2016-08-06 07:03:00

Timu ya wakimbizi huko Rio 2016 ni kilio cha amani na mshikamano!


Baba Mtakatifu Francisko ametuma salam na matashi mema kwa Timu ya Wakimbizi wanaoshiriki katika Michezo ya Olympic huko Rio de Janeiro, Brazil kwa mwaka 2016, mashindano ambayo yamefunguliwa rasmi Ijumaa, tarehe 5 Agosti 2016. Timu hii inaundwa na wanamichezo: Rami Anis, Yiech Pur Biel, James Nyang Chiengjiek, Yonas Kinde, Anjelina Nada Lohalith, Rose Nathike Lokonyen, Paulo Amotun Lokoro, Yusra Mardini, Popole Misenga na Yolande Bukasa Mabika.

Baba Mtakatifu katika ujumbe wake anasema, amefuatilia kwa makini kuhusu timu hii pamoja na mahojiano mbali mbali waliyoyafanya kwenye vyombo vya habari, ili kuweza kuwa karibu zaidi pamoja nao katika historia ya maisha na matumaini yao kwenye mashindano ya Olympic huko Rio de Janeiro. Baba Mtakatifu anawatakia heri na mafanikio mema katika mashindano haya, ili ujasiri na nguvu watakayoionesha wakati wa mashindano, isaidie kuwa ni kilio kwa ajili ya amani na mshikamano.

Baba Mtakatifu anasema, kwa njia ya wanamichezo wakimbizi, Jumuiya ya Kimataifa itambue kuwa, amani ni jambo linalowezekana na kwamba kwa njia ya amani, kila jambo ni ushindi, lakini kwa vita kila kitu kinapotea. Ushiriki wa wakimbizi hawa uwe ni ushuhuda na mafao kwa kila mtu. Baba Mtakatifu anasema kwamba, anawaombea na anawaomba pia kumkumbuka katika sala na sadaka yao katika maisha na utume wake kama Khalifa wa Mtakatifu Petro.

Wakati huo huo, Shirika la Kuhudumia Wakimbizi la Umoja wa Mataifa, UNHCR, limepokea kwa mikono miwili tamko la Kamati ya Olympic Kimataifa, COI kuhusu ushiriki wa wakimbizi katika michezo ya Olympic kwa mwaka huu huko Rio de Janeiro. Hawa ni wakimbizi wanaotoka Syria, DRC, Ethiopia na Sudan ya Kusini. Ushiriki wa wakimbizi ni changamoto kubwa ya matumaini kwa wakimbizi wakati huu ambapo Jumuiya ya Kimataifa inashuhudia wimbi kubwa la wakimbizi na wahamiaji likitafuta hifadhi na usalama wa maisha yake.

Takwimu zinaonesha kwamba, hadi kufikia mwishoni mwa Mwaka 2014 idadi ya wakimbizi na wahamiaji duniani ilikuwa imevuka watu millioni 59.5 na kwamba, idadi hii inaendelea kuongezeka siku kwa siku. Shirika la Kuhudumia Wakimbizi la Umoja wa Mataifa linazitaka Serikali mbali mbali kuhakikisha kwamba, zinatoa huduma ya elimu kwa watoto wakimbizi ili kuwajengea matumaini ya leo na kesho iliyo bora zaidi kwa njia ya elimu makini; pamoja na kuzikirimia familia za wakimbizi malazi bora zaidi na fursa ya kazi pale inapowezekana pamoja na kuwapatia fursa ya kuweza kujifunza mambo mapya wanapokuwa uhamishoni. Mawazo haya yanatarajiwa kuwasilishwa kwenye mkutano mkuu wa Umoja wa Mataifa utakaojadili kuhusu changamoto ya wakimbizi, hapo Septemba, 2016 huko New York, Marekani.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.