2016-07-29 14:31:00

Tafakari ya Fumbo la Mateso ya Mwanadamu!


Padre Federico Lombardi, Msemaji mkuu wa Vatican anabainisha kwamba, Alhamisi, tarehe 28 Julai 2016 imekuwa ni siku muhimu sana katika maadhimisho ya Siku ya Vijana Duniani kwani Baba Mtakatifu Francisko ameonesha ufundi wa kuzungumza na kujadiliana na vijana katika sherehe za kuwakaribisha rasmi vijana kutoka sehemu mbali mbali za dunia nchini Poland. Vijana wamepeperusha bendera 178 kielelezo cha majadiliano yanayopania kukuza na kudumisha misingi ya haki, amani na maridhiano kati ya watu!

Huu ni ujumbe mkubwa ambao vijana wanataka kushuhudia kwa walimwengu kwamba, inawezekana kukaa na kuishi kwa pamoja kwa kufumbata tunu msingi za maisha ya kiutu, kiroho na kimaadili, tayari kusimama kidete kutangaza na kushuhudia Injili ya huruma ya Mungu na furaha; chachu ya mabadiliko katika ulimwengu mamboleo. Huduma makini ya upendo na mshikamano; imani na matumaini ni ujumbe makini kwa walimwengu kwa nyakati hizi.

Maadhimisho ya Jubilei ya miaka 1050 ya Ukristo nchini Poland ni tukio ambalo limekuwa na uzito wa pekee katika kukuza, kudumisha na kushuhudia imani inayobubujika kutoka katika kisima cha Ubatizo. Tafakari ya Baba Mtakatifu kwenye Kambi za mateso na mauaji ni changamoto ya kuangalia historia iliyopita tayari kusimama kidete kulinda na kudumisha: maisha, utu na heshima ya binadamu. Njia ya Msalaba ni changamoto ya kumwilisha matendo ya huruma: kiroho na kimwili katika maisha ya watu wanaoendelea kufuata Njia ya Msalaba kutokana na sababu mbali mbali.

Maadhimisho ya Fumbo la Ekaristi Takatifu kama kilele cha maadhimisho ya Siku ya Vijana Duniani kwa Mwaka huu, itakuwa ni fursa ya kuanza kujizatiti katika maisha na utume wa Kanisa katika mapambazuko ya Millenia ya tatu ya Ukristo. Hapa mkazo ni Uinjilishaji mpya unaojikita katika ushuhuda wa maisha! Siku ya Alhamisi, tarehe 28 Julai 2016, Baba Mtakatifu alipata nafasi ya kutembelea Madhabahu ya Bikira Maria, Malkia wa Poland, mahali ambapo familia ya Mungu nchini Poland imeweza kuboresha, imani, matumaini na mapendo yake kwa Kristo na Kanisa lake.

Baba Mtakatifu Francisko, Alhamisi jioni aliwasili kwenye mapokezi ya vijana akiwa amepanda treni ya umeme, huku akiwa ameambatana na walemavu pamoja na wagonjwa. Baba Mtakatifu anapenda kuwahamasisha waamini kumwilisha matendo ya huruma: kiroho na kimwili katika uhalisia wa maisha kama alivyofanya kwa kumtembelea Kardinali Francisko Macharski. Hii ni sehemu ya utaratibu wa kawaida wa Baba Mtakatifu kuwatembelea  Makardinali wanapokuwa wamelazwa au kwenye nyumba za mwazee ili kuonesha huruma na upendo wa kibaba! Hii ni njia muafaka ya kuweza kuishi kikamilifu maadhimisho ya Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu.

Tarehe 29 Julai 2016 ni Siku ya Njia ya Msalaba, Kanisa linapotafakari kwa kina na mapana mateso na kifo cha Kristo Yesu yanayoendelea kushuhudiwa kwa watu mbali mbali hata katika ulimwengu mamboleo. Ni siku ambayo Baba Mtakatifu ametembelea Kambi za mateso na mauaji ya Auschwitz- Birkenau pamoja na kutembelea Hospitali ya Watoto wadogo. Umekuwa wakati wa ukimya na machozi ya masikitiko kutokana na ukatili dhidi ya utu na heshima ya binadamu.

Ijumaa imekuwa ni Siku ya Kutafakari Fumbo la Mateso na mahangaiko ya mwandamu yanayofumbatwa katika umaskini, magonjwa na ujinga: Ni mateso yanayojionesha katika vita, vitendo vya kigaidi, nyanyaso na dhuluma za aina mbali mbali. Kumbe, Njia ya Msalaba inayojikita katika Matendo ya Huruma kiroho na kimwili ni jibu makini ya mateso na mahangaiko ya binadamu.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.