2016-07-21 15:29:00

Mtandao wa huduma ya ukarimu!


Changamoto ya afya mara nyingi inakwenda sanjari na umaskini pamoja na udhaifu wa kibinadamu! Hali hii inaweza kuwa mbaya zaidi, kama inawakumba watoto na vijana katika familia zao. Ili kukabiliana na changamoto ya ugonjwa ambayo wakati mwingine inasababisha familia kukata tamaa ya maisha, kuna haja ya kujenga na kudumisha mtandao wa mshikamano wa huduma ndani na nje ya hospitali ili kuwahudumia watoto wagonjwa kwa hali na mali.

Hii ni changamoto ambayo imetolewa hivi karibuni na Kardinali Pietro Parolin, Katibu mkuu wa Vatican alipokuwa anazindua taarifa ya sekta ya afya na utafiti wa kisayansi, kwa mwaka 2015 kutoka Hospitali ya Bambino Gesù inayomilikiwa na kuendeshwa na Vatican. Kardinali Parolin anasema, mtandao wa mshikamano anaokazia ni ule unaofumbatwa katika ukarimu unaotibu na kuganga.

Huu ni mshikamano unaowaambata madaktari, wazazi na watoto wagonjwa, na wanaposhirikiana na kusikamana kwa dhati, wanaiwezesha hospitali ya Bambino Gesù kuwa ni shuhuda wa huduma ya upendo ya Papa na Kanisa inayotolewa kwa unyenyekevu na akili. Kwa mara ya kwanza taarifa hii imewasilishwa kwenye Makao makuu ya Taasisi ya Kipapa ya Sayansi, mahali muafaka pa kufanyia tafakari, tafiti na majaribio ya kisayansi na athari zake katika maisha ya watu.

Kardinali Parolin amewashukuru kwa juhudi, maarifa na ujuzi ambao wanaendelea kuchangia kwa Kanisa ili kukabiliana na changamoto na hatimaye kutoa majibu muafaka kwa changamoto hizi. Katika miaka ya hivi karibuni, Hospitali ya Bambino Gesù imeendelea kuboresha huduma na tafiti kwa kutoa kipaumbele cha kwanza kwa watoto wagonjwa na familia zao; kwa kuheshimu na kuzingatia haki na mahitaji yao msingi.

Huu ndio utume wa hospitali ili kufanya tafiti na uchunguzi wa magonjwa pamoja na kutoa tiba inazingatia kanuni maadili na miiko ya kazi, kielelezo cha hali ya juu kabisa cha weledi na ukweli. Kutokana na tunu hizi msingi, Hospitali ya Bambino Gesù inaendelea kujipambanua kuwa ni Jumuiya inayopania kuboresha afya, ustawi na maendeleo ya wagonjwa kwa kujikita katika tafiti, huduma na kinga, mambo ambayo ni ya kujivunia kabisa!

Kardinali Parolin anakaza kusema, kwa kujiwekea mkakati wa kutoa huduma bora zaidi kwa watoto wagonjwa, kuna haja ya kuwekeza zaidi katika tafiti na maboresho katika huduma kadiri ya mahitaji ya watoto wagonjwa. Hospitali hii inaendelea kuchangia kwa kiasi kikubwa huduma bora zaidi kwa watoto ndani na nje ya Italia kwa kupandikiza viungo pamoja na kutoa tiba kwa magonjwa ya muda mrefu na changamani.

Mwaka 2015 umekuwa ni mwaka wenye mafanikio makubwa kutokana na huduma bora za afya zinazoendelea kutolewa hospitalini hapo kwa watoto wagonjwa kutoka ndani na nje ya Italia, kwa kutoa kipaumbele cha kwanza kwa utu na heshima ya watoto wagonjwa. Ni hospitali inayojikita katika tafiti, tiba na ukarimu hasa kwa kusaidia kuwafunda madaktari watakaosaidia kutoa huduma makini kwenye hospitali mahalia, kama ilivyo kwa madaktari kutoka Jamhuri ya Afrika ya Kati, ambao mara baada ya hija ya kitume ya Baba Mtakatifu Francisko Barani Afrika, Hospitali ya Bambino Gesù imechukua dhamana ya kuwasomesha madaktari watakaosaidia kuboresha huduma za watoto wadogo nchini humo.

Uzinduzi wa taarifa hii umehudhuriwa na Askofu Marcelo Sanchèz Sorondo. Mkuu wa Taasisi ya Kipapa ya Sayansi, Mama Mariella Enoc, Rais wa Hospitali ya Bambino Gesù na Dr. Bruno Dallapiccola, Mkurugenzi wa Idara ya Utafiti.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.