2016-08-03 14:22:00

Michezo ya Olympic iwe ni chachu ya amani, maridhiano na upatanisho


Baba Mtakatifu Francisko wakati wa Katekesi yake, Jumatano tarehe 3 Agosti 2016 ametuma salam na matashi mema kwa wananchi wa Brazil, lakini kwa namna ya pekee kabisa raia wa mji wa Rio de Janeiro ambao ni wenyeji wa Mashindano ya  31 ya Olympic Duniani. Ni mji ambao unatoa ukarimu kwa wanamichezo pamoja na mashabiki wao kutoka sehemu mbali mbali za dunia, dunia ambayo kwa sasa ina kiu na shahuku kubwa ya amani, maridhiano na upatanisho.

Ni matumaini ya Baba Mtakatifu Francisko kwamba maadhimisho ya Mashindano ya Olympic kwa mwaka huu huko Rio yatawawezesha wadau mbali mbali kusema kama Mtakatifu Paulo “Nimevipiga vita vilivyo vizuri, mwendo nimeumaliza, imani nimeilinda” sasa wanasubiri kuvitwa taji la ushindi lililo muhimu sana litakalowasaidia kujenga ustaarabu wa mshikamano unaotambua kwamba watu wote wanaunda familia moja ya binadamu licha ya tofauti zao za: kitamaduni, rangi ya ngozi ya mtu, dini au imani yake.

Baba Mtakatifu anawaalika wananchi wa Brazil ambao kwa kawaida ni watu wenye furaha na wamepewa dhamana ya kuandaa michezo ya Olympic wahakikishe kwamba, hii inakuwa ni fursa ya kusherehekea Siku kuu ya Michezo; ili kuvuka nyakati ngumu na kuanza kushirikiana na kutekeleza majukumu kama timu moja, ili kujenga nchi ya Brazil inayojikita katika haki, usalama kwa kuwa na matumaini kwa leo na kesho iliyo bora zaidi. Mwishoni, Baba Mtakatifu anawatakia washiriki wote baraka zake za kitume!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.