2016-07-29 13:46:00

Maisha ya ndoa yataka moyo kweli kweli!


Baba Mtakatifu Francisko, Alhamisi tarehe 28 Julai 2016 baada ya chakula cha usiku alijitokeza mbele ya Makao makuu ya Jimbo kuu la Cravovia na kuwasalimia wanandoa wapya. Baba Mtakatifu amewapongeza kwa kuonesha kushuhudia ujasiri katika maisha kwani si rahisi kuweza kuunda familia na kuipatia mahitaji yake msingi pamoja na kuchukua maamuzi magumu ya kufunga ndoa kwa maisha yote.

Katika kukuza, kudumisha na kushuhudia Injili ya familia, Baba Mtakatifu Francisko anawataka wanandoa kujikita katika maneno makuu matatu: Naomba, Asante na Samahani. Ni maneno ambayo yanaweza kuimarisha sana udumifu wa maisha ya ndoa na familia. Wanandoa wawe na ujasiri wa kuomba na kushauriana katika maisha bila kumtelekeza mwenzi wa ndoa. Wanandoa wajenge na kudumisha utamaduni wa kushukuru, kwani kwa njia ya Sakramenti ya Ndoa, watu hawa wawili, yaani mume na mke wanaungana na kuwa kitu kimoja.

Katika safari ya maisha, kukosa na kukoseana ni jambo la kawaida, kusamehe na kusahau ni kuanza hija ya utakatifu wa maisha; wanandoa wajenge utamaduni wa kusameheana kwa unyenyekevu, jambo muhimu sana katika maisha ya ndoa na familia. Maneno haya pia yawasaidie wanandoa watarajiwa katika maisha na utume wao. Kukosa na kukosehana; kurusha na kurushiana sahani; kupimana kwa sauti ni mambo ya kawaida!

Haya ni mambo ya kawaida, lakini jambo la msingi ni kuhakikisha kwamba, wanaimaliza siku kwa kuombana msamaha, ili kuanza upya. Kamwe wasiwe na vita baridi kwani ni hatari sana kwa maisha ya ndoa. Hapa hakuna haja ya kutafuta waalimu, bali ishara ya upendo, inatosha kuona mwenzi wa maisha akitoa tabasamu la kukata na shoka!. Baba Mtakatifu pamoja na wanandoa wapya na watarajiwa walisali pia kwa ajili ya kuziombea familia mbali mbali, ili ziweze kusimama kidete kulinda, kushuhudia na kutangaza Injili ya familia!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idha ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.