2016-07-27 13:12:00

Uchu wa mali na utajiri wa haraka haraka unavyowatesa watu!


Wanataalimungu, wanasayansi jamii na wanafalsafa wengi ulimwenguni wanamuelezea mwanadamu kuwa ni mwanajumuiya. Hii inamaanisha kwamba ukweli juu ya mwandamu na udhati wa hadhi yake unaonekana katika mahusiano na wengine. Mwanadamu hawezi kuishi peke yake kama kisiwa au gendaeka. Daima anayo nguvu inayomsukuma kutoka ndani kutafuta mahusiano na mwingine. Hii yote inapata maana yake kutokana na fumbo la uumbaji ambamo tunajiona kuwa sote tunayo asili moja na hivyo kusukumwa kuishi kindugu. Ndiyo maana dhana ya undugu huwa inajitokeza katika maeneo mengi ya kusisitiziwa kama nyenzo muhimu ya kujikamilisha mtu binafsi na jamii yote inayomzunguka katika ujumla wake.

Ulimwengu mambo leo unamvuta mwanadamu kutoka katika tunu hii njema ya undugu. Binadamu anajijengea ukuta na kutaka kuishi peke yake na kutafuta faida yake mwenyewe. Moja ya mambo yanayomfanya mwanadamu kuingia katika kadhia hiyo ni mali. Masomo yote ya Dominika hii ya 18 ya mwaka yanatuelekeza katika kuitafakari hatari hiyo inayotunyemelea na hivyo kutupendekezea njia itakayotuokoa na hivyo kuendelea kustawi katika udugu wetu. Mfano tunaousikia katika Injili unatupeleka moja kwa moja katika mwelekeo wa mwanadamu wa leo ambaye yupo tayari kujilimbikizia mali hata kama inatapoteza uhusiano na ndugu yake: “mwambie ndugu yangu anigawie urithi wetu”. Ombi hili kwa Kristo linaashiria juhudi za kutafuta utengano kwa sababu ya mali.

Kristo anatutahadharisha kwa kututaka kujilinda na choyo akisema: “uzima wa mtu haupo katika wingi wa vitu vyake alivyo navyo”. Uzima wa mtu au usalama wake si katika mali bali ni katika mahusiano mema ya kindugu. Uchoyo hututenga na wenzetu na haya ni matunda ya ubinafsi. Tangu mwanzoni Mungu alimuumba mwanadamu katika mahusiano ya kindugu, aliwaumba mwanamme na mwanamke akiwaambia zaeni mkaongezeke, mkaijaze dunia na kuitiisha. Hivyo, ufanisi wetu tangu awali haukuwekwa katika mazingira ya kibinafsi bali ni katika mazingira ya umoja. Mafanikio ya mmoja ndani ya familia ya mwanadamu yanapata maana si katika wingi wa akili zake au mali zake au cheo chake bali ni katika mahusiano mema ya kushirikishana na wanafamilia wenzake. Kwa kifupi anachosisitiza Kristo ni kwamba uzima wetu upo katika umoja wetu kwa kushikamana na kushirikishana.

Mfano wa tajiri mpumbavu ambao Kristo anautoa unatuonesha kwa kina na mapana katika maana ya mwanadamu kutafuta mali na kuendelea kujilimbikizia hata kama itaharibu undugu na wenzangu. Huu ndiyo uhalisia tunao uona katika mazingira ya kijamii na kiuchumi. Wenye mamlaka na matajiri wengi wanaendelea kujichumia mali nyingi ambazo hata wakati mwingine huzidi mahitaji yao ya lazima. Kwa kuwa wanafanya hivyo kusudi waendelee “kupumzika kula na kufurahi” kamwe hawawezi kuwa tayari kumpokea ndugu yao ambaye yupo pembeni anateseka. Hii ni kwa sababu hana uhakika na kesho kama ataendelea kuwa na vitu hivyo na hivyo kama akitoa basi anaweza kuingia katika mahangaiko. Lakini zaidi ni kwa sababu haoni muunganiko na ndugu yake huyu aliye pembeni yake akimlilia. Mali zimemfumba macho.

