2016-07-20 11:45:00

Jubilei ya miaka 800 ya Msamaha wa Assisi!


Baba Mtakatifu Francisko tarehe 4 Agosti 2016 atatembelea mji wa Assisi ili kusali kwenye Kikanisa cha “Porziuncola” ambacho kwa mapenzi ya Mungu na ugunduzi wa Mtakatifu Francisko wa Assisi, katika kipindi cha miaka 800 kimekuwa ni chemchemi ya neema na baraka kwa watu kutoka sehemu mbali mbali za dunia. Hija hii binafsi ya Baba Mtakatifu ni sehemu ya maadhimisho ya Jubilei ya miaka VIII ya Msamaha wa Assisi, itakayoadhimishwa kwa Ibada ya Misa Takatifu hapo tarehe 2 Agosti 2016 na Kardinali Gualtiero Bassetti, Askofu mkuu wa Jimbo kuu la Perugia.

Matukio makuu matatu yanayofumbatwa katika hija hii binafsi ya Baba Mtakatifu Francisko huko Assisi ni: Sala binafsi, tafakari kwa waamini watakaokuwa wamehudhuria katika eneo hili kutoka katika Injili ya Mathayo 18: 21- 28: kuhusu huruma mwishoni, Baba Mtakatifu atawatembelea Watawa wanaotunzwa kwenye Kanda ya “Porziuncola”. Baba Mtakatifu atakapowasili jioni mjini Assisi atapokewa na viongozi wa Kanisa na Serikali mahalia. Kabla ya kuondoka na kurejea tena mjini Vatican atapata nafasi ya kusalimiana na waamini pamoja na mahujaji watakaokuwa kwenye Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Francisko wa Assisi, huko Assisi.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.