2016-07-25 11:16:00

Sala ya kuwasindikiza vijana huko Poland


Waamini wa Parokia ya Mtakatifu Anna iliyoko mjini Vatican kwa muda wa siku tatu wanafanya sala na maombi maalum kwa ajili ya hija ya kitume ya Baba Mtakatifu Francisko nchini Poland kuanzia tarehe 27 Julai hadi 31 Julai 2016 kama sehemu ya maadhimisho ya Siku ya XXXI ya Vijana Duniani kwa mwaka 2016. Sala hii inafikia kilele chake, Jumanne tarehe 26 Julai 2016, Kanisa linapoadhimisha Kumbu kumbu ya Mtakatifu Anna, Mama yake mzazi wa Bikira Maria. Kardinali Angelo Comastri, mhudumu mkuu wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican ataongoza Ibada ya Misa Takatifu, Jumanne asubuhi na jioni, Fumbo la Ekaristi takatifu litaadhimishwa na Askofu mkuu Georg GĂ nswein, Mkuu wa nyumba ya Kipapa.

Parokia hii tangu kunako mwaka 1929 imekuwa na utamaduni wa kufanya Ibada maalum kwa kuomba ulinzi na tunza ya Mtakatifu Anna, Mama yake Bikira Maria. Mama huyu ni kimbilio la wanawake wajawazito wanaoomba usalama wa watoto wao wachanga ambao bado hawajazaliwa, ili kweli waweze kupata ulinzi na tunza ya Mama Anna aliyebahatika kuwa ni Mama wa Bikira Maria aliyepata mimba kwa njia ya Roho Mtakatifu na kumzaa Neno wa Mungu aliyefanyika mwili na kukaa kati ya watu wake.

Taarifa zinaonesha kwamba, hata leo hii, wanawake wengi wajawazito wanakwenda Parokiani hapo kuomba ulinzi na tunza ya Mtakatifu Anna kwa ajili ya vichanga wao, ili hata wao wenyewe waweze kuwa kweli ni vyombo vya Injili ya uhai dhidi ya utamaduni wa kifo unaomwandama mwanadamu katika ulimwengu mamboleo.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.