2016-07-30 10:20:00

Majibu yanapatikana kwenye Fumbo la Msalaba!


Umati mkubwa wa vijana kutoka sehemu mbali mbali za dunia, Ijumaa jioni tarehe 29 Julai 2016 umeadhimisha Ibada ya Njia ya Msalaba iliyongozwa na kauli mbiu “Njia ya Msalaba, Njia ya Huruma ya Mungu”. Kwa muda wa masaa matatu kabla ya kuwasili Baba Mtakatifu Francuisko vijana wameweza kushiriki tukio hili kwa kusikiliza na kuona shuhuda mbali mbali za watu wanaomwilisha matendo ya huruma: kiroho na kimwili katika uhalisia wa maisha ya watu. Wakati wa Njia ya Msalaba, vijana mbali mbali walishiriki katika kuubeba Msalaba, alama ya upendo na huruma ya Mungu kwa waja wake!

Baba Mtakatifu Francisko wakati wa tafakari yake, amechambua kwa kina na mapana Matendo ya huruma kiroho na kimwili: Yaani: Kulisha wenye njaa; kunywesha wenye kiu; kuvika walio uchi; kukaribisha wageni; kutembelea wagonjwa, kutembelea wafungwa na kuzika wafu! Matendo ya huruma kiroho ni: kushauri wenye shaka, kufundisha wajinga, kuonya wakosefu, kufariji wenye huzuni, kusamahe makosa, kuvumilia wasumbufu, kuombea wazima na wafu!

Baba Mtakatifu anasema, maneno ya Yesu kuhusu matendo ya huruma yanakabiliwa na maswali magumu yasiokuwa na majibu ya mkato kuhusu uwepo wa Mungu, wakati dunia inaendelea kusheheni maovu kila kukicha! Watu wanakufa kwa njaa, kiu, ukosefu wa makazi bora na salama; kuna wimbi kubwa la wakimbizi na wahamiaji! Mwenyezi Mungu yuko wapi wakati watu wasiokuwa na hatia wanauwawa kinyama kutokana na vita na vitendo vya kigaidi.

Lakini Mwenyezi Mungu yuko wapi wakati kuna watoto wananyanyasika, wanadhulumiwa na kuteseka kwa magonjwa yasiyokuwa na tiba. Haya ni maswali ambayo hayana majibu ya kibinadamu, lakini Yesu anajibu kwa kusema kwamba, hata katika matukio yote haya, Mwenyezi Mungu yupo! Kristo anateseka na kunyanyasika kati yao, kwani anajitambulisha kati yao! Wote hawa wameungana na Kristo Yesu, kiasi cha  kuunda mwili mmoja!

Yesu amechagua kujifananisha na wale wote wanaoteseka kiroho na kimwili, kwa kukubali kufanya Njia ya Msalaba kuelekea Kalvari. Kwa kifo chake Msalabani, akajiaminisha mikononi mwa Mwenyezi Mungu na kujivika mwilini wake yote haya kama kielelezo cha upendo unaojisadaka kwa ajili ya kuponya madonda ya kimwili, kimaadili na kiroho kwa binadamu wote. Kristo Yesu, kwa kukumbatia Mti wa Msalaba, ameukumbatia pia utupu wa binadamu, baa la njaa, kiu na upweke hasi; machungu na kifo cha watu wa nyakati zote.

Baba Mtakatifu anasema, Njia ya Msalaba huko kwenye Uwanda wa Blonia (Buonye) inawakumbatia kwa namna ya pekee wakimbizi na wahamiaji kutoka Syria ambao wamelazimika kuikimbia nchi yao kutokana na vita. Kwa njia ya Msalaba, vijana wameweza kujifananisha na Yesu katika matendo ya huruma kiroho na kimwili, yaliyochora na kuandika vituo vya Njia ya Msalaba wakati wa maadhimisho ya Siku ya XXXI ya Vijana Duniani. Matendo haya yanawawezesha vijana kujifunua kwa huruma ya Mungu sanjari na kuomba neema ya kutambua umuhimu wa huruma ya Mungu inayowawezesha kutenda mengi katika maisha. Waamini wanahamasishwa kumwilisha matendo ya huruma kama njia ya kumhudumia Kristo Yesu anajitambulisha kwa kila mtu katika mahitaji yake msingi. Ni katika matendo ya huruma kwamba, waamini wanaweza kukutana na Mwenyezi Mungu na kwamba, hii ndiyo Protokali ambayo itatumiwa na Kristo Yesu atakapokuja kuwahukumu wazima na wafu.

Baba Mtakatifu anaendelea kufafanua kwamba, matendo ya huruma kiroho, yanawawezesha waamini kuwaonjesha jirani zao ukarimu kwa wale wanaoteseka kimwili na kiroho kutokana na dhambi, kielelezo makini cha ushuhuda wa Wakristo. Walimwengu wanawahitaji watu kama vijana hawa wanaojisadaka kwa ajili ya huduma makini kwa maskini na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii, kama kielelezo cha ushuhuda wa ufuasi wao kwa Kristo Yesu, aliyejisadaka kwa ajili ya huduma hadi tone la mwisho la maisha yake. Wakristo watambue kwamba, wanaishi kwa ajili ya kuhudumia, vinginevyo wanamsaliti Kristo mwenyewe!

Baba Mtakatifu anawataka vijana kuonesha jeuri katika kutoa huduma kwa ajili ya walimwengu wanaoteseka: kiroho na kimwili, ili kweli waweze kuwa ni alama ya upendo wa huruma ya Mungu kwa binadamu kwa kuambata Njia ya Msalaba inayobubujika furaha na amani ya kweli kwani hapa mwamini anaonja utimilifu wa maisha yake yanayofumbatwa katika Fumbo la Msalaba, njia na mtindo wa maisha ya Mungu yanayooneshwa kwa namna ya pekee na Kristo Yesu hata katika ulimwengu mamboleo unaosheheni mipasuko, kinzani, rushwa na ukosefu wa haki.

Njia ya Msalaba anasema Baba Mtakatifu ni kielelezo cha ushindi dhidi ya dhambi, ubaya na mauti, kwani Msalaba unadhihirisha mwanga angavu wa Kristo Mfufuka, mwanzo mpya na utimilifu wa maisha. Ni njia ya matumaini kwa sasa na kwa siku za usoni. Kwa mwamini anayetembea katika Njia ya Msalaba kwa imani, anaweza kujisadaka kwa ajili ya binadamu na kupandikiza matumaini, changamoto kwa vijana wa kizazi kipya!

Baba Mtakatifu anahitimisha tafakari yake kwa kusema, siku ile ya Ijumaa kuu, wafuasi wengi wa Yesu walirejea majumbani mwao wakiwa wamesongwa na huzuni kubwa mioyoni mwao; wengine hawakutaka hata kuikumbuka kashfa hii ya Msalaba. Baba Mtakatifu anawauliza vijana baada ya maadhimisho haya wanapenda kurejea wakiwa katika hali ya namna ya gani, lakini watambue kwamba, ulimwengu unawakodolea macho! Kila kijana anapaswa kujibu changamoto hii kutoka katika undani wa moyo wake!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.