2016-07-30 13:48:00

Onjeni huruma ya Mungu inayogusa sakafu ya maisha yenu!


Baba Mtakatifu Francisko, Jumamosi tarehe 30 Julai 2016 ametembelea Madhabahu ya Huruma ya Mungu, Jimbo kuu la Cracovia na hapo amepata nafasi ya kukutana na Watawa wa Shirika la Bikira Maria Mama wa huruma wapatao 300. Kati yao pia kulikuwepo na watoto 80 wanaohudumiwa na watawa hawa katika hija ya maisha yao ya kila siku. Baba Mtakatifu amebariki Picha kubwa ya Huruma ya Mungu pamoja na kusalimiana na watawa.

Baba Mtakatifu Francisko akiwa madhabahuni hapo amewasalimia waamini pamoja na watu wenye mapenzi mema waliokuwa wamekusanyika nje ya Madhabahu ya Huruma ya Mungu kwa kuwaambia kwamba, hata leo hii, Mwenyezi Mungu bado anawapatia waja wake fursa ya kusikia na kuonja huruma yake inayogusa sakafu ya maisha ya waja wake. Anawaalika waamini kumwambata Kristo Yesu katika hija ya maisha yao, hata pale wanapofikiri na kudhani kwamba,  kutokana na dhambi pamoja na mapungufu yao ya kibinadamu, Mwenyezi Mungu hawezi tena kuwaangalia, lakini hata katika hali kama hii, bado Mwenyezi Mungu anataka kuwaonesha uso wa huruma na mapendo.

Huruma ya Mungu inawatakasa waamini. Baba Mtakatifu anawaalika waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema kuitumia kikamilifu siku hii ili kuweza kujichotea huruma ya Mungu katika maisha! Mwishoni, Baba Mtakatifu alisali pamoja na waamini wao akawapatia baraka zake za kitume na hatimaye akaelekea kwenye Madhabahu ya Mtakatifu Yohane Paulo II kwa ajili ya kuadhimisha Ibada ya Misa Takatifu kwa ajili ya Wakleri na Watawa kutoka Poland!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican








All the contents on this site are copyrighted ©.