2016-07-29 14:01:00

Vijana Cuba, iweni ni majembe ya huruma ya Mungu!


Vijana zaidi ya 1,400 kutoka Cuba, kuanzia tarehe 28- 31 Julai 2016 wanashiriki Siku ya Vijana Duniani nchini Cuba sanjari na maadhimisho ya Siku ya Vijana Duniani yanayoendelea nchini Poland. Hili ni tukio ambalo linawaunganisha vijana kutoka Cuba ambao hawakupata nafasi ya kwenda nchini Poland kutokana na sababu mbali mbali, lakini wanataka kuungana na kushikamana na Baba Mtakatifu Francisko katika maadhimisho haya.

Huu ni muda wa Katakesi, Sala, Tafakari na Maadhimisho ya Sakramenti za Kanisa. Vijana kutoka Cuba katika barua waliyomwandikia Baba Mtakatifu wanasema, kamwe hawawezi kukata tamaa kuadhimisha Siku kuu ya zawadi ya imani kutokana na matatizo ya kiuchumi na ukata wa fedha. Hata wakiwa nchini Cuba, bado wanaweza kuonesha kuwa kweli wao ni majembe ya huruma ya Mungu kwa wananchi wa Cuba.

Baba Mtakatifu Francisko katika ujumbe wake kwa vijana hawa huko Cuba, anawataka wajenge utamaduni wa kukutana na watu; kuheshimiana na kuthaminiana pamoja na kuwa na ndoto ya maisha bora zaidi. Wajenge tabia ya kusikiliza, kutafakari na kulimwilisha Neno la Mungu katika maisha yao, kwani Injili inasaidia kufunda moyo wa mwanadamu, kwani Neno la Mungu ni roho na uzima na linapaswa kumwilishwa katika uhalisia wa maisha.

Njia ya Msalaba, iwakumbushe upendo kwa Mungu na jirani kwani Msalaba ni kielelezo cha hali ya juu kabisa cha upendo, huruma na msamaha wa Mungu kwa binadamu. Ni kielelezo cha ushindi dhidi ya dhambi na mauti na chemchemi ya uzima wa milele. Vijana wanapopitia Lango la huruma ya Mungu, wawe wepesi kuguswa na upendo wenye huruma kutoka kwa Mwenyezi Mungu, tayari kuwashirikisha wengine, wema, upendo, huruma na msamaha unaobubujika kutoka kwa Kristo na Kanisa lake.

Vijana wanapofanya Ibada ya Kuabudu Sakramenti Kuu, waombe nguvu na ujasiri wa kuwa na upendo unaoweza kusamehe na kusahau ubaya; upendo unaowajenga na kuwawezesha kuwa ni vyombo na mashuhuda wa huruma ya Mungu bila woga wala makunyanzi. Vijana wawe na ujasiri wa kumwilisha matendo ya huruma: kiroho na kimwili, kwa maskini na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii, ili kuwaonjesha maisha mapya.

Vijana kutoka Cuba, wawe ni cheche za matumaini na ujasiri kama walivyoachiwa n ana Mtumishi wa Mungu Padre Felix Varela, kwa kuthubutu kuwa na ndoto ya maisha ya bora zaidi! Bila ndoto, vijana wanajifungia katika ubinafsi wao. Baba Mtakatifu anawaambia vijana kwa anayo matumaini makubwa kutoka kwao, kumbe wasikate wala kukatishwa tamaa ya maisha, bali wawe na imani na matumaini kwa Kristo Yesu. Matumaini yawe ni chachu ya ujenzi wa urafiki wa kijamii ili kudumisha uzalendo, amani na utulivu.

Vijana wawe ni wajenzi wa madaraja ya watu kukutana na kusaidiana kwa mawazo, maneno na matendo mema. Wajenge historia kwa kushirikiana na kushikamana na wote; kwa kutembea na kusaidiana. Bikira Maria mama wa upendo, awasaidie na kuwaimarisha vijana wa Cuba, ambaye kwa takribani miaka 400 amewasindikiza waamini katika imani na matumaini, daima wakiwa tayari kutekeleza yale atakayowaamuru. Baba Mtakatifu Francisko anapenda kuwahakikishia uwepo wake wa karibu kiroho wakati wa maadhimisho haya ya Siku ya Vijana nchini Cuba.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.