2016-07-18 10:03:00

SECAM kushiriki katika utekelezaji wa ajenda za maendeleo!


Hivi karibuni, Shirikisho la Mabaraza ya Maaskofu Katoliki Afrika na Madagascar, SECAM liliendesha semina maalum kuhusu mabadiliko ya tabiachi, uhakika na usalama wa chakula. Baada ya semina hii, wajumbe waliitaka SECAM kuhakikisha kwamba inashirikiana na wadau mbali mbali ili familia ya Mungu Barani Afrika iweze kufaidika na ujuzi na maarifa mbali mbali yanayotolewa katika maeneo haya, ili kushiriki vyema katika utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote pamoja na kupambana na baa la njaa; mambo ambayo yanendelea kuchangia udhalilishaji wa utu na heshima ya binadamu.

Wajumbe wamelishauri Shirikisho la Mabaraza ya Maaskofu Katoliki Afrika na Madagascar kushiriki kikamilifu katika utekelezaji wa Agenda za Maendeleo Barani Afrika ifikapo mwaka 2063; Maendeleo endelevu kwa mwaka 2030 kutoka Umoja wa Mataifa pamoja na utekelezaji wa makubaliano ya Itifaki ya Paris, kuhusu mchakato wa kudhibiti athari za mabadiliko ya tabianchi. Wajumbe walipembua kwa kina mapana ili kuangalia utekelezaji wa Waraka wa kitume wa Baba Mtakatifu Francisko, juu ya utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote, Laudato si katika ngazi ya kikanda, kitaifa na kijimbo.

Wajumbe wanakaza kusema, mambo yote haya ni muhimu sana kama sehemu ya mchakato wa Uinjilishaji wa kina unaogusa mahitaji ya mtu mzima Barani Afrika sanjari na mapambano dhidi ya baa la njaa, umaskini na uharibifu wa mazingira, mambo yanayoendelea kuchangia maafa makubwa kwa watu na mali zao. Wajumbe wamejiwekea kalenda ya miaka mitatu, ili kuangalia ni jinsi gani ambavyo Kanisa limeweza kutekeleza masuala ya uhakika na usalama wa chakula sanjari na kudhibiti athari za mabadiliko ya tabianchi kama ilivyokubalika na kutiwa sahihi kwenye mkutano wa kimataifa juu ya udhibiti wa mabadiliko ya tabianchi kwenye Itifaki ya Paris, Ufaransa.

Ufuatiliaji huu unaanza kutekelezwa kuanzia mwaka 2016- 2018. Wajumbe wamekubaliana kimsingi kwamba, wataendelea kushirikishana habari mintarafu mchango wa Kanisa katika uragibishaji wa masuala yanayohusiana na mabadiliko ya tabianchi na usalama wa chakula miongoni mwa mtandao wa wajumbe hawa. Semina hii ilifunguliwa rasmi na Padre Joseph Komakoma, Katibu mkuu wa SECAM kwa niaba ya Askofu Gabriel Mbilingi, Rais wa Shirikisho la Mabaraza ya Maaskofu Katoliki Afrika na Madagascar, SECAM.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.