2016-07-18 06:55:00

Msimwage damu ya ndugu zenu!


Baba Mtakatifu Francisko mara baada ya Sala ya Malaika wa Bwana kwenye Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican, Jumapili tarehe 17 Julai 2016 aliyaelekeza macho na mawazo yake mjini Nice, nchini Ufaransa ambako Alhamisi, tarehe 14 Julai 2016 kulitokea mauaji ya kigaidi ambako watu 84 walipoteza maisha na wengi wao wakiwa ni watoto wadogo. Baba Mtakatifu kwa mara nyingine tena amependa kuonesha uwepo wake wa karibu kwa familia zilizoguswa na kutikiswa na maafa haya na kwamba, anapenda pia kuonesha ukaribu wake kwa nchi nzima ya Ufaransa wakati huu wa maombolezo.

Baba Mtakatifu anawaombea marehemu wote waliotangulia mbele ya haki, huruma ya Mungu, ili waweze kupumzika katika usingizi wa amani. Mwenyezi Mungu mwingi wa huruma na mapendo awasaidie majeruhi kuweza kupona haraka pamoja na kuzifariji familia zote zinaomboleza. Anamwomba Mwenyezi Mungu afutilie mbali mipango ya kigaidi inayopandikiza mbegu ya utamduni wa kifo unaofumbatwa katika chuki, uhasama na hali ya kutaka kulipizana kisasi. Baba Mtakatifu Francisko anapenda kuwakumbatia wananchi wa Nice na Ufaransa katika ujumla wao katika upendo wa kibaba na kidugu. Baba Mtakatifu ametumia nafasi hii kusali kwanza kwa ukimya na waamini na mahujaji waliokuwa wamefurika kwa wingi kwenye Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican. Baadaye, wote hawa akawapatia baraka zake za kitume na kuwatakia Jumapili njema!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican








All the contents on this site are copyrighted ©.