2016-07-19 14:20:00

SECAM: Kumekucha Luanda, Angola!


Shirikisho la Mabaraza ya Maaskofu Katoliki Afrika na Magadascar, SECAM, Jumanne tarehe 19 Julai 2016 limeanza maadhimisho ya mkutano mkuu wa 17 unaowashirikisha wajumbe 150 kutoka ndani na nje ya Bara la Afrika. Mkutano huu unafunguliwa kwa Ibada ya Misa Takatifu kwenye Kanisa kuu la Familia Takatifu Jimbo kuu la Luanda, Angola. Mkutano huu utafungwa rasmi hapo tarehe 25 Julai 2016.

“Familia Barani Afrika: Jana, Leo na Kesho kadiri ya mwanga wa Injili” ndiyo kauli mbiu inayoongoza maadhimisho haya ili kuweza kupembua kwa kina na mapana sera na mikakati itakayotumiwa na familia ya Mungu Barani Afrika ili kuimarisha utume wa familia mintarafu Wosia wa Kitume uliotolewa na Baba Mtakatifu Francisko “Furaha ya upendo ndani ya familia”. Wajumbe wa SECAM wanajadili tema hii kadiri ya mazingira ya familia ya Mungu Barani Afrika.

Kamati tendaji ya SECAM iliyowasili mjini Luanda, Jumatatu tarehe 18 Julai 2016 lilifanya kikao cha maandalizi ya mkutano mkuu wa 17 wa SECAM. Familia ya Mungu Barani Afrika anasema Askofu mkuu Thomas Msusa wa Jimbo kuu la Blantyre, Malawi inataka kuonesha mshikamano wa dhati katika kulinda, kutetea na kudumisha Injili ya familia. SECAM inataka kuwa na sauti moja ili kutekeleza dhamana na utume wake wa kinabii dhidi ya ukosefu wa haki msingi za binadamu, ili hatimaye, kulinda utu na heshima ya binadamu.

Ni mkutano ambao pia unapenda kuimarisha SECAM kwa hali na mali, ili iweze kutekeleza dhamana na majukumu yake barabara, tayari kumkaribisha Khalifa wa Mtakatifu Petro katika maadhimisho ya Jubilei ya miaka 50 tangu kuanzishwa kwa SECAM kunako mwaka 1969 wakati Mwenyeheri Paulo VI alipotembelea Bara la Afrika kwa mara ya kwanza katika historia ya Kanisa. Itakumbukwa kwamba, mkutano mkuu wa SECAM, mara ya mwisho uliadhimishwa kuanzia tarehe 8- 15 Julai 2013 huko Kinshasa, nchini DRC kwa kuongozwa na kauli mbiu “Kanisa Barani Afrika kwa ajili ya huduma ya upatanisho, haki na amani”.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.