2016-07-20 07:52:00

Mshikamano wa upendo na wananchi wa Amerika ya Kusini!


Monsinyo Segundo Tejado Munoz, Katibu mkuu msaidizi wa Baraza la Kipapa linaloratibu misaada ya Kanisa Katoliki, Cor Unum amerejea kutoka katika safari ya kikazi huko nchini Colombia na Equador alikokwenda kushuhudia imani inayomwilishwa katika matendo, kielelezo cha Baba Mtakatifu Francisko anavyoguswa na mahangaiko ya maskini na watu wanasoukumizwa pembezoni mwa jamii. 

Katika mahojiano maalum na Gazeti la L’Osservatore Romano, Monsinyo Munoz anasema, miradi 80 ya huduma za kijamii imepitishwa na itagharimiwa na Mfuko wa Maendeleo ya Watu wa Amerika ya Kusini, baada ya kuchambuliwa na wakurugenzi wakuu wa Mfuko huo katika mkutano wake uliohitimishwa hivi karibuni huko mjini Bogotà, nchini Colombia. Miradi hii ni midogo midogo lakini inayokidhi mahitaji ya watu wa kawaida katika mchakato wa maboresho ya maisha yao katika sekta ya kilimo, ufugaji, kazi za mikono na elimu ambayo ni mkombozi wa maskini.

Monsinyo Munoz anasema, miradi mingi imejikita katika maboresho ya sekta ya elimu ili kuweza kuwajengea wananchi mahalia uwezo wa kukabiliana na changamoto za maisha kwa ujasiri mkubwa. Lengo ni kumhudumia mtu mzima: kiroho na kimwili. Itakumbukwa kwamba, miradi hii baada ya kupitishwa na uongozi wa Mfuko wa Maendeleo Watu wa Amerika ya Kusini unaosimamiwa na kuratibiwa na Cor Unum, miradi hii hufadhiliwa na Baraza la Maaskofu Katoliki Italia, CEI.

Kwa mwaka 2016 miradi mingi iliyopitishwa kwenye mkutano huu ni kwa ajili ya wananchi wa Perù, Colombia, Equador na Bolivia. Nchi nyingine ni Argentina, Uruguay na Paraguay bila kusahau wananchi wa kutoka katika Visiwa vya Caraibi. Kanisa limekuwa mstari wa mbele kuonesha mshikamano wa huduma na upendo kwa waathirika wa majanga asilia kama ilivyotokeza nchini Haiti kwa kujenga shule, Ufilippini kwa kujenga kituo cha wazee  na watoto yatima; kituo ambacho kilizinduliwa na Baba Mtakatifu Francisko wakati wa hija yake ya kitume nchini Ufilippini kunako mwezi Januari, 2015 na kwamba, msaada mwingine uliotolewa kwa wananchi wa Japan walioathirika na Tsunami.

Baba Mtakatifu anapenda kuonesha kwa matendo jinsi ambavyo imani inapaswa kumwilishwa katika uhalisia wa maisha ya watu. Kwa sasa jicho la huruma na upendo kutoka kwa Baba Mtakatifu Francisko linaelekezwa huko Equador kwa ajili ya kusaidia ujenzi wa shule na hospitali ili kusaidia kumwilisha matendo ya huruma katika maisha ya wananchi wote pasi na ubaguzi.

Monsinyo Munoz anasema wakati wa ziara yake ya kikazi huko Amerika ya Kusini alikuwa ameandamana na Askofu mkuu Giacomo Guido Ottonelo, Balozi wa Vatican nchini Equador. Wametembelea na kujionea maeneo mbali mbali yaliyoharibiwa kutokana na tetemeko la ardhi na kwamba, Cor Unum itachangia kiasi cha Euro 600, 000 kwa ajili ya kukarabati shule inayomilikiwa na kuendeshwa na Kanisa. Mipango iko mbioni kwa ajili ya ujenzi wa makazi kwa ajili ya familia maskini zinazoishi katika mazingira magumu. Kadiri fedha itakavyopatikana mradi huu utaendelea kuboreshwa kama sehemu ukarimu wa Kanisa kwa maskini!

Bado pia kuna haja ya ujenzi wa nyumba za ibada kwa majimbo kadhaa nchini Equador, ili kusaidia juhudi zinazofanywa na familia ya Mungu nchini humo, licha ya umaskini na hali ngumu ya uchumi. Hiki ni kielelezo cha mshikamano wa umoja, upendo na udugu kutoka kwa Baba Mtakatifu Francisko kwa waathirika wa majanga asilia huko Equador. Itakumbukwa kwamba, Baba Mtakatifu Francisko mwaka 2015 alitembelea nchini humo na bado watu wengi wanaikumbuka hija hii ya kitume!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.