2016-08-06 15:58:00

Usiwekeze kwenye madafu utapanda pipa la msiba!


Mtu mmoja amefuatilia historia ya thamani ya sarafu ya Tanzania amesema kwamba shilingi 100 “Mwaka 1962 iliweza kununua eka moja ya ardhi. Mwaka 1970 ilinunua nguo ya ndoto yako. Mwaka 1990 ilinunua mche wa sabuni. Mwaka 2000 ilitanikiwa kununulia paketi ya viberiti. Mwaka 2016 inatumika kwa kukwangulia vocha.” Kutokana na upembuzi huu mimi naona itakakapofika mwaka 2020 shilingi hiyo itafifia kama sungura iliyokuwa thumni au samaki iliyokuwa senti tano.

Pesa ya sasa ya Tanzania ina thamani ya kununulia madafu ndiyo maana inaitwa Pesa ya Madafu kama anavyoimba Jay Moe: “Pesa ya madafu: miamia ukizichanga changa unaweza kujenga nyumba ya ghorofa.” Pesa ya madafu kwa sababu huwezi kuitumia nje ya nchi. Unapotakiwa kutoka nje ya nchi inabidi kubeba Pesa ya madafu na kwenye ofisi maalumu inayoitwa Bureau de Change, na kununua pesa ngeni ili kutumia uendako. Pesa yako ya madafu inabaki nchini iendelee kutumika na wengine.

Ndugu zangu mali za duniani hapa ni kama Pesa ya madafu, zinatumika duniani hapa tu mwisho. Utakapotakiwa kuingia pipa la msiba na kupaa kwenda nchi ya ahadi unahitaji kwenda Bereau de Change na kununua pesa ya kigeni zinazotumika huko majuu ahera, kwa sababu huruhusiwi kuingia pipa na pesa ya madafu kama wasemavyo waswahili “sanda haina mifuko.” Lakini kwa sababu siku hiyo ya chek-in haijulikani, itakuwa ngumu sana hutapata muda wa kubadili mali yako. Leo utaelekezwa ofisi maalumu ya kubadilisha Pesa yako ya Madafu, na utaelekezwa pia namna ya kubadili. Tafadhali fanya haraka kubadili pesa yako kwani hujui lini utaingia pipa. Mimi sikutishi bali nakupa ushauri wa bure.

Juma lililopita Yesu alituangalisha kuhusu mkulima yule tajiri, aliyejichumia mali kutosha, na akaambiwa kuwa hiyo ni Pesa ya madafu tu, itabidi uiache kwani unatakiwa kuingia pipa usiku wa leo. Tukamshuhudia yule mtu jinsi alivyoenda zake akiziacha Pesa za madafu hivi hivi tu hapa duniani.

Leo Yesu anatupatia ushauri nasaha ili tuweze kuepukana na karaha hii mbovu katika maisha kama ya yule tajiri. Fasuli inaanza kwa kusema: “Msiogope, enyi kundi dogo, kwa kuwa Baba yenu ameona vema kuwapa ule ufalme.” Wanafunzi wa Yesu yaani wale wanaotaka kuingia katika ufalme huo ni kikundi kidogo tu. Yesu anawapa ushauri wa kubadili pesa anaposema: “Viuzeni mlivyo navyo, mtoe sadaka.” Isieleweke kuwa sasa tuanze mradi wa kuuza nyumba na kutoa kwa maskini, la hasha, bali Yesu anataka kusema kwamba mali yote mliyo nayo ni pesa za madafu tu, tena siyo zenu bali ni mali ya Mungu, ametoa kama mtaji tu wa kutumika hapa duniani, hivi yabidi zigawiwe kwa wote hasa wanaohitaji. Kwa hiyo kuuza, maana yake ni kugawa kwa wengine.

