2016-08-01 11:02:00

Vijana wanapaswa kusikiliza, kuamua na kutenda!


Baba Mtakatifu Francisko kabla ya kuondoka nchini Poland kurejea Vatican baada ya kuhitimisha maadhimisho ya Siku ya XXXI ya Vijana Duniani, Jumapili tarehe 31 Julai 2016 alikutana na kusalimiana na vijana waliojitolea katika huduma kwa maelfu ya vijana waliokuwa wanahudhuria Siku ya Vijana Duniani huko Cracovia, Poland kuanzia tarehe 26 – 31 Julai 2016.

Vijana hawa anasema Baba Mtakatifu wamekuwa ni mashuhuda wa huduma, imani, upendo, umoja na mshikamano. Ni vijana waliojisadaka kwa ajili ya vijana wenzao. Si jambo rahisi kuandaa maadhimisho ya Siku ya Vijana Duniani kwani hii ni huduma ya ukarimu inayofumbatwa katika: kazi na majitoleo makubwa yasiyokuwa na malipo! Baba Mtakatifu anawashukuru vijana waliojitolea pamoja na wafadhili mbali mbali waliochangia kwa hali na mali ili kufanikisha maadhimisho haya.

Lakini kwa namna ya pekee, anawashukuru kwa sala iliyomwilishwa katika kazi, bila kuwasahau Wakleri waliokuwa wanaandamana nao ili kuhakikisha kwamba, mambo yote yanakwenda kama yalivyopangwa huku wakiwa na matumaini na hatimaye kufanikisha maadhimisho haya katika kiwango kikubwa. Vijana ni matumaini ya Kanisa na Jamii katika ujumla wake, hivyo wanapaswa kuzingatia mambo makuu mawili: historia ya: watu wao, familia na ile ya mtu binafsi inayoshuhudiwa katika uhalisia wa maisha.

Baba Mtakatifu anasema, hii ni historia ya safari ndefu ya maisha ambayo kijana anaendelea kurithishwa kutoka kwa jamii kwani kijana bila ya historia, huyo hawezi kuwa na matumaini kwa leo na kesho iliyo bora Zaidi. Vijana wawe na ujasiri wa kuendeleza yale mema yaliyofanywa na wazazi wao katika maisha yao. Kumbe, maandalizi ya maadhimisho ya Siku ya Vijana Duniani kwa Mwaka 2019, Baba Mtakatifu anawataka vijana kujenga majadiliano ya kina na “vijana wa zamani” ili kuweza kujichotea hekima na busara za wahenga wao.

Baba Mtakatifu anasema jambo la pili ni kuwa na ujasiri wa kuthubutu kutenda kama kijana mmoja alivyoshuhudia kwa kuwaaga vijana wenzake kwani anakiona kifo mbele yake kutokana na ugonjwa wa Saratani. Lakini kwa miaka mingi amepambana na ugonjwa huu, lakini sasa amefika mwisho wa mapambano na anapenda kujikabidhi mbele ya Mwenyezi Mungu, mwingi wa huruma na mapendo! Hata katika ugonjwa wake, kijana huyu amepandikiza mbegu ya matumaini ya leo na kesho iliyo bora Zaidi.

Baba Mtakatifu anasema hana uhakika kwamba, atakuwepo nchini Panama kwa ajili ya maadhimisho ya Siku ya Vijana kwa Mwaka 2019, lakini ana uhakika kwamba, Khalifa wa Mtakatifu Petro atakuwepo kushiriki pamoja na vijana. Vijana wataulizwa ikiwa kama wamejenga utamaduni wa majadiliano na wazee wao, ili kupata hekima na busara itakayowasaidia kujenga na kudumisha kumbu kumbu hai katika safari ya maisha yao. Mambo makuu matatu ya ambayo vijana wanapaswa kuzingatia ni: kumbu kumbu, Ujasiri na Matumaini ya leo na kesho iliyo bora Zaidi.

