2016-08-08 11:45:00

Uchaguzi mkuu Zambia! Kumekucha!


Familia ya Mungu nchini Zambia inategemea kufanya uchaguzi mkuu hapo tarehe 11 Agosti 2016 katika haliĀ  ya upinzani mkali kati ya Chama tawala na vyama vingine vya upinzani. Lakini viongozi wa Baraza la Makanisa nchini Zambia linawataka wananchi wote kuhakikisha kwamba, wanafanikisha mchakato wa uchaguzi mkuu ili Zambia iweze kuendelea kubaki kuwa ni kisiwa cha amani kabla, wakati na baada ya uchaguzi mkuu.

Serikali kwa upande wake inapaswa kuwajibika ili uchaguzi uweze kuwa huru na wa haki na hivyo kuwapatia wananchi wa Zambia viongozi watakaosaidia kusukuma mbele gurudumu la maendeleo ya watu wao. Uchaguzi mkuu unaweza kupata mafanikio yanayokusudiwa ikiwa kama raia wenye haki ya kupiga na kupigiwa kura watatekeleza dhamana na wajibu wao barabara anasema Dr. Peggy Mulambya Kabonde, Katibu mkuu wa Baraza la Makanisa Zambia.

Zambia inapaswa kuwa ni mfano bora wa kuigwa kwa kuondokana na vurugu za uchaguzi kabla, wakati na baada ya mchakato mzima wa uchaguzi mkuu. Ikumbukwe kwamba, wakati wa kampeni za uchaguzi kuna matukio ambayo yalipelekea uvunjifu wa misingi ya haki, amani na maridhiano kati ya watu kati ya Chama tawala na vyama vya upinzani. Wananchi wa Zambia wanafanya uchaguzi ili kupata viongozi wa Serikali za mitaa, wabunge na Rais pamoja na kupiga Kura ya Maoni kuhusu Katiba.

Baraza la Makanisa nchini Zambia linasema, linaendelea kuunga mkono juhudi za kudumisha misingi ya haki, amani na utulivu nchini Zambia na kwamba, binadamu wote ni sawa mbele ya Mungu na hakuna mtu anayeweza kujigamba kuwa yeye ni bora kuliko Wazambia wengine wote. Wananchi wa Zambia hawana budi kujenga na kudumisha utamaduni wa upendo, umoja na mshikamano wa kitaifa. Ikumbukwe kwamba, uchaguzi mkuu ni suala la siku moja, lakini misingi ya haki, amani na utulivu ni nyenzo muhimu sana katika mchakato wa maendeleo kiroho na kimwili.

Wananchi wa Zambia wanapaswa kuendelea kuwa wameshikamana hata baada ya uchaguzi mkuu kwa kuhakikisha kwamba, wanawekeza kwa ajili ya ustawi na maendeleo endelevu ya wananchi wengi za Zambia. Vyama vya siasa vitakuja na kupita, lakini uzalendo, umoja na upendo ni masuala mtambuka. Baraza la Makanisa Ulimwengu linaendelea kuwaombea wananchi wa Zambia ili amani, utulivu, umoja na mshikamano wa kitaifa viweze kutawala wakati wote wa mchakato wa uchaguzi mkuu.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.