Kisha Yesu anatuelekeza mbinu za kuzibadili na kuziweka kwenye masanduku yanayoweza kupita kwenye check-in na kuingia nazo mbinguni anaposema: “Jifanyieni mifuko isiyochakaa, akiba isiyopungua katika mbingu, mahali pasipokaribia mwivi, wala nondo haharibu. Kwa kuwa hazina yenu ilipo, ndipo itakapokuwpo na mioyo yenu.”  Hazina maana yake ni kile tunachokijali katika maisha yetu. Chemchemi ya msingi ya maisha yetu hutegemea hazina ambayo kila afanyacho mtu hujikitika. Kwa hiyo kwa njia ya mifano mitatu Yesu anatuonesha hazina au pesa inayotumika ugenini ambako ni mbinguni na mbinu ya kuinunua tukiwa bado hapahapa duniani:

Mosi, kuhusu Bwana yule aliyeenda arusini akiwaachia watumishi wake, mali yake. Watumishi walishajua kwamba siku moja bwana wao atarudi, lakini hawakujua muda atakaorudi. Kwa hiyo iliwabidi waitunze vyema mali hiyo. Mazingira haya ya watumishi ni taarifu kwetu kwamba yatubidi kujiandaa kubadili pesa ya madafu. Yesu anasema jiangalieni au kesheni. Hili neno kujiangalia siyo la kututisha, bali ni anatutaka tuwe tayari na kujua kwamba Bwana atakapokuja atukute kila tumeshabadili pesa tayari kwa safari.

Kisha Yesu anatuingiza polepole kwenye ofisi ya kubadili madafu na namna ya kuzipata hazina hizo ngeni. Anaonesha picha mbalimbali za mtumishi anayejiandaa anaposema: “Viuno vyenu na viwe vimefungwa” yenye maana pia ya kujikwinda, au kufunga kibwebwe au Kufunga sawasawa skapulari ili uweze kufanya kazi kwa uhuru, bila kizuizi hasahasa kama kazi hiyo ni ya kutumikia wengine kama vile kugawa chakula na vinywaji. Kumbe picha hii ya kufunga viuno inamaanisha kutumikia. Hivi Bwana atakapofika atukute tunatumikiana.

Pili, Yesu anasema: na taa zenu ziwe zinawaka. Taa inasaidia kuangalia. Kwa hiyo mtumishi daima anahitaji mwanga wa taa muda wote ili kuangalia mahitaji ya Bwana. Hapa Bwana ni sawa na kila mhitaji. Huyo mhitaji anaweza kukujia wakati wowote na kwa njia ya mtu yeyote yule. Kwa kufanya hivi maisha haya yanafanikiwa kadiri ya mapendekezo ya Yesu, yaani kutumikiana hasa kwa kumjali kila mtu hasa fukara. Kwa hiyo mfano wa kwanza wa kukesha unaishia kwa picha hii ya anayetumikia inabidi ajikwinde kumsubiri wa Bwana atakapofika.

Lakini katika ujio wa mwisho atakaporudi Bwana toka arusini  inasemwa:“Heri watumwa wale, ambao bwana wao ajapo atawakuta wanakesha.” Hapo yeye mwenyewe ndiye sasa atakayejikwinda vazi na kutumikia kama anavyosema: “Amin, nawaambieni, atajifunga na kuwakaribisha chakulani atakuja na kuwahudumia.” Hivi ndivyo Yesu anavyomwonesha mtu aliyefanikiwa katika maisha.  Mfano wa pili ni ule ambao Yesu anajionesha kama mwizi. “Lakini fahamuni neno hili: Kwamba mwenye nyumba angalijua saa atakayokuja mwivi, angalikesha, wala asingaliacha nyumba yake kuvunjwa. Nanyi jiwekeni tayari, kwa kuwa saa msiyodhani ndipo ajapo Mwana wa Adamu.” Picha hii ya mwizi inaweza kueleweka vibaya kwani inamwonesha Mungu kuwa mwizi anayenyemelea na kufika chigafula siku usiyojisahau na kukuhukumu kama hauko tayari. Kwa vyovyote Mungu atafika siku tusiyodhani, lakini hiyo isitutishe.

