2016-08-04 14:17:00

Mwilisheni Injili ya Kristo: kwa kuhubiri, ushuhuda na upendo!


Baba Mtakatifu Francisko Alhamisi, tarehe 4 Agosti 2016 amekutana na kuzungumza na wajumbe wa mkutano mkuu wa Shirika la Wadominikani waliokuwa wanaongozwa na mkuu wa Shirika Padre Bruno Cadorè. Baba Mtakatifu amesema, hii ni siku maalum sana kwani Myesuiti amekuwa kati ya Wadominikani na jioni akawa kati ya Wafransikani katika kilele cha maadhimisho ya Jubilei ya miaka 800 ya Msamaha wa Assisi.

Mwaka huu ni maalum pia kwa Wadomenikani wanaoadhimisha Jubilei ya miaka 800 tangu Shirika hili lilipotambuliwa na Papa Onorio III na wamekuwa ni wadau wakuu katika maisha na utume wa Vatican na Kanisa katika ujumla wake, daima wakionesha uaminifu katika huduma yao hadi nyakati hizi. Miaka 800 ni kipindi cha kumbu kumbu ya imani, maandiko na tafakuri sanjari na umissionari, ushuhuda na utume wa upendo na huruma ya Mungu ambayo imemwilishwa katika sehemu mbali mbali za dunia, kwa kulirutubisha Kanisa na kulionesha njia ya ya kumwilisha Injili ya Kristo kwa: kuhubiri, ushuhuda na upendo.

Baba Mtakatifu anasema, hizi ni nguzo kuu msingi zinazotoa dira na mwongozo wa Shirika la Wadominikani kwa siku za usoni pamoja na kuendelea kupyaisha karama yao kwa kusoma alama za nyakati. Mwenyezi Mungu alimsukuma Mtakatifu Domeniko kuanzisha Shirika la Wahubiri, ili kuendeleza katika kutangaza habari Njema ya Wokovu hadi miisho ya dunia kwa kutafakari na kufundisha, lakini kwanza wao wenyewe wanapaswa kuinjilishwa na Mwenyezi Mungu ili waweze kupata nguvu ya kuinjilisha, dhamana inayojikita katika mahusiano ya dhati na Mwenyezi Mungu, ili kuzaa matunda yanayokusudiwa katika nyoyo za watu.

Baba Mtakatifu anakazia umuhimu wa elimu makini mintarafu masuala ya kitaalimungu yanayowawezesha kuukaribia na kuukumbatia ukweli, tayari kuwashirikisha watu wa Mungu. Mhubiri ni mtu anayetafakari kwa kina na mapana Neno la Mungu na maisha ya watu, ili watu waweze kumwelewa na hatimaye, kutangaza na kushuhudia Neno la Mungu kwa ufanisi mkubwa. Hapa Baba Mtakatifu anasema, Kanisa linawahitaji majaalimu waaminifu wa ukweli na mashuhuda jasiri wa Injili; wanaomwilisha Injili katika uhalisia wa maisha kwa kuwashirikisha wote pasi na kubagua. Ni watu wenye uwezo wa kuongeza Injili ya furaha katika ukweli kwa kuwasaidia watu kutambua kuwa wanapendwa na Mungu na kwamba wao ni lengo kuu la huruma ya Mungu.

Mtakatifu Dominiko aliwashauri wanashirika wake kujisadaka wakati wa kuhubiri, kwani alitambua kwamba dhamana hii ilikuwa inawawezesha Wadominikani kukanyaga maeneo matakatifu kama ilivyokuwa kwa Musa wakati aliposhuhudia kichaka kinawaka moto bila ya kuteketea. Hii inatokana na ukweli kwamba mhubiri anabeba ndani mwake mambo matakatifu na walengwa pia ni watakatifu. Waamini wanahaki ya kupokea Neno la Mungu katika ukamilifu wake na kushuhudiwa pia maisha ya wale wanaolihubiri.

Watakatifu wengi waliweza kupata mafanikio makubwa katika maisha yao kwani waliweza kuunganisha maisha na utume wao, lugha inayogusa sakafu ya maisha ya kiroho na wala haina vizingiti kwani inaweza kufahamika na wote. Wahubiri wanapaswa kuwa ni mashuhuda wa upendo na huruma ya Mungu katika maisha kwa kutambua kwamba, sehemu ya Fumbo la Mwili wa Kristo limekufa na linaendelea kuteseka, kielelezo cha Kristo aliye hai na anayeendelea kuteseka kwa kumpigia kelele mhubiri bila kumwachia nafasi ya kutulia.

Kilio cha maskini na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii kinawafanya viongozi wa Kanisa kutambua kwamba, kweli Yesu alikuwa na huruma na upendo kwa maskini. Baba Mtakatifu anasema, leo hii Kanisa limezungukwa na watu wanaoendelea kupiga kelele kwa kusema kwamba, wana kiu; wanataka kuonjeshwa udugu na huruma; mambo yanayopaswa kuingizwa katika mpango mkakati wa shughuli za kichungaji, tayari kujibu kilio cha watu hawa kwa kuwa na miundo mbinu muafaka ndani ya Shirika; tayari kuzima kiu ya watu wa Mungu. Kwa njia hii wataweza kuhubiri ukweli unaofumbatwa katika upendo na huruma ya Mungu.

Baba Mtakatifu anakaza kusema, kwa kukutana ana kwa ana na sehemu ya Fumbo la Mwili wa Kristo, wataweza kuinjilishwa na hatimaye kugundua kuwa kweli ni wahubiri na mashuhuda wa upendo wake, ili kuwaokoa watu kutoka katika kishawishi cha watu mamboleo cha kuweza kutumbukia katika upofu wa imani. Baba Mtakatifu Francisko amehitimisha hotuba yake kwa Wadominikani wanapoadhimisha Jubilei ya miaka 800 tangu kuanzishwa kwa Shirika lao kwa kumshukuru Mungu kwa neema nyingi ambazo Shirika limeweza kupokea kutoka kwa Mungu na Kanisa na kwamba, anapenda kuwatia shime kufuata kwa furaha kuu karama ya Shirika ya Wadominikani ambayo imeendelea kutekelezwa na familia ya Wadominikani kwa uzito tofauti.

Mfano wa Mtakatifu Dominiko uwawezeshe kuwa na matumaini kwa siku za usoni kwa kutambua kwamba Mwenyezi Mungu daima anapenda kupyaisha yote na kamwe hawezi kumtupa mja wake. Bikira Maria, Mama wa Kanisa na Mama wa Rozari takatifu awaombee na kuwapatia tunza yake ya kimama, ili kweli waweze kuwa ni wahubiri na mashuhuda jasiri wa upendo wa Mungu.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.