2016-08-06 15:32:00

Wekeza kwa Mungu na kesha katika imani kwa Kristo Yesu!


Dominika ya 19 ya mwaka inatualika kuitafakari fadhila ya imani kama nyenzo muhimu ya udumifu wetu katika uaminifu wetu kwa Mungu. Fadhila hiyo inajitokeza kama hekima ya Mungu katika somo la kwanza na mwandishi katika Waraka kwa Waebrania anaielezea kuwa ni “hakika ya mambo yatarajiwayo, ni bayana ya mambo yasiyoonekana”. Somo la Injili linatuhakikishia faida za kuwekeza katika Mungu: Ifanyieni mifuko isiyochakaa, akiba isiyopungua katika mbingu, mahali pasipokaribia mwivi, wala nondo haharibu”. Akiba hii haipungui kwa sababu Mungu wetu ni mwenye haki na mwaminifu daima. Yeye humlipa kila mmoja sawasawa na alivyojiwekea na unapowekeza kwake ni kuendelea kukua na kuimarika katika utu. Akiba hii haichakai kwa sababu Mungu wetu upendo wake mkuu ni wa milele (Rej Zab 136:1). Upendo wa Mungu hauna tarehe ya mwisho ya matumizi na upendo huo hufanyika upya kila siku.

Imani ya Babu yetu katika imani Ibrahimu ilijikita katika kuutazama na kuukumbatia mpango wa Mungu. “Maana alikuwa akiutazamia mji wenye misingi, ambao mwenye kuubuni na kuujenga ni Mungu”. Hii inamaanisha kwamba, imani inapaswa kutuelekeza katika kuyatafuta na kuyatekeleza yaliyo mapenzi ya Mungu. Sisi wanadamu tunapaswa kufurahia kuyatimiza mapenzi ya Mungu. Katika sala ya Baba yetu tunasema: “utakalo lifanyike duniani kama mbinguni”. Kabla ya kutekeleza mpango wowote hapa duniani tunapaswa kujitafakari na kuona kama kweli ni mpango wa Mungu au la. Mpango wa Mungu daima unanuia mema na hivyo dalili za mpango wa Mungu huonekana katika nia ya kujenga undugu, ushirikiano, juhudi za kupatanisha, kuwasaidia wenye mahitaji na mengineyo mengi ambayo yanaendelea kumtukuza Mungu na kuufanya ubinadamu kuendelea kufarijika.

Ulimwengu wa leo ambao unajitahidi kwa namna nyingi kumtoa mwanadamu katika tunu hii njema unatuelekeza katika shimo. Ni ulimwengu ambao hautupatii nafasi ya kuimarisha imani yetu, yaani kuweka hazina yetu kwa Mungu. Ni ulimwengu ambao unafanya juhudi ya kuuondoa moyo wa mwanadamu kutoka kwa Mwenyezi Mungu na hivyo kuondoa paji la imani. Matokeo yake unakuwa ni ulimwengu unaozidi kujenga ukuta kati ya watu na watu. Ni ulimwengu ambao unawatambua wenye mali na wasio nazo, wenye kipaji hiki na walionyimwa kile, wenye karama hii na wenye karama ile na hivyo kuwatenga kila mmoja kwa namna yake. Haya kwa hakika si mapenzi ya Mungu na matokeo yake ni balaa kwa ubinadamu badala ya baraka. Tutaendelea kushuhudia vita na mafarakani, unyonyaji na ukoloni mambo leo hata kama tutajidai kutaka kuujenga ulimwengu katika hali ya umoja. Umoja huo ni bandia kwani umoja usiojengwa katika Mungu unakosa kiungo chake muhimu na daima huwa ni kama mkusanyiko tu wa kundi la watu ambao kila mmoja hujitafutia yake.

