2016-08-05 15:45:00

Rio 2016! Jihadharini na biashara ya binadamu na utumwa mamboleo!


Mashirika ya Kitawa na Kazi za Kitume nchini Brazil, yanawataka wanamichezo pamoja na mashabiki mbali mbali kuhakikisha kwamba, wanalinda: maisha, utu na heshima ya binadamu aliyeumbwa kwa sura na mfano wa Mungu. Wanawataka wanamichezo kucheza kwa ajili ya maisha na kuondokana na kishawishi cha utumwa mamboleo na biashara haramu ya binadamu; mambo ambayo kwa bahati mbaya yanaambatana pia na mashindano makubwa ya kimataifa.

Kunako mwaka 2014 wakati wa Mashindano ya Kombe la Dunia, kutokana na kampeni ya uragibishaji dhidi ya utumwa mamboleo, zaidi ya asilimia 42% ya kesi za utumwa mamboleo zilitolewa taarifa na wahusika kushughulikiwa na vyombo vya sheria. Kampeni hii inaongozwa na mtandao wa kimataifa wa watawa dhidi ya biashara haramu ya binadamu unaojulikana kama “Talitha Kum”.

Lengo kuu ni kuwahabarisha wananchi wa Brazil hatari iliyoko mbele yao ikiwa kama hawatakua makini kutokana na wimbi kubwa la watu wanaokusanyika nchini humo kwa ajili ya mashindano ya 31 ya Michezo ya Olympic kwa mwaka 2016. Wananchi wasikubali kunyanyaswa kijinsia kwa kutumbukizwa katika utumwa mamboleo na biashara haramu ya binadamu; mambo ambayo ni kinyume kabisa cha utu na heshima ya binadamu.

Kamwe, binadamu wasigeuzwe kuwa kama bidhaa sokoni, kwani wana utu na heshima yao, daima wasimame kidete kulinda, kutetea na kudumisha Injili ya maisha dhidi ya utamaduni wa kifo! Baba Mtakatifu Francisko aliwahi kusema, utumwa mamboleo na biashara haramu ya binadamu ni uhalifu dhidi ya ubinadamu unaoacha makovu ya kudumu katika maisha ya watu. Mtandao wa kimataifa wa Talitha Kum unatekelezwa na mtandao uliogawanyika katika makundi 26 yanayofanya kazi kwa sas anchini Brazil.

Mtandao unawahamasisha wananchi kutoa taarifa kwa vyombo vya ulinzi na usalama na viongozi wahusika wanapaswa kuchukua hatua makini ili kudhibiti vitendo hivi vinavyodhalilisha utu na heshima ya binadamu. Mtandao huu unatekeleza dhamana na wajibu wake kwa njia ya mitandao ya kijamii, ili kuweza kuwafikia walengwa wengi zaidi pamoja na elimu makini kwa vijana wa kizazi kipya, ambao wengi wao wako hatarini kutumbukizwa katika biashara haramu binadamu na utumwa mamboleo.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.