lililozoeleka la mama Tereza wa Calcutta, na hivyo atajulikana kama Mtakatifu Mama Tereza, Papa alieleza na  kushangiliwa kwa nguvu na waliokuwa wakimsilikiza. 

 Papa alieleza hili wakati wa homilia yake aliyoitoa katika  Ibada iliyofanyika katika uwanja wa Kanisa Kuu la Mtakatifu Petro Vatican  kwa nia ya kumtangaza kuwa Mtakatifu Mama Tereza wa Calcutta.  Ibada ilihudhuriwa na umati mkubwa wa watu karibia  120,000, kutoka pande zote za dunia.

Homilia ya  Papa , ililenga katika maisha ya Mtawa  Mama Tereza wa Calcultta, mtu maskini aliyefariki mwaka 1997, ambaye alizamisha maisha yake kusaidia jamii iliyosahaulika na kutengwa , watu wanaoishi mitaani bila makazi,  wanaodharaulika  katika mitaa ya India , wakionekana kama watu wasiokuwa na faida. Juhudi za Mama Tereza , kusaidia maskini hao, ziliwatia aibu viongozi wa dunia kwa kutojali umaskini ulioundwa  na wenye mamlaka.  Juhudi za  Mtawa huyo kwa maskini , ziligusa mioyo ya wengi , na hivyo  kuona haja ya kutoa msaada kwa maskini na wanaoteseka.

Papa Francisko , alieleza na kumtangaza  Mama Tereza wa Calcutta, kuwa Mtakatifu , mfano wa  unaong’ara  wa Kanisa linalokwenda hadi katika mipaka yote ya dunia na vitongojini , mijini na vijijini, kutoa mwanga wa injili kwa maskini na mioyo iliyojeruhiwa , mwanga wenye faraja zote.

Papa altoa mwaliko kwa wote , kulibeba tabasamu la Mama Tereza moyoni  na kuonyesha tabasamu hilo kwa wengine wote wanaokutana nao katika  safari ya maisha na hasa wale walio katika hali za umaskini na wanaoteswa na sababu zilizo nje ya uwezo wao. Papa amemtaja  Mtakatifu Mama Teresa kuwa Mtakatifu mwenye huruma , anayetetea maisha tangu yale yasiyozaliwa bado hadi yale yanayotelekezwa mitaani.

Alisema  kuwa, Mtakatifu Tereza , aliinamia wote na hasa walikuwa wameachwa kufa barabarani , aliwafariji na kuinua hadhi ya utu wao, ambayo ni zawadi ya Mungu  kwa binadamu wote.  Papa ameomba  Mwanga wa Imani na huruma  wa Mtakatifu Mama Tereza, uendelee kumulikia njia sahihi kwa  watu wengi waliogubikwa na giza la maisha, hasa walipoteza matumaini ya kuwa na maisha bora .  Ushuhuda wa Mama Tereza wa kuishi kwa kumtegemea Mungu , na uendelee kuwaleta wote hasa maskini wa maskini , karibu na Mungu. 








All the contents on this site are copyrighted ©.