“Viuno vyenu na viwe vimefungwa, na taa zenu ziwe zinawaka; nanyi iweni kama watu wanaomngoja bwana wao atakaporudi kutoka harusini, ili atakapokuja na kubisha, wamfungulie mara”. Kuwekeza kwa Mungu kunatudai udumifu. Uaminifu wetu kwa Mungu si suala la muda tu na hasa pale tunapotafuta fadhila kwake. Hii ni taadhari ya kuepuka upendo wa nipe nikupe, upendo ule ambao ni wa kibinafsi, upendo ambao unawaka wakati tu mmoja anapohitaji kutimiziwa yake. Mifano ya Wazee wetu wa imani Abrahamu na mkewe sara inatuonesha njia. Walipitia hali ngumu pengine hata kunyanyapaliwa na jamii kwa sababu walikosa mtoto lakini upendo wao kwa Mungu uliendelea, waliendelea kumtumaini Mungu kwa sababu ya imani yao thabiti. Mipango ya Mungu si ya mwanadamu na njia zake si njia zetu. Tunaalikwa kubaki daima waaminifu kwake kusudi wakati ufaao ambao kadiri ya mipango yake fadhili zake zitatupitia tukutwe tupo waaminifu kwake.

Ni nafasi ya kujitafakari kwamba tumewekeza wapi leo hii? Tunakesha wapi leo hii? Tunakesha kusubiri nini? Tunayo hakika kwamba Bwana atarudi lini? Kukesha kwetu kunapata nguvu na uelewa wetu wa imani yetu juu ya huyo tunayemkeshea. Kujitajirisha kwetu katika elimu ya Mungu kwa njia ya sala, tafakari na matendo mema ndiko kutatupeleka katika kumwelewa zaidi mwenyezi Mungu na kujitegemeza kwake kwa imani. Hauwezi kuvuna zabibu katika michongoma. Mtu ambaye hajishughulishi katika kuitafuta elimu ya Mungu ndani ya moyo wake na akili zake ni aghalabu kumwelewa Mungu na kuwekeza katika yeye. Hapa tunagutushwa kuwa na taadhari na ulimwengu huu wa leo ambao unajitahidi kuiondoa elimu ya Mungu kutoka miongoni mwa wanajamii. Wale wanaohusika kwa nafasi ya pekee na malezi ya awali ya ubinadamu, mathalani wazazi, walimu na viongozi wa dini wanapaswa kujibidisha katika kuepa mwelekeo huo kwa maana kile tutakachowajengea watoto wetu ndicho kitawapatia hazina yao.

Kubaki katika udumifu huu inahitajika hekima ya kimungu. Hekima hii ni paji la Roho Mtakatifu ambalo hutusaidia kujua maana ya kila sauti. Katika somo la kwanza tunaambiwa kwamba hekima hiyo inatuonya: “usiku ule Baba zetu walitangulia kuonywa, ili wakiwa na ufahamu hakika, wafurahishwa na viapo walivyovitegemea; kwa hiyo watu wote waliutazamia wokovu wa wenye haki na uharibifu wa adui”. Hekima ya Mungu hutusaidia kudumu katika imani yetu kwa Mungu kwa sababu inatufunulia maana ya matukio mbalimbali ya kimaisha na kutuonesha njia. Inatuonesha ubatili wa kutegemea mali za kiulimwengu ambazo hupita tu na mwisho inatuonesha ukuu wa Mungu na umilele wa upendo wake kwetu. Hekima ya Mungu itatukumbusha kuendelea kumwabudu Mungu daima na hivyo kuendelea kupokea fadhili zake. Hii ni kwa sababu tunapowekeza kwa Mungu “wala nondo hawaharibu na mwivi hawezi kupakaribia.

Leo hii tutambue umuhimu wa paji hili la imani na kuomba hekima ya Mungu ili tuendelee kukesha katika uaminifu wetu kwa Mungu. Tuwekeze kwa Mwenyezi Mungu kwa kuwa Yeye daima ni mwaminifu na Upendo wake mkuu ni wa milele. Hekima yake ituongoze ili tuweze kuyatambua mapenzi yake na mithili ya Mama yetu Bikira Maria daima tuitikie: “Tazama mimi ni mtumshi wa Bwana na iwe kwangu kama ulivyonena”.

Kutoka Studio za Radio Vatican mimi ni Padre Joseph Peter Mosha.








All the contents on this site are copyrighted ©.