Baba Mtakatifu katika hotuba aliyoiandika na baadaye kuikabidhi kwa familia ya Mungu nchini Poland amemshukuru kwa namna ya pekee Bikira Maria aliyewatembelea kwa njia ya Picha ya Bikira Maria wa Kalwaria Zebrzydowska, iliyoheshimiwa sana na Mtakatifu Yohane Paulo II. Bikira Maria ni kielelezo cha usikivu makini na utendaji unaoshuhudia huduma ya upendo kwa jirani. Hapa mambo makuu matatu yanapewa kipaumbele  cha pekee: kusikiliza, kuamua na kutenda.

Bikira Maria baada ya kuambiwa kwamba, angekuwa ni Mama wa Mungu, aliutafakari ujumbe huu kwa makini, akaumwilisha katika ukarimu na uwajibikaji kwa kumsaidia binadamu yake aliyekuwa ni mzee na anahitaji msaada wa dharura. Kuna matukio mbali mbali ambayo Mwenyezi Mungu anapenda kuyaweka mbele ya safari ya maisha ya kila mwamini, jambo la msingi ni kuhakikisha kwamba, matukio yote haya yanaangaliwa na kupimwa kwa mwanga wa Injili. Bikira Maria baada ya kusikiliza na kutafakari anachukua uamuzi wa kukubali mpango wa Mungu katika maisha yake na kwa njia hii anakuwa ni Tabernakuko ya kwanza ya Neno wa Mungu aliyefanyika mwili. Baba Mtakatifu anawataka vijana kufanya maamuzi magumu katika maisha bila kuchelewa, kielelezo cha ujasiri hata kama baadaye wataweza kupambana na matatizo na changamoto za maisha, lakini kwa kutambua kwamba, Mwenyezi Mungu daima yuko pamoja nao!

Bikira Maria baada ya kusikiliza, kutafakari ana amua kufanya maamuzi ya kwenda kumtembelea binadamu yake Elizabeth, kwani ndani mwake anajisikia ile nguvu ya Neno la Mungu ikitenda kazi. Uamuzi wake umesheheni huduma ya upendo inayomsukuma kutoka katika undani wake, ili kuwaendea wengine, tayari kuwashirikisha zawadi ya Mungu ndani mwake, yaani Neno wa Mungu aliyefanyika mwili kwake Yeye Bikira Maria, akawa mwanadamu kwa njia ya Roho Mtakatifu. Bikira Maria akawa ni chemchemi ya furaha inayowashirikisha watoto wawili ambao bado hawajazaliwa.

Baba Mtakatifu anasema huduma ya kujitolea ni muhimu sana katika maisha na utume wa Kanisa, kwani inawawezesha vijana kujiweka wazi mbele ya Kristo Yesu na kuwawezesha kutenda na kuwashirikisha wengine ile furaha inayobubujika kutoka mioyoni mwao. Vijana waliojitolea wakati wa maadhimisho ya Siku ya Vijana Duniani wamekuwa ni Wainjilishaji, kwani Kanisa lipo kwa ajili ya huduma na Uinjilishaji. Bikira Maria baada ya kuhitimisha huduma yake kwa Elizabeth, alirejea nyumbani kwake.

Baba Mtakatifu anasema, si rahisi kuweza kuona kwa haraka matunda ya maadhimisho ya Siku ya Vijana Duniani, lakini vijana wengi wanarejea makwao wakiwa na furaha na upendo na kwamba, Mwenyezi Mungu ndiye peke yake anayetambua sadaka na majitoleo yao. Mwenyezi Mungu mwingi wa huruma na mapendo, atawarudishia maradufu kwa wakati wake kwa wema na ukarimu waliowatendea vijana pamoja na Khalifa wa Mtakatifu Petro wakati wa maadhimisho ya Siku ya Vijana Duniani kwa mwaka 2016. Bikira Maria ni mfano na kielelezo makini cha huduma ya Kikristo, awaombee na kuwakirimia tunza yake ya kimama!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.

 








All the contents on this site are copyrighted ©.