2016-07-22 16:13:00

Huruma ya Mungu inavyozima kiu ya mahitaji ya binadamu!


Sala ni mazungumzo yetu na muumba wetu. Ni tendo ambalo linatupatia fursa ya kujifunua mioyo yetu kwa Mungu. Mwanadamu anaalikwa mara nyingi kujiunganisha na Mungu kwa njia hii kwa ajili ya kumsifu kwa sababu ya ukuu wake, kumshukuru kwa neema na fadhili nyingi anazomjalia na kuomba ulinzi na baraka zake ziendelee kukaa naye. Hivyo tunaweza kusema kwamba sala ni uhakika wa uwepo wa Mungu katikati ya jamii ya wanadamu, uwepo ambao unaendelea kumwakikishia mwanadamu usalama katika maisha yake na hivyo kukua katika imani, matumaini na mapendo kwa Mungu.

Neno la Mungu katika Dominika hii ya 17 ya Mwaka linatutafakarisha juu ya uhakika wa uhusiano huu wa sala. Uhakika huo unajionesha kwa kuhakikishiwa usikivu wa Mungu katika sala zetu kwake. Huruma ya Mungu hujibu maombi yetu kwa kadiri ya mahitaji yetu. Tunapomkimbilia yeye katika sala anatusikiliza na anatujalia kadiri ya mahitaji yetu. Kristo anasisitiza katika somo la Injili kwamba “ikiwa ninyi mlio waovu mnajua kuwapa watoto wenu vipawa vyema, je, Baba aliye mbinguni hatazidi sana kuwapa Roho Mtakatifu hao wamwombao?”. Mzaburi anakazia ukweli huu kwa kusema kwamba “siku ile niliyokuita uliniitikia, Ukanifariji nafsi kwa kunitia nguvu”.

Mahusiano yetu na Mungu katika sala yanadhihirisha huruma na upendo wa Mungu ambaye anaendelea kuwaangalia watu wake. Tangu mwanzoni wakati wa uumbaji Mungu ameidhihirisha huruma hiyo na daima ameitikia kilio cha sala ya watumishi wake. Katika Agano la Kale tunashuudia maeneo mengi wana wa Israeli, Taifa teule la Mungu walikuwa wanamlilia Mungu katika maisha yao yote. Mwenyezi Mungu aliendelea kudhihirisha huruma yake na kuisikiliza sala yao hata kama mwanadamu alimkosea. Habari ya Sodoma na Gomora inaonesha huruma hiyo ya Mungu katika kusikiliza na kuipatia nafasi sauti ya mwanadamu anayetubu bila kujali idadi ya wachaji wake ndani yake. Mwenyezi Mungu alisema: “Nikiona katika Sodoma wenye haki hamsini mjini, nitapaacha mahali pote kwa ajili yao” lakini baadaye akasema pia “sitaharibu kwa ajili ya hao kumi”.

Masomo ya leo pia yanatukumbusha jambo lililo muhimu katika sala zetu. Hii ni namna ambavyo tunafanya sala zetu. Pengine mara nyingi sala zetu zinakuwa ni za madai mbele ya Mungu na zaidi kujitanguliza sisi. Sala anayotufundisha Kristo ikiwa ni jibu kwa ombi la mitume wake inatupatia nguzo muhimu za sala iliyo bora. Katika nafasi ya kwanza sala inamhitaji anayesali kutambua mahusiano yake na Mungu. Yeye ni Baba yetu na tunapaswa kujiweka mbele yake kama watoto wake. Hapa inadokezwa fadhila ya unyenyekevu mithili ya mtoto anayejiaminisha mbele ya baba yake. Mtoto mdogo mbele ya wazazi wake anategemea kupata ulinzi na kuwezeshwa katika mahitaji yake muhimu na ya lazima.

Hatua ya pili katika sala ni kumpatia heshima anayostahili huyu Baba yetu. “Jina lako litukuze, ufalme wako uje”. Huenda wengine wakajiuliza, ‘Kwa nini Mungu anapaswa kutukuzwa? Si tayari Mungu ametukuka?’ Ni kweli kwamba Mungu ndiye aliyetukuka zaidi katika ulimwengu wote, lakini hilo halimaanishi kwamba wanadamu wote humwona hivyo. Katika Biblia, maana ya msingi ya neno la Kiebrania linalotafsiriwa “utukufu” ni “uzito.” Linarejelea kitu chochote ambacho humfanya mtu aonekane na wengine kuwa mwenye kutokeza au mashuhuri. Linapotumiwa kumhusu Mungu, neno hilo hurejelea kile ambacho humfanya Mungu awe mwenye kutokeza kwa wanadamu. Pia sala bora inaendelea kumfanya Mungu atawale yaani ufalme wake uje kwetu. Sifa hii inaunganika na ombi linalofuata ambalo hututaka kutimiza mapenzi yake na Injili inatuambia “hapa duniani kama huko mbinguni” ikimaanisha kwamba ni utayari wa kupokea baraka na neema za Mungu kwa kadiri ya mahitaji.

