2016-08-11 16:25:00

Mama Theresa wa Calcutta, Jembe la huruma ya Mungu!


Baba Mtakatifu Francisko hapo tarehe 4 Septemba 2016, majira ya saa 4:30 kwa saa za Ulaya anatarajiwa kuadhimisha Ibada ya Misa Takatifu na kumtangaza Mama Theresa wa Calcutta kuwa ni Mtakatifu. Ibada hii itakuwa pia ni sehemu ya maadhimisho ya Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu kwa watu wanaojitolea na wale wanaoendelea kujitaabisha kumwilisha matendo ya huruma: kiroho na kimwili kwa watu mbali mbali duniani.

Mama Theresa wa Calcutta ni muasisi wa Shirika la Wamissionari wa Upendo, maarufu kama Watawa wa Mama Theresa wa Calcutta, ni mwanamke wa shoka aliyesimama kidete kutangaza na kushuhudia Injili ya huruma ya Mungu ikimwilishwa katika maisha ya maskini na wale wote waliokuwa wanasukumizwa pembezoni mwa jamii. Kwa njia ya huduma makini inayofumbatwa katika moyo wa huruma na mapendo, watu wengi waliweza kuonja huruma ya Mungu katika maisha yao hata leo hii bado wanaendelea kumkumbuka Mama Theresa wa Calcutta, Mtakatifu wa huruma ya Mungu. Kardinali Angelo Comastri, Mhudumu mkuu wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican katika kitabu chake “Mimi nimemfahamu Mtakatifu”, kilichochapishwa hivi karibuni anakiri kwamba, kila mara alipokuwa anabahatika kukutana na Mama Theresa wa Calcutta, alikuwa anapata amani na utulivu ndani mwake, ilikuwa kama ni dirisha la tabasamu ya Mungu kwa binadamu anayeogelea katika dimbwi la mahangaiko mbali mbali ya maisha.

Kardinali Comastri anasema, mara ya mwisho kukutana na kuzungumza na Mama Theresa wa Calcutta ilikuwa  nitarehe 22 Mei 1997, akiwa mgonjwa na hapo mtu angeweza kugundua kwamba, Mama Theresa alikuwa amebakiza siku chache kabisa za kumwilisha huruma ya Mungu kwa maskini hapa duniani, tayari kujiunga na Muumba wake, ili aweze kumkirimia taji ya ushindi baada ya kujisadaka bila ya kujibakiza katika mchakato wa kushuhudia Injili ya huruma ya Mungu, kipimo ambacho Mwenyezi Mungu atakitumia kwa ajili ya kuwahukumu watu siku ile ya mwisho.

Kardinali Comastri anafafanua kwamba, alipokuwa anazungumza na Mama Theresa wa Calcutta alimshirikisha kwamba, Mama yake mzazi alikuwa amefariki siku chache tu zilizokuwa zimepita na kumfariji kwa maneno kwamba, Mama yake alikuwa amemwacha kimwili hapa duniani, lakini yuko karibu naye zaidi huko mbinguni. Akamwambia hata mimi ninajiandaa kwenda mbinguni, nitakuwa nawe karibu zaidi; maneno ambayo yameacha chapa ya faraja ya kudumu katika moyo wake.

Kardinali Comastri anasema, watakatifu mbinguni hawana haja ya kushangiliwa sana kama alivyowahi kusema Mtakatifu Yohane Paulo II, bali wanachotaka kutoka kwa waamini wanaosafiri huku bondeni kwenye machozi ni kufuata nyayo zao, ili hata wao waweze kuwa watakatifu na wakamilifu kama Baba yao wa mbinguni alivyo mkamilifu. Mama Theresa wa Calcutta daima aliwahimiza waamini kuchuchumilia utakatifu wa maisha na kwamba, hii ndiyo amana wanayopaswa kuisimamia kidete katika mchakato wa maisha yao hapa duniani, mengine yote yanapita tena ni ubatili mtupu kama anavyosema Mhubiri.

Maisha ya mwanadamu hapa duniani anasema Mama Theresa wa Calcutta yanapaswa kusheheni matendo ya huruma kwani huu ni wakati wake na kwamba, yatamsaidia mwamini katika safari yake ya mbinguni. Ikumbukwe kwamba, sanda kamwe haina mfuko! Maisha ya sala ndiyo siri kubwa ya mafanikio katika maisha na utume wa Mama Theresa wa Calcutta. Ni mwanamke wa shoka na mtawa aliyebahatika kuzungumza kwenye Baraza kuu la Umoja wa Mataifa.