Hapa Yesu anatutaka tujiweke sawa katika kujiandaa juu ya wakati atakaofika tusioufahamu. Maana yake Yesu anafika kwa njia ya maskini na fukara. Hao wanaofika wakati tusiotegemea, wakati usio mzuri hasa pale tunaposema umefika chigafula yaani wakati usiodhani. Kumbe wewe kama mkristu huna budi daima kuwa tayari kumpokea Yesu anapofika katika vazi la fukara na maskini. Huyo ndiye mkombozi anayekukomboa kutoka katika kujilimbikizia mali ya ulimwengu huu, na anayetuokoa katika ulimwengu huu ni maskini na fukara. Kwa hiyo watu fukara na maskini, ni ofisi ya kubadili pesa na ndiye pesa ya kigeni ( hazina na lulu).

Mfano wa tatu, ni jibu kwa swali analotoa Petro. “Bwana mithali hiyo umetuambia sisi tu, au watu wote pia?” Mfano wa Yesu anapojibu swali la Petro, unahusu zaidi mbinu na utaratibu wa kubadili Pesa ya madafu kwa viongozi, yaani wale walio na majukumu katika jumuia, anaposema: “Ni nani, basi aliye wakili mwaminifu, mwenye busara, ambaye bwana wake atamweka juu ya utumishi wake wote, awape watu posho kwa wakati wake? Heri mtumwa yule, ambaye bwana wake ajapo atamkuta anafanya hivyo.” Yesu anapendekeza aina mbili za utaratibu kubadili pesa kwa viongozi.:

Utaratibu wa kwanza ni, kugawa vyema chakula (posho). Wahitaji na wenye njaa ni wengi. Viongozi ni wale wanaoangalia na kuwajali wale walio na njaa, na kuwasaidia kwa kuwagawia mali wakati wake. Kwa hiyo, viongozi wanaojali na kuwalisha chakula wenye shida hao ndiyo wanafanya mapenzi ya Mungu. Viongozi wanaofanya hivyo Yesu anawaambia: “Atamweka juu ya vitu vyake vyote.”

Utaratibu mwingine ni ule anaosema: “Lakini mtumwa yule akisema moyoni mwake, Bwana wangu anakawia kuja, akaanza kuwapiga wajoli wake wanaume kwa wanawake, akila na kunywa na kulewa; Bwana wake mtumwa huo atakuja siku asiyodhani na saa asiyojua, atamkata vipande viwili na kumwekea fungu lake pamoja na wasioamini.” Hapa tunataadharishwa wote kutojisahau na kupurukusha agizo hili la kubadili mali zetu. Kishawishi hiki kinaweza kuwakumba wote hasa wale walio katika mstari sahihi wa kubadili pesa yaani wale wanaokesha na kutumikia. Ingawaje wako katika njia sawa lakini wana hatari ya kujisahau. Wakati wa kutumikia wanaweza kujisahau kuketi mezani na wakaanza kudai na wenyewe kutaka kutumikiwa. Hatari hii inatukumba zaidi wakristu tunaomtumikia Kristu katika ngazi mbalimbali za uongozi. Tunaweza kujisahau na kufikiri kwamba Bwana anchelewa kufika, tunajidanganya kukaa kwenye kiti na kudai kuhudumiwa.

Mfano wa nne ni tahadhari kwa viongozi wanaomfahamu Kristu anasema: “anaojua mapenzi ya bwana wake, asijiweke tayari, wala kuyatenda mapenzi yake,” Yesu anaongea kwa ukali sana kwamba mtumishi huyo: “atapigwa sana.” Yesu amekerwa zaidi na viongozi wa jumuia anaposema mtu huyo “atamkata vipande viwili” kwa kigiriki ni hotomezei, maana yake, maisha ya watu hao yatakuwa yamegawanyika makundi mawili. Ule upande waliojidai kama mabwana utapotea, na ule upande wa maisha ya ya utumishi kwani ni pesa ngeni iliyoishabadilishwa itahifadhika mbinguni. Kwa hiyo Yesu anatutahadharisha sote anapotuambia: Muwe kama watu wanaomngonjea bwana wao, atakaporudi kutoka arusini, ili atakapokuja na kubisha wamfungulie mara.

Na Padre Alcuin Nyirend, OSB.








All the contents on this site are copyrighted ©.