2016-07-20 07:02:00

Siku ya 31 ya Vijana Duniani: Hija ya imani na udugu!


Heri wenye rehema maana hao watapata rehema! Hii ndiyo kauli mbiu inayoongoza maadhimisho ya Siku ya 31 ya Vijana Duniani yanayofanyika Jimbo kuu la Cracovia kuanzia tarehe 26 - 31 Julai 2016. Tayari makundi ya vijana yameanza kuelekea nchini Poland kwa maadhimisho haya! Baba Mtakatifu Francisko katika ujumbe wake kwa njia ya video anasema, kumekucha! Anasubiri kwa hamu kuweza kukutana na vijana kutoka sehemu mbali mbali za dunia pamoja na kutembelea nchi ya Poland.

Matukio yote haya yanafumbatwa katika maadhimisho ya Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu; kumbu kumbu endelevu ya Mtakatifu Yohane Paulo II, muasisi wa Siku ya Vijana Duniani na kiongozi makini aliyeiongoza familia ya Mungu nchini Poland katika hija ya historia kuelekea uhuru wa kweli! Baba Mtakatifu anapenda kuwashukuru na kuwapongeza vijana wa kizazi kipya kutoka Poland ambao wamejitaabisha usiku na mchana kwa ajili ya maandalizi haya, lakini zaidi kwa njia ya sala, ili kufanikisha siku ya Vijana Duniani huko Jimbo kuu la Cracovia.

Baba Mtakatifu Francisko anapenda kuwabariki vijana kutoka Ulaya, Afrika, Amerika, Asia na Oceania pamoja na kuzibariki nchi wanamotoka, nia zao njema wanapoelekea Jimbo kuu la Cracovia, ili kweli safari yao, iwe ni hija ya imani na udugu. Anawaombea ili Mwenyezi Mungu aweze kuwakirimia neema ya kuweza kuonja ndani mwao ”Heri wenye rehema maana hao watapata rehema”. (Mt. 5:7).

Baba Mtakatifu Francisko anasema, anatamani kukutana na vijana kutoka sehemu mbali mbali za dunia ili kutoa kielelezo kipya cha utulivu unaokumbatiwa kwa uwepo wa nyuso mbali mbali za binadamu kutoka katika kabila, lugha na tamaduni wote wakiwa wameungana kwa njia ya jina la Yesu ambaye ni Sura ya huruma ya Mungu.

Baba Mtakatifu akiigeuikia familia ya Mungu nchini Poland anasema kutoka moyoni mwake kwamba, anajisikia kuwa ni zawadi maalum kutoka kwa Mwenyezi Mungu kwenda kuwatembelea, kwani hawa ni watu ambao katika historia ya maisha ya nchi yao wamekumbana na magumu ya maisha, lakini wameweza kuvuka yote haya kwa njia ya imani pamoja na ulinzi na tunza ya Bikira Maria. Baba Mtakatifu ana uhakika kwamba hija yake kwenye Madhabahu ya Bikira Maria wa Czestochowa itakuwa ni nafasi kwake kuweza kuzama katika imani ambayo imejaribiwa sana na kwa hakika litakuwa ni tukio jema sana kwake.

Baba Mtakatifu anapenda pia kuchukua nafasi hii kuwashukuru kwa sala wanazoendelea kumtolea Mwenyezi Mungu kama sehemu ya maandalizi ya hija yake kitume nchini Poland. Anawashukuru wakleri, watawa, waamini walei lakini kwa namna ya pekee familia ambazo anapenda kuwakabidhi wosia wake wa kitume ”Furaha ya upendo ndani ya familia”. Afya ya kimaadili na kiroho kwa taifa lolote lile inajionesha kwa njia ya familia: ndiyo maana Mtakatifu Yohane Paulo II alipenda kutoa kipaumbele cha pekee kwa wanandoa watarajiwa, wanandoa wapya pamoja na familia. Baba Mtakatifu anaitaka familia ya Mungu nchini Poland kuendelea kujikita katika mwelekeo huu. Mwishoni, Baba Mtakatifu anasema, ujumbe huu ni alama ya upendo wake kwao na anawataka waendelee kuwa wameshikamana kwa njia ya sala! Anawakia wote heri na baraka, wakutane huko Poland panapo majalia!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.