2016-08-06 12:07:00

Askofu mkuu Pennacchio ateuliwa kuwa Balozi wa Vatican nchini Poland


Baba Mtakatifu Francisko amemteua Askofu mkuu Salvatore Pennacchio kuwa Balozi mpya wa Vatican nchini Poland. Hadi kuteuliwa kwake, Askofu mkuu Pennacchio alikuwa ni Balozi wa Vatican nchini India na Nepal. Itakumbukwa kwamba, Askofu mkuu Pennacchio alizaliwa tarehe 7 Septemba 1952 huko Napoli, Kusini mwa Italia. Baada ya masomo na majiundo yake ya Kikasisi, akapadrishwa kunako tarehe 18 Septemba 1976 kwa ajili ya Jimbo Katoliki la Aversa.

Kunako tarehe 28 Novemba 1998 akateuliwa na Papa Yohane Paulo II kuwa Balozi wa Vatican nchini Rwanda na kumpandisha hadhi ya kuwa Askofu mkuu na kuwekwa wakfu na Papa Yohane Paulo II kunako tareh 6 Januari 1999. Kunako mwaka 2003 akateuliwa kuwa ni mwakilishi wa Vatican huko Thailand, Singapore, Cambodia pamoja na kuwa ni mwakilishi wa kitume huko Birmania, Laos, Malaysia na Brunei. Kunako mwaka 2010 Baba Mtakatifu mstaafu Benedikto XVI akamteuwa kuwa Balozi wa Vatican nchini India na Nepal.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.