2016-08-11 10:26:00

Radio Maria na changamoto za Uinjilishaji mpya nchini Tanzania!


Radio Maria ilianzishwa kunako mwaka 1982 kama Radio ya Parokia kutokana na ugunduzi wa Padre Mario Gabliati, aliyependa kuhakikisha kwamba, familia ya Mungu katika Parokia yake inapata ujumbe wa Nenola Mungu, Mafundisho ya Kanisa na maadili, ili kuwasaidia watu kuambata njia ya maisha ya uzima wa milele. Wakristo kwa njia ya Ubatizo wanashiriki dhamana ya: Unabii, Ukuhani na Ufalme wa Kristo, kumbe walikuwa pia na dhamana ya kuchangia ukuaji na ustawi wa Radio Maria ambayo kwa miaka mingi inajitambulisha kuwa ni Radio ambayo inaendeshwa kwa mchango na ufadhili wa wasikilizaji wake!

Kunako mwaka 1987, Chama cha Radio Maria kikazaliwa na hivyo kuiwezesha Radio Maria kuwa ni Radio ya Kitaifa nchini Italia. Kunako mwaka 1998 Radio Maria ikapanua wigo wa huduma na hapo kukaundwa Familia ya Radio Maria Duniani na hapo Radio Maria ikaanza kurusha matangazo yake sehemu mbali mbali za dunia kwa kutumia njia za mawasiliano ya kisasa. Idadi ya wapenzi wa Radio Maria ikaongezeka maradufu, kiasi cha kuifanya Radio Maria kuwa ni kati ya Radio za Kanisa zinazosikilizwa na watu wengi zaidi duniani.

Hii inatokana na ukweli kwamba, Radio Maria iko karibu zaidi na wasikilizaji wake, wakati wa raha, shida na magumu. Kutokana na mwelekeo huu, Radio Maria kikawa ni chombo makini sana cha Uinjilishaji wa kina, unaogusa mahitaji ya mtu mzima: kiroho na kimwili. Radio Maria kwa kiasi kikubwa inategemea msaada wa wasikilizaji na wafadhili mbali mbali wanaoendelea kujisadaka kwa hali na mali ili kuhakikisha kwamba, Sauti ya Kikristo inasikika katika masikio na kukita mizizi yake katika akili na nyoyo za watu, ili kuwa watu wema na watakatifu; watu wanaoshiriki kikamilifu katika ustawi na maendeleo yao: kiroho na kimwili. Neno la Mungu, Mafundisho ya Kanisa, Katekesimu Mpya ya Kanisa Katoliki na Ibada kwa Bikira Maria ni mambo msingi yanayopamba vipindi vya Radio Maria sehemu mbali mbali za dunia!

Lengo kuu la Radio Maria ni kushiriki kikamilifu katika mchakato wa Uinjilioshaji wa watu, dhamana ambayo inavaliwa njuga kwa sasa na Mama Kanisa. Inapania kuwasaidia waamini kuifahamu vyema imani yao, tayari kuitangaza, kuishuhudia na kuieneza kwa jirani zao kwa njia ya matendo ya huruma: kiroho na kimwili, kama anavyokazia Baba Mtakatifu Francisko katika Maadhimisho ya Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu. Hii ni sehemu ya mchakato wa toba na wongofu wa ndani, tayari kuambata utakatifu wa maisha. Radio Maria inapania pamoja na mambo mengine kukuza na kudumisha mafungamano ya kijamii kwa kukazia umoja, udugu, upendo na mshikamano kati ya watu.

Familia ya Radio Maria nchini Tanzania inaadhimisha kumbu kumbu ya miaka 20 tangu Radio maria ilipoanzishwa nchini Tanzania kunako tarehe 26 Aprili 1996 katika Jimbo kuu la Songea, kwa lengo la kuwasaidia waamini kujifunza kutoka katika shule ya Bikira Maria ili kiumfahamu, kumpenda na kumtumikia Kristo Yesu kwa njia ya huduma makini kwa jirani zao kama alivyofanya Bikira Maria katika maisha yake. Maadhimisho haya yaliyofanyika Jimbo kuu la Dar es Salaam yalihudhuriwa na Kardinali Polycarp Pengo, Askofu mkuu wa Jimbo kuu la Dar es Salaam ambaye ametoa rai kwa Uongozi wa Radio Maria Tanzania kuhakikisha kwamba, wanakuza na kudumisha ari, mwamko na maudhui ya Radio Maria, ili Radio hii iendelee kuwa ni chombo cha Uinjilishaji, huruma na upendo wa Mungu kwa waja wake.

Kardinali Pengo amekumbusha kwamba, Radio Maria ni sauti ya Kikristo ndani ya familia inayowasaidia wanafamilia kuwa wamoja na kukua katika upendo na utakatifu wa maisha, kwa kutajirishwa na Neno la Mungu. Radio Maria inapaswa kuwa ni kiungo makini cha tunu msingi za maisha ya ndoa na familia, dhamana inayovaliwa njuga na Mama Kanisa kwa wakati huu.

Kardinali Pengo amewashukuru waamini na watu wote wenye mapenzi mema wanaoendelea kuchangia kwa hali na mali ili kuhakikisha kwamba, Radio Maria inatekeleza dhamana na utume wake kwa familia ya Mungu ndani na nje ya Tanzania. Kwa njia hii, wanaendelea kumuenzi Bikira Maria katika dhamana ya kumpeleka Kristo Yesu kati ya watu wa mataifa.

Akizungumza katika sherehe hii, Humphrey Kira, Rais wa Radio Maria Tanzania ameiomba Serikali ya Tanzania kuangalia uwezekano wa kurekebisha sheria ya leseni ya Radio za Jamii ili ziweze kuwa na vituo vingi vya kurushia matangazao yake. Radio za Kikanisa zimekuwa mstari mbele katika kusaidia kukuza na kudumisha imani, maadili na utu wema miongoni mwa jamii. Ufinyu wa sehemu ya usikivu ni changamoto kubwa kwa Radio Maria nchini Tanzania. Amewashauri waamini pamoja na watanzania wenye mapenzi mema kuendelea kuitegea sikio Radio Maria kwani kwa sasa Radio Maria inaweza pia kusikika kwa njia ya simu za viganjani. Radio Maria kwa sasa ina vituo kumi na viwili nchini Tanzania.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.