2016-07-26 07:21:00

Sudan ya Kusini: Majadiliano ya amani katika ukweli, uwazi na haki!


Machafuko ya kisiasa yaliyoibuka hivi karibuni nchini Sudan ya Kusini na kusababisha watu kadhaa kupoteza maisha na wengine wengi kuyakimbia makazi yao kwa kuhofia usalama wa maisha yao yalimsikitisha sana Baba Mtakatifu Francisko, kiasi cha kumteua Kardinali Peter Turkson, Rais wa Baraza la Kipapa la haki na amani kwenda kusaidia juhudi za upatanisho huko Sudan ya Kusini. Lengo kuu ni kusaidia mchakato wa majadiliano ya amani katika ukweli na uwazi, kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya wananchi wengi wa Sudan ya Kusini.

Kardinali Turkson akiwa nchini Sudan ya Kusini amepata nafasi ya kukutana na kuzungumza na viongozi wa Kanisa na Serikali, ili kuangalia jinsi ya kutekeleza mkataba wa amani uliotiwa sahihi mwaka 2015 pamoja na mambo mengine ni uundwaji wa serikali ya umoja wa kitaifa. Kwa sasa mapigano yanaonekana kusitishwa lakini bado kuna wasi wasi kwamba, mapigano haya yanaweza kuzuka tena na hivyo kusababisha maafa makubwa kwa watu na mali zao.

Mapigano yanapozuka raia wengi wanapoteza maisha yao na wengine wanalazimika kuyakimbia makazi, hali inayovuruga maendeleo ya nchi. Kwa miaka mitano sasa tangu Sudan ya Kusini ilipojipatia uhuru wake kwa kura ya maoni, bado amani, utulivu na maendeleo vimekuwa ni ndoto kwa wengi kutokana na uchu wa mali, madaraka na kinzani za kikabila ambazo hazina mvuto wala mashiko kwa ustawi na maendeleo ya wananchi wengi wa Sudan ya Kusini.

Kardinal Turkson anasikitika kusema wanawake na watoto wengi wamelazimika kukimbilia kwenye nyumba za ibada na shule ili kutafuta hifadhi ya maisha yao. Makanisa yamekuwa msatari wa mbele kuwahudumia wakimbizi na wahamiaji kwa hali na mali. Kardinali Turkson anasema, kuna haja kwa Serikali na viongozi wa upinzani kuhakikisha kwamba, wanarejesha amani, usalama na maendeleo ya watu sanjari na kuweka sera na mikakati ya mabadiliko ya dhati kuelekea uchaguzi mkuu nchini Sudan ya Kusini, unaotarajiwa kufanyika kunako mwaka 2018.

Kardinali Turkson anasema, viongozi wa Serikali na upinzani wamemhakikishia kwamba, wataendeleza mchakato wa mageuzi ambao ulisitishwa kutokana na machafuko ya kisiasa yaliyojitokeza hivi karibuni nchini Sudan ya Kusini. Amewafikishia viongozi wote hawa salam, matashi mema na mshikamano kutoka kwa Baba Mtakatifu Francisko anayewahimiza kwanza kabisa kukutana kama ndugu, ili kujadiliana katika ukweli na uwazi na hatimaye, kusaidia mchakato wa haki, amani na upatanisho wa kitaifa kwa kuaminiana na kuthaminiana. Ni wajibu wao kutambua kwamba wamepewa dhamana na wajibu wa kuwaongoza watu wao katika haki na amani.

Kardinali Turkson anakaza kusema, Vatican kwa kupitia Baraza la Kipapa linaloratibu misaada ya Kanisa Katoliki, Cor Unum linaendelea kujipanga ili kutoa msaada wa hali na mali kwa wakimbizi na wahamiaji wanaoendelea kuteseka kutokana na machafuko ya kisiasa nchini Sudan ya Kusini. Msaada wa haraka zaidi ni huduma ya afya ili kudhibiti magonjwa ya mlipuko yanayoweza kusababisha maafa makubwa zaidi pamoja na kuhakikisha kwamba, watu wanapata chakula cha msaada.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.