2016-08-02 10:06:00

Akina mama nyonyesheni watoto wenu kuwakinga na magonjwa na vifo!


Shirika la Kuhudumia Watoto la Umoja wa Mataifa, UNICEF kuanzia tarehe 1 hadi 7 Agosti linaadhimisha Siku ya Kunyonyesha Watoto, ili kuwahamasisha akina mama kuwanyonyesha watoto wao, ili kuwapatia virutubisho muhimu vya afya vinavyiopatikana kutokana na maziwa ya mama, ili kuwakinga watoto dhidi ya magonjwa na vifo! Takwimu zinaonesha kwamba, kati ya watoto millioni 77 wanaozaliwa duniani ni mmoja tu kati ya watoto wawili anayepata bahati ya kunyonya maziwa ya mama.

Takwimu za kimataifa zinaonesha kwamba, ni asilimia 34% ya watoto duniani wanaonyonyeshwa maziwa ya mama, hali inayohatarisha sana maisha ya watoto wachanga. UNICEF inawataka akina mama wanaonyesha kuhakikisha kwamba, wanatekeleza wajibu huu msingi kwa ajili ya ustawi, maendeleo na afya za watoto wao. Watoto wachanga wanapaswa kunyonyeshwa na mama zao baada ya masaa mawili hadi ishirini na manne tangu mtoto anapozaliwa.

Barani Afrika ambako bado kuna kiwango kikubwa cha vifo vya watoto wadogo, tabia ya kuwanyonyesha watoto masaa machache tu baada ya kuzaliwa umeongezeko kwa asilia 10% tangu mwaka 2000 hadi Mwaka huu kwa watoto wanaozaliwa Afrika Mashariki, wakati takwimu zinaonesha kwamba, sehemu nyingine za Bara la Afrika hakuna mabadiliko makubwa.

Takwimu zinaonesha kwamba, Barani Asia kumekuwepo na maboresho makubwa katika kipindi cha miaka 15 iliyopita kwani kutoka katika asilimia 16% hadi kufikia asilimia 45% ni mafanikio ya kuridhisha, ingawa bado kuna haja ya kuendelea kuboresha mwenendo huu ili kuhakikisha kwamba, watoto millioni ishirini na moja wanaozaliwa wananyonyeshwa na mama zao kwa muda muafaka.

UNICEF inasema, ikiwa kama watoto wachanga wangeweza kunyonyeshwa na mama zao wazazi tangu pale wanapozaliwa hadi miezi sita tangu baaada ya kuzaliwa, maisha ya watoto wengi duniani yangeweza kuokolewa. Maziwa ya mama ni chanjo ya kwanza kwa mtoto dhidi ya magonjwa. Wanawake wanaojifungua kwa njia ya upasuaji wana hatari ya kuchelewa kuwanyonyesha watoto wao, ikilinganishwa na wanawake wanaojifungua wenyewe. Wanawake wanapaswa kujizatiti ili kuhakikisha kwamba, wanawaonyesha watoto wao mapema ili kuwapatia kinga dhidi ya magonjwa na vifo!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.