2016-08-22 16:07:00

Papa awakumbuka katika sala wahanga wa bomu Uturuki


Jumapili iliyopita, Baba Mtakatifu Francisko wakati wa sala ya Malaika wa Bwana , aliwaombea  wahanga na waathirika wa shambulio la bomu la mtu aliyejilipua wakati wa sherehe ya arusi  siku ya Jumamosi ,  kusini mwa Uturuki. Shambuli lililosababisha watu 50 kupoteza maisha na wengine wengi kujeruhiwa .  Mshambuliaji huyo wa kujitoa mhanga ametajwa kuwa mtoto wa kiume mwenye umri wa miaka 12 au 13, na  alifyatua bomu aliliokuwa amejifunga nalo kiunoni kama mkanda na baada ya kujichanganya vizuri kwenye umati mkubwa wa watu waliokuwa wakisheherekea arusi katika mji wa  Gaziantep Uturuki. Wengi  wa waliofariki ni Wanawake na watoto. 

Akizungumza baada ya sala ya Malaika wa Bwana , mbele ya umati wa watu waliokusanyika katika Uwanja wa Kanisa Kanuu la Mtaktifu Petro Vatican,  Papa Francisko alionyesha masikitiko yake  kuhusu mashambulizi ya umwagaji damu, yanayotokea  katika  taifa pendwa la Uturuki, na aliwaalika wote wasali pamoja nae,   kwa ajili ya waathirika, wahanga na majeruhi, kuwaombea  zawadi ya amani ya Bwana na faraja zake kwa wote . 








All the contents on this site are copyrighted ©.