2016-08-09 15:17:00

Padre James Yarrot anasherehekea Jubilei ya miaka 25 ya Upadre!


Maadhimisho ya Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu yanaonesha kwa namna ya pekee jinsi ambavyo Mwenyezi Mungu anavyojitaabisha ili kumshirikisha mwanadamu huruma na upendo wake usiokuwa na mipaka. Mwenyezi Mungu anataka kuwaona watu walioumbwa kwa sura na mfano wake wakiwa na afya njema na furaha inayobubujika kutoka katika Fumbo la Utatu Mtakatifu, kwa kuoneshana na kuonjeshana huruma. Huruma ni msingi thabiti wa uhai wa Kanisa na kwamba, ushuhuda wenye mvuto na mashiko unafumbatwa katika huruma ya Mungu. Huruma ni chachu makini ya Uinjilishaji mpya anasema Baba Mtakatifu Francisko.

"Iweni na huruma" ndiyo changamoto inayotolewa kwa namna ya pekee kwa Mapadre ambao kimsingi ni vyombo na mashuhuda wa huruma ya Mungu kwa njia ya Mafumbo wanayoadhimisha kwa niaba ya Mama Kanisa. Padre James Yarrot  kutoka Jimbo Katoliki Mbulu, Tanzania anaadhimisha Jubilei ya miaka 25 ya Upadre. Katika kipindi chote hiki, amekuwa ni Mhudumu wa Neno la Mungu, Sakramenti za Kanisa na matendo ya huruma yanayofumbatwa katika shughuli na mikakati ya kichungaji. Jubilei hii ni mwaliko kwa Padre Yarrot kukumbuka kwamba, ameteuliwa kati ya watu kwa ajili ya mambo matakatifu na kwamba, amewekwa wakfu ili kuwa ni chombo cha huruma ya Mungu kwa watu wake.

Katika mahubiri ya Ibada ya Misa Takatifu kwa ajili ya kumpongeza Padre James Yarrot kwa kutimiza Miaka 25 ya Upadre, kumbu kumbu inayokwenda sanjari na Maadhimisho ya Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu, Padre John Almas amemshukuru Mungu kwa karama na mapaji aliyomkirimia Padre Yarrot katika maisha na utume wake kama Padre hasa zaidi huduma kwa wagonjwa, moja ya matendo ya huruma kimwili.

Ni Padre ambaye ameonesha ukomavu wa imani, mapendo na matumaini na kwamba, daima amejitahidi kuwa ni chombo cha huruma, msamaha na upatanisho kati ya watu, ili waweze kuonja tena ndani mwao, huruma, msamaha na upendo wa Mungu uliofunuliwa kwa njia ya Fumbo la Pasaka, yaani mateso, kifo na ufufuko wa Kristo Yesu. Waamini nao wametakiwa kuwa mstari wa mbele katika ujenzi wa Ufalme wa Mungu unaojikita katika haki, amani, upendo na mshikamano wa dhati, tayari kudhihirisha imani yao inayomwilishwa katika matendo ya huruma.

Na Sr. Edith Temu.

Jimbo Katoliki Mbulu, Tanzania.








All the contents on this site are copyrighted ©.