2016-08-08 09:45:00

Ruksa kuvaa hijabu darasani!


Mahakama kuu ya rufaa nchini Nigeria imetoa ruhusa kwa wanafunzi wa kike wa dini ya Kiislam kuvaa hijabu kuanzia shule ya msingi hadi sekondari. Lakini hapo awali walikuwa wamezuiliwa ili kudumisha uhuru wa kuabudu na umoja wa kitaifa, amri iliyokuwa imetolewa na mahakama moja nchini Nigeria kunako Oktoba 2014, hukumu ambayo ilipingwa na waamini wa dini ya Kiislam. Kwa wakati huo wanafunzi wote bila kujali imani na dini zao, walitakiwa kuvaa sare moja iliyotambuliwa na shule husika.

Baadhi ya waamini wa dini ya Kiislam wanadai kwamba, kuwakataza kuvaa hijabu ni kuwanyima uhuru wa kidini, kuabudu na kujieleza. Mahakama kuu ya Nigeria imeridhia matakwa ya waamini hawa na kutoa kibali kwa wanafunzi kuanzia shule ya msingi hadi sekondari mjini Lagos, Nigeria kuvaa hijabu. Bi Saheed Ashafa, Rais wa Chama cha Wanafunzi wa Dini ya Kiislam nchini Nigeria ni ushindi wa dini ya Kiislam na Waislam wenyewe.

Hukumu hii itakata mzizi wa fitina ya nyanyaso walizokuwa wanafanyiwa wasichana wa dini ya Kiislam nchini Nigeria kutokana na uamuzi wa kuvaa hijabu wakati wanapokuwa shuleni. Wachunguzi wa masuala ya kimataifa wanasema, uamuzi huu unaweza kuvuruga umoja na mshikamano wa kitaifa kwa misingi ya udini usiokuwa na mvuto wala mashiko!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.