Mara nyingi sisi wanadamu huwa tunamdai Mwenyezi Mungu na sala zetu zinatawaliwa na matamanio yetu tu wala si katika kulitukuza jina la Mungu. Mungu wetu ni mithili ya Baba mwema. Kamwe hawezi kutupatia jiwe badala ya mkate, nyoka badala ya samaki au nge badala ya yai. Yeye anajua yote na mahitaji yetu anayafahamu kadiri ya uhitaji wake. Wakati mwingine unaweza kumwomba Mwenyezi Mungu uwezo wa kuelewa na kufaulu mitihani yako lakini yaweza kuwa ni kwa ajili ya kutafuta tambo mbele ya wenzako. Mungu wetu katika upendo wake mkuu anaweza kukupitisha katika njia ngumu na hata pengine kutofaulu katika hatua fulani kusudi akufunze unyenyekevu na hata pale utakapofanikiwa basi ukumbuke pia zipo nyakati nyingine mbaya. Kibinadamu twaweza kutoelewa hivyo lakini kama tukitafakari na kwa uwezo wa neema ya Mungu tutaona kwamba tulichopokea ni yai wala si nge na kwa njia hiyo tutaendelea kuimarika katika tunu njema za utu.

Sehemu inayofuatia ya sala hii inayaonesha maombi yetu muhimu mbele ya Mungu Daima: utupe leo mkate wetu wa kila siku ikimaanisha kwamba kujisikia uhitaji wa daima mbele ya Baba yetu mwema; utusamehe makosa yetu kwa sababu tunakubali udhaifu wetu na tunajifunza zaidi kwa kuona kuwa hata wengine wanakosa. Hivyo tunajinyenyekeza mbele ya Mungu; na mwisho ni kuomba kuepushwa na maovu yanayotuzingira daima. Sehemu hii inaonesha umuhimu wa kujiuliza umuhimu wa kile unachokiomba kwa Mungu na ulazima au uhitaji wake kwako. Je, unachokiomba kitatimiza mahitaji yako ya kila siku? Mahitaji ambayo yataendelea kukuza mahusihano yake na muumba wako na pia jirani zako? Kwa maneno mengine inatupeleka kuepuka ulafi na kujifikiria wenyewe tu kila siku. Hapa inatutepeleka hata katika kuuona huitaji wetu kwa ajili ya kutimiliza uhitaji wa wengi iwe ni kwa kuwakirimu au kwa kuwaombea mema katika maisha yao.

Sehemu hiyo ya maombi yatuhusuyo sisi inatupeleka katika hatua nyingine muhimu ya kutafuta upatanisho kati yetu na Mungu na kati yetu sisi wenyewe. Kama tulivyoanza kutafakari hapo juu sala ni mahusiano na hivyo mahusiano hudokeza uwepo wa suluhu kati ya wawili wanaohusiana. Sala zetu kama hazitupeleki katika kupata upatanisho zinakosa kiungo muhimu. Ni vigumu kueleweka katika mazingira ya kawaida watu wanaodaiana kuhusiana vema. Na mwisho ombi letu kwa Mungu linapaswa kunuia kutafuta ulinzi wake dhidi ya upinzani wa shetani. Hivyo ni sehemu ianyotutaka kuomba neema zake na kutafakari Neno lake kwa ajili ya kupokea nguvu na njia za kuepa vishawishi vya muovu.

Jambo la mwisho la kutafakari leo hii ni udumifu katika sala. Mwanadamu hapaswi kuacha kuungana na Mungu kwa njia ya sala kwa sababu kwanza Mungu kwa upande wake haachi kumwangalia mwanadamu. Hivyo hali zetu za kujiweka mbele ya Mungu katika kutegemea baraka na neema zake kwa ajili ya maisha yetu ya kila siku inapaswa kuwa ni ya kudumu. Pili, mwanadamu daima anahitaji kuuona ukuu wa Mungu na kumtukuza, kutafuta yaliyo mapenzi yake na kuyatekeleza na mwisho kuzitegemea fadhili zake katika mahitaji ya kila siku kiroho na kimwili. Mfano wa Babu yetu katika imani Abrahamu katika somo la kwanza na mtu aliyekwenda kuomba usiku kwa rafiki yake hadi akapata mahitaji yake inatuimarisha katika hilo.

Kifo cha Kristo msalabani, anatuambia Mtakatifu Paulo katika somo la pili, kinatuondolea dhambi ambayo ilikuwa imetutenga na Mungu na “kuigongomea Msalabani”. Hivyo basi sisi Wakristo tumefanywa kuwa watoto huru wa Mungu. Tunaalikwa leo kujiweka mbele yake Mungu Baba yetu kama watoto wake huku tukitumaini katika huruma yake kwa kuwa huruma hiyo hujibu maombi yetu kwa kadiri ya mahitaji yetu.

Kutoka studio za Radio Vaticani mimi ni Padre Joseph Peter Mosha.








All the contents on this site are copyrighted ©.