2016-07-22 15:44:00

Urithi wa Hayati Askofu mkuu Zimowski!


Askofu mstaafu Josè Luis Regrado Marchite, aliyewahi kuwa Katibu mkuu wa Baraza la Kipapa la huduma za kichungaji kwa wafanyakazi katika sekta ya afya, Alhamisi, tarehe 21 Julai 2016 ameongoza Ibada ya Misa Takatifu kwa ajili ya kumkumbuka na kumwombea marehemu Askofu mkuu Zygmunt Zimowski, Rais wa Baraza la Kipapa la huduma za kichungaji kwa wafanyakazi katika sekta ya afya aliyefariki hivi karubini nchini Poland kutokana na ugonjwa wa Saratani ya ini.

Ibada hii imeadhimishwa kwenye Kanisa la Santo Spirito in Sassio mjini Roma na kuhudhuriwa na viongozi wakuu wa Vatican, wafanyakazi, waamini na watu wenye mapenzi mema waliobahatika kuonja huduma ya kichungaji iliyotolewa na Askofu mkuu Zimowski wakati wa uhai wake! Ni kiongozi aliyeendelea kuandika kurasa za Injili kwa njia ya huduma kwa wagonjwa na maskini wa nyakati hizi.

MonsinyoKrzysztof  Nykiel ndiye aliyetoa mahubiri katika Ibada hii ya kumwombea Marehemu Askofu mkuu Zimowski, kwa kumweka chini ya huruma na upendo wa Mungu, mtumishi wake mwaminifu aliyeupenda wito na maisha yake ya Kipadre; akalihudumia Kanisa la Kristo kwa kuwatakatifuza, kuwaongoza na kuwafundisha watu wa Mungu kama Askofu wa Jimbo Katoliki Radom, Poland. Akaonesha Ibada ya pekee kwa Bikira Maria kiasi kwamba, akajitoa bila ya kujibakiza kwa ajili ya huduma ya Uinjilishaji kwa njia ya Radio Maria.

Alikuwa ni Jaalimu nguli katika nyaraka za Mababa wa Mtaguso mkuu wa Pili wa Vatican; mwandishi aliyebobea katika taaluma na fani, aliyebahatika kuandika zaidi ya vitabu 120 na barua 42 za kichungaji. Kwa hakika alikuwa ni Padre na Askofu mwaminifu kwa Kristo na Kanisa lake, alionesha upendo na ukarimu kwa maskini, wagonjwa na wote waliokuwa wanasukumizwa pembezoni mwa jamii; akajenga na kudumisha moyo wa upendo na mshikamano na wote.

Alisaidia kujenga kituo cha huduma ya uponyaji kwa vijana waliokuwa wameathirika kwa matumizi haramu ya dawa zakulevya nchini Poland. Ni Askofu katika utume wake kwenye Baraza la Kipapa la huduma kwa wafanyakazi katika sekta ya afya aliyekazia kwa namna ya pekee kabisa utamaduni wa ukarimu kwa wagonjwa na maskini na kuwataka waamini na watu wote wenye mapenzi mema kuiga mfano wa Msamaria mwema, kushuka na kuinama chini kabisa ili kuganga na kuponya madonda na mahangaiko ya wagonjwa duniani.

Hiki ni kielelezo cha hali ya juu kabisa cha umwilishaji wa matendo ya huruma: kiroho na kimwili, hasa wakati huu, Mama Kanisa anapoadhimisha Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu. Aliwataka wahudumu wa sekta ya afya kuhakikisha kwamba, wanatekeleza dhamana na majukumu yao kwa kuongozwa na dhamiri safi, utu, heshima na haki msingi za binadamu. Watekeleze huduma hii kwa uvumilivu, upole na ukarimu.

Marehemu Askofu mkuu Zimowski alijisadaka maisha yake kwa ajili ya huduma na wala si kwa kuhudumiwa. Hata katika ugonjwa wake, aliendelea kulitumikia Kanisa kadiri ya uwezo wake, hadi pale Kristo Yesu alipochukua ili aweze kupata pumziko la milele. Aliyatolea mateso na mahangaiko yake ya ugonjwa kama sehemu ya kumtolea Mungu sifa, utukufu na shukrani, huku akiachilia mikononi mwa Kristo aliyeteswa, akafa na kufufuka kwa wafu! Alikuwa ni kiongozi mwenye imani thabiti kwa Kristo na Kanisa lake, mwishoni akijiachilia chini ya huruma ya Mungu!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.