2016-08-02 15:13:00

P. Lombardi, SJ. ateuliwa kuwa Rais wa Mfuko wa Joseph Ratzinger


Kardinali Pietro Parolin, Katibu mkuu wa Vatican amemteua Padre Federico Lombardi, aliyekuwa msemaji mkuu wa Vatican kuwa Rais wa Baraza la Mfuko wa Joseph Ratzinger, Benedikto XVI. Itakumbukwa kwamba, huu ni mfuko ulioanzishwa na Baba Mtakatifu Mstaafu Benedikto XVI kunako mwaka 2010, baada ya kusikiliza kilio na hamu kutoka kwa wasomi wengine ya kutaka kusambaza mawazo na nyaraka za wakati huo Professa Joseph Ratzinger pamoja na kuipatia taasisi hii hadhi ya kisheria.

Hadi kufikia mwaka 2015, Monsinyo Giuseppe Scotti ndiye aliyekuwa Rais wa Mfuko wa Joseph Ratzinger- Benedikto XVI kwa kipindi cha miaka mitano. Itakumbukwa kwamba, Monsinyo Scotti alikuwa pia ni Katibu mwambata wa Baraza la Kipapa la Mawasiliano ya Jamii kuanzia mwaka 2010. Lengo ma Mfuko wa Joseph Ratzinger ni kusaidia mchakato wa wasomi kufahamu kwa kina taalimungu, kuandaa na kuratibu makongamano makubwa ya kitamaduni na kisayansi; kutoa tuzo kwa wasomi wanaojipambanua kutokana na mchango wao katika machapisho na tafiti mbali mbali.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.