2016-07-30 10:35:00

Bado kuna watu duniani waliobaki Ijumaa kuu!


Baba Mtakatifu Francisko mara baada ya chakula cha usiku, Ijumaa tarehe 29 Julai 2016 alijitokeza mbele ya Makao makuu ya Jimbo kuu la Cracovia na kusalimiana na umati wa vijana uliokuwepo mahali hapo! Amesema, Ijumaa, ilikuwa ni Siku ya Njia ya Msalaba kwa kutafakari Fumbo la Pasaka, yaani mateso, kifo na ufufuko wa Kristo. Ni mateso ya Kristo ambayo hadi leo hii yanaendelea kujionesha kati ya watu, hata kama niĀ  zaidi ya miaka elfu mbili iliyopita.

Baba Mtakatifu anakaza kusema kuna wagonjwa na waathirika wa vita; maskini na watu wasiokuwa na makazi; kuna watu wanaokufa kwa baa la njaa na utupu; kuna watu wenye mashaka na wasi wasi ya maisha; kuna wale ambao hawana furaha na faraja ya maisha, watu wanaoelemewa na mzigo wa dhambi zao!

Baba Mtakatifu anakaza kusema, Jioni, alipata nafasi ya kutembelea Hospitali ya Watoto ya Prokocim na kujionea mateso na mahangaiko ya watoto. Bado anaendelea kujiuliza sababu ya mateso na mahangaiko ya watoto hawa! Hata Yesu mwenyewe bado anaendelea kuteseka kati ya watoto hawa na kwamba, mateso ni fumbo kubwa katika maisha ya mwanadamu. Hakuna majibu ya mkato katika maswali kama haya!

Baba Mtakatifu anasema, ametembelea kwenye Kambi za mateso na kifo huko Auschwitz na Birkenau ambako amewakumbuka maelfu ya watu, walioteswa na kuuwawa kikatili takribani miaka 70 iliyopita. Hawa ni watu walioumbwa kwa sura na mfano wa Mungu. Lakini hata leo hii, bado kuna ukatili, nyanyaso na dhuluma zinazoendelea duniani. Kuna wafungwa wanateswa; magereza yamejaa na kufurika wafungwa na huko wanaishi kama wanyama; utu na heshima yao kama binadamu vimewekwa rehani. Kuna watu bado wananyongwa, wanapigwa risasi hadharani au kuuwawa kwa sumu na gesi.

Baba Mtakatifu anawaalika waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema kusali kwa ajili ya kuombea watu wanaoteseka: kiroho na kimwili sehemu mbali mbali za dunia. Katika mateso na mahangaiko yote haya, Yesu Kristo amejitwisha mzigo wa dhambi na mapungufu ya binadamu. Kila mtu anaelemewa na mzigo wa dhambi, lakini bado Yesu anawapenda na kuwasamehe dhambi zao wanapokimbilia huruma na upendo wake.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.