Wakati huo, Katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa Bwana Pèrez de Cuèlla alipokuwa anamtambulisha Mama Theresa wa Calcutta kwa wajumbe wa Baraza kuu la Umoja wa Mataifa alisikika akisema “Ninapenda kuwatambulisha mwanamke jasiri duniani, kwani moyo wake umesheheni maskini wa dunia hii. Lakini Mama Theresa wa Calcutta kwa unyenyekevu  mkuu alijibu akasema, “mimi hapa ni mtawa ninayesali tu nikimwomba Yesu aweze kunijalia upendo moyoni mwangu, ili niweze kuwashirikisha na kuwamegea maskini ninaokutana nao katika hija ya maisha yangu”.

Mama Theresa wa Calcutta kwa macho makavu kabisa bila woga wala makunyanzi akawaambia wajumbe wa Baraza kuu la Umoja wa Mataifa “hata ninyi salini, hivyo mtaweza kugundua maskini wanaowazunguka pembeni mwenu, hata pengine ni kati ya jirani zako! Mama Theresa alijenga utamaduni wa kuabudu Ekaristi Takatifu na huko akajichotea ari, nguvu na moyo mkuu wa kuweza kutangaza na kushuhudia Injili ya huruma na mapendo iliyokuwa inabubujika kutoka kwa Kristo na Kanisa lake. Kwake, Ibada ya Misa takatifu ilikuwa ni chanzo na hatima ya maisha na utume wake miongoni mwa maskini na wale wote waliokuwa wanadharauliwa na jamii, akawa na ujasiri wa kuwainua tena ili kukuza na kudumisha utu wao kama watoto wapendwa wa Mungu!

Mama Theresa wa Calcutta alikuwa na urafiki wa pekee na Malkia Diana wa Uingereza ambaye kwake alikuwa ni mtu wa kawaida ambaye alikuwa na mateso pamoja na machungu mengi moyoni mwake. Hii inaonesha kwamba, Mama Theresa wa Calcutta alikuwa na uwezo wa kujishusha na kuguswa na mahangaiko ya watu wote pasi na ubaguzi, kwani wote hawa aliwatambua kuwa ni watoto wapendwa wa Mungu.

Mama Theresa anasema, aliweza kupata ujasiri wa kuwahudumia maskini na wagonjwa waliokuwa kufani kutokana na nguvu na ujasiri aliojichotea katika sala na tafakari ya Neno la Mungu. Bila msaada na neema ya Mungu ni vigumu sana kuweza kujisadaka bila ya kujibakiza kwa ajili ya huduma kwa maskini na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii. Huduma ya kweli kwa maskini ni ile inayopata chimbuko lake katika maisha ya sala na adhimisho la Fumbo la Ekaristi Takatifu.

Mama Theresa wa Calcutta alitangazwa kuwa Mwenyeheri na Mtakatifu Yohane Paulo II; mtume amini wa huruma ya Mungu kwa watu wa nyakati hizi; Mama Thereza wa Calcutta anatangazwa kuwa Mtakatifu na Papa Francisko wakati huu Mama Kanisa anapoadhimisha Jubilei ya Mwaka Mtakatifu wa huruma ya Mungu, kielelezo makini kwamba, Mama Theresa wa Calcutta kweli amekuwa ni chombo na shahidi wa huruma ya Mungu kwa watu wa nyakati hizi.

Ni mtawa aliyekuwa na furaha katika maisha yake kwani mikono yake ilibahatika kupangusa machozi ya watu waliokuwa wanateseka: kiroho na kimwili; akabahatika kufunga macho ya wagonjwa waliokuwa kufani kwa huruma, imani, mapendo na matumaini kwa Kristo Yesu aliyemwaga damu yake azizi kwa ajili ya kumkomboa mwanadamu kutoka katika lindi la dhambi na mauti! Mama Theresa wa Calcutta anakuambia hata wewe ndugu msikilizaji wa Radio Vatican ukitaka kuwa na macho na moyo wenye furaha jisadake kuwasaidia na kuwahudumia maskini! Hii ndiyo siri ya urembo na mafanikio katika maisha!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.

 

 








All the contents on this site are copyrighted ©.