2016-07-28 11:49:00

Vijana ponyeni majeraha ya kiroho na kimwili; acheni ukatili!


Maadhimisho ya Siku ya XXXI ya Vijana Duniani ni muda wa sala, tafakari na sherehe miongoni mwa vijana wa kizazi kipya! Baba Mtakatifu Francisko, akiwa nchini Poland, Jumatano jioni, tarehe 27 Julai 2016 amezungumza na vijana kutoka Italia wanaohudhuria Siku ya Vijana Duniani huko Poland na kujibu maswali matatu kwa njia ya televisheni. Baba Mtakatifu anasema, ajali inapotokea watu wanapata madonda ya mwili na roho yanayowasababisha hofu na wasi wasi, changamoto na mwaliko wa kuvuka hofu hii kwa kuambata hekima na mambo mazuri yanayopatikana katika maisha kwa: furaha, imani na matumaini.

Vijana wasikubali hata kidogo kujikatia tamaa ya maisha na matokeo yake ni kutumbukia katika matumizi haramu ya dawa za kulevya na utumwa mamboleo. Vijana wawe na ujasiri wa kupambana na changamoto za maisha kwa ari na moyo mkuu huku wakishuhudia furaha katika maisha.

Baba Mtakatifu amezungumzia kuhusu ukatili wanaokumbana nao watoto wadogo na hata watu wazima katika hija ya maisha yao: kiroho na kimwili; utu, heshima na utaifa wao. Ukatili ni mzizi wa vita, chuki, uhasama na mipasuko ya kijamii. Ukatili unaharibu sifa njema za watu wengine. Umbeya ni ugaidi wa maneno ambao vijana wanapaswa kupambana nao bila kuchoka kwa kujikita katika: ukimya, uvumilivu, haki, amani na msamaha. Lakini anawakumbusha vijana kwamba, kusamehe na kusahau si jambo rahisi sana, lakini kwa neena ya Mungu inawezekana. Vijana wajenge utamaduni wa upendo, ukarimu na mshikamano kwa wageni. Unyenyekevu ni fadhila muhimu sana katika ulimwengu mamboleo, ili kuambata msamaha wa kweli.

Baba Mtakatifu anasema, mashambulizi ya kigaidi yanayoendelea kujitokeza sehemu mbali mbali za dunia ni kielelezo cha ukosefu wa amani na badala take chuki na uhasama vinatawala. Kuna kundi la vijana 350 kutoka Verona, Kaskazini mwa Italia, lilibidi kusitisha safari yake baada ya kusikia mashambulizi ya kigaidi hivi karibuni na matokeo yake, kutoka Verona wamefika vijana watatu na Padre mmoja tu kati ya vijana 350 waliokuwa safarini kuelekea Jimbo kuu la Cracovia, Poland!

Baba Mtakatifu anawataka vijana kujenga madaraja ya utu na heshima ya binadamu na kubomoa mambo yote yale yanayotaka kuwatenganisha na kuwagawa watu! Chuki na uhasama ni kuta za utengano. Vijana wasikatishwe tamaa na vizingiti vya maisha, bali waoneshe ujasiri wa kupambana kiume, hadi kieleweke katika kukuza na kudumisha Injili ya uhai.

Na Padre Richard A. Mjigwa. C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican. 








All the contents on this site are copyrighted ©.