2016-08-05 14:32:00

Jengeni na wekeni nia ya kusamehe na kusahau!


Baba Mtakatifu Francisko alipotembelea Kikanisa cha Porziuncola, kilichoko Mjini Assisi, Italia, Alhamisi, tarehe 4 Agosti 2016 alipata nafasi ya kusali katika hali ya ukimya kwa kitambo kirefu. Alipotoka nje ya Kikanisa alikutana na umati mkubwa wa waamini pamoja na watu wenye mapenzi mema wakiwa wanamsubiri kwa hamu. Baba Mtakatifu akawaonea huruma na kuwashukuru kwa moyo wa upendo na ukarimu waliomwonesha kwa kutaka kuwa karibu zaidi naye.

Baba Mtakatifu amewataka waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema kujenga na kudumisha utamaduni wa kusamehe na kusahau! Hata pale inapokuwa ni vigumu kukaribiana, lakini waoneshe ile nia njema ya kusamehe na kusahau! Watambue kwamba, Mwenyezi Mungu anapenda kuwasamehe daima wanapomkimbilia kwa moyo wa toba na wongofu wa ndani; lakini msamaha huu, utaweza kuwa na maana ikiwa kama hata wao watajitahidi kuwasamehe wale waliowakosea.

Baba Mtakatifu anakaza kusema, kila mtu ana kiu ya msamaha na hakuna awaye yote anayeweza kujigamba kwamba, hana haja ya msamaha. Kabla ya kuondoka na kurejea tena mjini Vatican, Baba Mtakatifu alipata nafasi ya kuwasalimia waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema waliokuwa mbele ya Kanisa kuu la Bikira Maria wa Malaika mjini Assisi na kuwataka kusimika maisha yao katia msamaha.

Wakati huo huo, Dr. Greg Burke, Msemaji mkuu wa Vatican anafafanua kwamba, hija ya Baba Mtakatifu Francisko mjini Assisi imejikita kwa namna ya pekee katika huruma na msamaha; fadhila ambazo zimeshuhudiwa na Baba Mtakatifu mwenyewe kwa kukaa katika kiti cha huruma ya Mungu na kuanza kuwaungamisha waamini kwa kutambua kwamba, kila mtu ana kiu ya huruma na msamaha wa Mungu. Baba Mtakatifu amesalimiana pia na Imam wa mji wa Perugia, changamoto ya kuendeleza majadiliano ya kidini! Kimsingi, Baba Mtakatifu anasema, dunia ina kiu ya msamaha, hata kama wakati mwingine ni vigumu kuweza kusamehe na kusahau, lakini Mwenyezi Mungu daima ni mwingi wa huruma na mapendo, kwa wale wanaomkimbilia kwa toba na wongofu wa ndani anasema Dr. Burke, Msemaji mkuu wa Vatican kwa sasa.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.

 

 








All the contents on this site are copyrighted ©.