2016-07-21 14:44:00

SECAM: Luanda, Angola kuna mambo huko!


Maadhimisho ya Mkutano wa 17 wa Shirikisho la Mabaraza ya Maaskofu Katoliki Afrika na Madagascar, SECAM yamefunguliwa rasmi tarehe 19 Julai 2016 kwa Ibada ya Misa Takatifu iliyoadhimishwa kwenye Kanisa kuu la Familia Takatifu na kuongozwa na Askofu mkuu Gabriel Mbilingi, Rais wa SECAM aliyekazia umuhimu wa familia ya Mungu Barani Afrika kusoma, kutafakari na kumwilisha Wosia wa Baba Mtakatifu Francisko “Furaha ya upendo ndani ya familia” “Amoris laetitia” kadiri ya mazingira na vipaumbele vya maisha na utume wa familia Barani Afrika.

Lengo la maadhimisho haya ni kuliwezesha Kanisa Barani Afrika kuibua mbinu mkakati wa shughuli za kichungaji kwa Familia ya Mungu Barani Afrika, ili kukabiliana na changamoto zinazoendelea kuibuliwa katika ulimwengu wa utandawazi na maendeleo ya sayansi na teknolojia.  Katika hotuba yake ya kuwakaribisha wajumbe wa SECAM nchini Angola, Bwana Manuel Vicente, Makamu wa Rais nchini Angola amewataka wajumbe kukuza na kudumisha uhusiano na ushirikiano kati ya Serikali ya Kanisa kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya wengi hususan kuhusiana na masuala ya kimaadili na utu wema.

Serikali na Kanisa havina budi kushirikiana kwa karibu zaidi katika mapambano dhidi ya nyanyaso za watoto wadogo, kumong’onyoka kwa kanuni maadili na utu wema; vipigo vya wanawake majumbani, ili hatimaye, Jamii iweze kukuza na kudumisha tunu msingi za maisha ya ndoa na familia. Ni matumaini ya Serikali ya Angola kwamba, Kanisa litaendelea kushirikiana na Serikali katika kukuza na kudumisha kanuni maadili, haki msingi za binadamu, heshima, demokrasia na utawala bora.

Kwa upande wake, Askofu mkuu Gabriel Mbilingi, Rais wa SECAM alitoa historia fupi ya SECAM, mafanikio, matatizo na changamoto zilizopo katika maisha na utume wa Kanisa Barani Afrika. Amepongeza juhudi zilizofikiwa hadi sasa kwa SECAM kupata mwakilishi wa kudumu kwenye Umoja wa Afrika. SECAM inatumaini kwamba, kutakuwepo na ushirikiano wa karibu zaidi kati ya Kanisa Katoliki Barani Afrika na Serikali mbali mbali kupitia Umoja wa Afrika

Salam na matashi mema kutoka Shirikisho la Vyama vya Kikatoliki vya Biblia yamejikita katika kukazia umuhimu wa Maandiko Matakatifu katika mchakato wa maisha na utume wa Kanisa Barani Afrika. Shughuli na mikakati ya kichungaji haina budi kupata chimbuko lake katika Maandiko Matakatifu na kwamba, Biblia ipewe kipaumbele cha pekee katika maisha ya waamini Barani Afrika, ili waweze kujisomea, kulitafakari na hatimaye, kulimwilisha Neno la Mungu katika maisha yao.

Familia ya Mungu Barani Afrika isaidie pia mchakato wa kutafsiri Biblia katika lugha mbali mbali ili waamini wengi waweze kufikiwa na Neno la Mungu hasa kwa njia ya Uinjilishaji wa kina unaogusa mahitaji ya mtu mzima: kiroho na kimwili. Kuna haja ya kuboresha utume wa Biblia Barani Afrika! Wajumbe wa SECAM wamehakikishiwa sala kutoka kwa vyama 335 vya Biblia vinavyofanya utume wake katika nchi 127 duniani.

Kwa upande wake, Shirika la Misaada la Baraza la Maaskofu Katoliki Ujerumani, “Miserior” ambalo tangu kunako mwaka 1958 limekuwa mdau mkubwa wa huduma ya maendeleo kwa familia ya Mungu Barani Afrika, linasema, linapenda kuendelea kuunga mkono huduma ya Kanisa katika mchakato wa kujenga na kuimarisha haki na amani Barani Afrika; utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote kama anavyokaza kusema Baba Mtakatifu Francisko; ukweli, uwazi, uaminifu wa matumizi ya rasilimali ya dunia na mali ya Kanisa katika ujumla wake.

Miserior inapenda pia kuijengea familia ya Mungu Barani Afrika uwezo wa kiuchumi ili kujiletea maendeleo yake, kwa kukuza utu, heshima na mafao ya wengi. Miserior itashirikiana na SECAM katika kukabiliana na changamoto katika masuala ya usawa wa kijinsia pamoja na kudumisha haki msingi za wanawake Barani Afrika.

Wakati huo huo, Shirika la Misaada la “Missio” kutoka Ujerumani ambalo limekuwa mstari wa mbele katika kuzijengea uwezo wa kiuchumi familia nyingi Barani Afrika linasema, Mababa wa Sinodi ya Maaskofu kwa ajili ya familia kwa miaka miwili wametilia mkazo umuhimu wa kukuza na kudumisha tunu msingi za maisha ya ndoa na familia sanjari na kuzijengea uwezo familia, ili ziweze kusimama imara na thabiti kutangaza na kushuhudia Injili ya familia na uhai, dhidi ya utamaduni wa kifo. Malezi na majiundo makini kwa walei ni muhimu sana.

Missio itaendelea kushirikiana na AMECEA katika kuwanoa wafanyakazi wa Kanisa katika masuala ya rasilimali fedha. Katika kipindi cha miaka mitatu, Missio imechangia kiasi cha Euro millioni 34 kwa ajili ya kugharimia miradi mbali mbali ya maendeleo Barani Afrika.

Shirika la Huduma ya Misaada ya Kanisa Katoliki, “Catholic Relief Services” katika salam zake, limeitaka SECAM kusimama kidete katika mapambano dhidi ya umaskini, magonjwa, vita na baa la njaa linaloendelea kudhalilisha utu na maisha ya watu wengi Barani Afrika. UKIMWI na EBOLA ni kati ya magonjwa ambayo yanahatarisha sana maisha ya nguvu kazi Barani Afrika. Kanisa Barani Afrika lina mchango mkubwa katika ustawi na maendeleo ya familia ya Mungu Barani Afrika. Kanisa limekuwa mstawi wa mbele kulinda na kudumisha utu wa binadamu; tunu msingi za maisha ya ndoa na familia; utakatifu wa maisha ya binadamu pamoja na dhamana ya wazazi na walezi kwa elimu, majiundo makini na malezi kwa watoto wao.

Takwimu zinaonesha kwamba, katika kipindi cha miaka 30 kuanzia sasa idadi ya watu Barani Afrika itaongezeka maradufu kutoka billioni 1. 1 ya sasa hadi kufikia billioni 2. 5 ifikapo mwaka 2050, changamoto kubwa kwa Serikali na Kanisa katika ujumla wake. Hapa umoja, upendo na mshikamano ni nyenzo muhimu sana katika ujenzi wa ufalme wa Mungu hapa duniani.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.