Mhubiri katika somo la kwanza anatukumbusha uhalisia na maana ya mali za ulimwengu huu. Maandiko yake yanatuonesha kwa wazi kabisa ufupi wa mali zetu. Haya ni mambo yanayopita tu, haya ni mambo ambayo yanaupamba ubinadamu wetu lakini hayafanywi kuwa sehemu ya ubinadamu wetu. Mtu anaweza kufanya kazi nzuri na kwa ustadi mkubwa au mwingine anaweza kuwa na kipaji cha akili cha kuvumbua mengi mazuri kwa ajili ya maisha ya mwanadamu lakini mwishoni atakufa au kuyapoteza kwa sababu moja au nyingine. Mwishoni Mhubiri anatuambia kwamba hayo yote ni ubatili mtupu. Hii haimaanishi kwamba shughuli za binadamu hazina maana au mali na tunavyomiliki si vitu muhimu bali tunakumbushwa ukomo wa vitu hivyo na maana ya vitu hivyo uonekana katika kuhudumia ubinadamu. Hivyo hekima yetu isijikite katika mambo hayo tu bali itusaidie kuyatumia mambo hayo ili kupata kile kilicho chema, yaani utu wema unaofunuliwa kwetu kwa njia ya Kristo.

Mtume Paulo anatueleza vizuri haiba tunayoipokea baada ya ubatizo wetu. Haiba hiyo inapaswa kuonekana katika maisha yetu. Kwa ubatizo tunaipokea hali ya kuwa wana wa Mungu ni hivyo tunahimizwa kutafuta mambo ya juu na si ya ulimwengu huu. Mtume Paulo anaendelea kutubainishia mambo ya ulimwengu huu kuwa ni uasherati, uchafu, tamaa mbaya, mawazo mabaya na kutamani. Utu mpya tunaoupokea unatufanya kuwa ndugu na hivyo unatuuunganisha sote bila ubaguzi. Kwa maneno mengine ukristo unatudai kuishi kindugu na kushirikishana utajiri wa huruma ya Mungu unaomiminwa ndani mwetu kila mmoja kwa nafasi yake, kiwango chake na uwezo wake.

Jumuiya ya kindugu inayopaswa kujengwa katika Kristo ni mithili ya Jumuiya za mwanzo za Kanisa ambamo “hapana mmoja aliyesema ya kuwa kitu chochote alicho nacho ni mali yake mwenyewe; bali walikuwa na vitu vyote shirika ... wala hapakuwa na mtu miongoni mwao mwenye mahitaji; kwa sababu watu wote waliokuwa na viwanja au nyumba waliviuza, wakaileta thamani ya vitu vile vilivyouzwa, wakaiweka miguuni pa mitume; kila mtu akagawiwa kwa kadiri ya alivyohitaji” (Mdo 4: 32, 34 – 35).

Hii ni changamoto inayowekwa mbele yetu sisi kama wakristo. Mara nyingi tumekuwa tunatawaliwa na uchoyo na hivyo kushindwa kufungua hazina za huruma ya Mungu tulizokirimiwa. Wahitaji wanapotuelekea tunajikuta katika hali ya kuwatazama kana kamba si binadamu wenzetu na pengine kuanza kuhoji kwa nini watujie sisi badala ya kutulia na kuhangaika katika mazingira yao. Tunafumba macho na kushindwa kuona ukame unaoweza kuwasababishia njaa wao lakini kwetu tulipokea baraka ya mvua na kupata mazao mengi. Tunashindwa kuona vita na machafuko mengi ya kisiasa ambayo yanawafukuza kwao kulinganisha na hali ya utulivu tunayokuwa nayo. Tunapowasukumia huko katika hali zao ni sawa na kuwaambia hatutaki mshiriki katika hali yetu tunayomiliki. Tunapolalamika wanapotujia ni sawa na kijana wa mfano katika Injili anakataa kuwa na ushirika na ndugu yake bali tunamtaka Yesu agawanye urithi wetu, kila mmoja ajijue mwenyewe.

Tunakumbushwa leo hii kuutambua utajiri ambao tumekirimiwa na mwenyezi Mungu. Vyote hivyo ni hazina alizoziweka ndani ya kila mmoja wetu kwa ajili ya kuishi kindugu. Mungu amekukirimia uwezo wa kiakili, busara na hekima mithili ya mfalme Solomoni, uwezo wa kuongoza kama Mfalme Daudi, karama ya upatanishi kati ya ndugu na hata mali nyingene za kidunia zinazoshikika mfano wa nyumba, magari, nguo na vyakula. Utajiri huo ni kwa ajili ya kuufanya ubinadamu wote upumzike, ule, unywe na ufurahi. Hili linafanikishwa kwa mahusiano yetu ya kindugu na kushirikisha. Tukumbuke kwamba umoja ni nguvu bali utengano ni udhaifu.

Kutoka studio za Radio Vatican mimi ni Padre Joseph Peter Mosha.








All the contents on this site are copyrighted ©.