2016-07-30 14:00:00

Mbele ya mateso na ukatili wa mwanadamu, kimya kinatawala!


Padre Federico Lombardi, Msemaji mkuu wa Vatican anabainisha kwamba, kambi za mateso na kifo za Aushwitz  na Birkenau ni zilizotembelewa na Baba Mtakatifu Francisko, Ijumaa tarehe 29 Julai 2016 ni mahali ambapo Baba Mtakatifu ametafakari kwa kina na mapana Fumbo la mateso na kifo cha binadamu; ameangalia Injili ya uhai, utu, heshima na wito wa kila mwanadamu aliyeumbwa kwa sura na mfano wa Mungu. Ameona machoni pake ukatili mkubwa wa binadamu unaoendelea kushuhudiwa sehemu mbali mbali za dunia.

Limekuwa ni tukio ambalo katika ukimya wake, limetoa mwangwi mkubwa wa fumbo la mateso na mahangaiko ya mwanadamu hata katika nyakati hizi. Hapa ni mahali ambapo hakuna haja ya kuzungumza maneno mengi, bali kufanya toba na kuomba msamaha ili huruma ya Mungu iguse na kuponya madonda haya katika historia ya mwanadamu.

Baba Mtakatifu ameendelea kutafakari Njia ya Msalaba, mateso na mahangaiko ya mwanadamu kwa kutembelea Hospitali ya Watoto ya Protokocim, akashuhudia mateso na mahangaiko ya watoto wagonjwa; mateso ambayo hayana hata majibu ya mkato, bali Kristo Yesu anayafafanua kwa njia ya Fumbo la Msalaba. Njia ya Msalaba ni mahali ambapo Wakristo wanapata majibu ya maswali magumu na changamoto za maisha! Hakuna hakuna maneno mengi, bali Kristo alijiaminisha kwa Baba yake wa mbinguni, kwa kuyamimina maisha yake ili iweze kuwa ni fidia ya wengi.

Padre Lombardi anasema, Fumbo la Ufufuko wa Kristo ni mwaliko kwa waamini na watu wote wenye mapenzi mema, kulishuhudia kwa njia ya imani tendaji inayomwilishwa katika matendo ya huruma: kiroho na kimwili katika uhalisia wa maisha ya watu. Ijumaa imekuwa ni siku muhimu sana katika maadhimisho ya Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu kwa vijana wa kizazi kipya wanapoadhimisha Siku ya XXXI ya Vijana Duniani.

Baba Mtakatifu anawakumbusha vijana kwamba, ulimwenguni kuna wema na ubaya, kumbe, wanapaswa kusimama kidete kuwa ni mashuhuda wa Injili ya matumaini, amani, upendo na mshikamano dhidi ya vita, chuki na uhasama unaoendelea kuvuruga mafungamano ya maisha ya kijamii sehemu mbali mbali za dunia. Fumbo la Msalaba ni mahali ambapo vijana wanaweza kuona mwanga angavu unaowajalia ujasiri wa kujisadaka bila ya kujibakiza katika huduma makini kwa maskini na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii.

Vijana anasema Padre Lombardi, wanapaswa kutambua kwamba, kuna mapambano endelevu duniani kati ya wema na ubaya, kumbe wanapaswa kuwa macho na makini zaidi, ili kamwe wasimezwe na malimwengu. Uzoefu na mang’amuzi ya mateso na kifo kwenye kambi za mateso zinawaacha watu wengi wakiwa wameshikwa bumbuwazi, kama hata ambavyo Baba Mtakatifu Francisko ameamua kubaki katika hali ya ukimya.

Hapa ni kielelezo cha utamaduni wa kifo unaoendelea kufumbatwa katika biashara haramu ya silaha kwa ajili ya faida ya watu wachache wasioguswa na mateso na mahangaiko ya watu wengine, kwao ni fedha tu na hata kama inanuka damu ya watu wasiokuwa na hatia. Baba Mtakatifu anataka watu kuangalia hali ya magereza yalivyofurika kiasi hata cha kudhalilisha utu na heshima ya binadamu; mateso, nyanyaso na dhuluma wanazofanyiwa wafungwa ni mambo ambayo kamwe hayapaswi kufumbiwa macho! Hii ndiyo tafsiri sahihi ya ukimya wa Baba Mtakatifu katika kambi za mateso na kifo. Watu anasema Padre Lombardi, wanapaswa kusimama kidete kulinda, kutetea na kudumisha utu na heshima ya binadamu. Njia ya Msalaba bado inaendelea katika historia ya maisha ya mwanadamu hata nyakati hizi! Hapa hakuna kulala, hadi kieleweke!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.