2016-07-15 14:26:00

Ufaransa yatikiswa tena na mashambulizi ya kigaidi!


Padre Federico Lombardi, Msemaji mkuu wa Vatican katika taarifa yake kwa vyombo vya habari anasema, Vatican imefuatilia kwa umakini na wasi wasi mkubwa taarifa za mauaji ya kigaidi yaliyofanyika huko Nice, Ufaransa na kusababisha watu 84 kupoteza maisha na watoto 54 kulazwa hospitalini mjini humo. Vatican inapenda kushiriki na kuonesha mshikamano na wananchi wote wa Ufaransa walioguswa na kutikiswa na shambulizi hili la kigaidi lililofanywa Alhamisi, tarehe 14 Julai 2016. Hii ni Siku ambayo ilipaswa kuwa ni sherehe ya kitaifa, lakini imegeuka kuwa ni siku ya majonzi na maombolezo.

Vatican inalaani kwa nguvu zote mauaji na vitendo vya kigaidi vinavyoendelea kuhatarisha amani na mafungamano ya kijamii. Taarifa kutoka Paris, Ufaransa zinasema kwamba, dereva wa lori aliyehusika na mauaji ya kigaidi ametambuliwa na vyombo vya ulinzi na usalama. Inasadikiwa kwamba, alikuwa na umri wa miaka 31 na ni wananchi wa Ufaransa. Viongozi mbali mbali wa kitaifa na kimataifa wamelaani vitendo hivi vya kigaidi vinavyopaswa kushughulikiwa na Jumuiya ya Kimataifa katika hali ya umoja ili kuhakikisha kwamba, amani, usalama na utulivu vinarejeshwa tena katika medaniĀ  za kimataifa.

Habari kutoka Umoja wa Mataifa zinasema kwamba, Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa limelaani mauaji ya kigaidi yaliyotokea huko Nice, Ufaransa na kwamba, vitendo vya kigaidi katika mfumo wake wote vinahatarisha amani, usalama na mafungamano ya Jumuiya ya Kimataifa. Wajumbe wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa wanasema, kuna haja ya kuhakikisha kwamba wahusika wote wa vitendo vya kigaidi wanafikishwa kwenye vyombo vya sheria, ili mkondo wa sheria kitaifa na kimataifa uweze kufanya kazi yake.

Kwa upande wake, NATO inasema vitendo vya kigaidi vinaendelea kubomoa misingi ya uhuru na demokrasia; maisha na mali za watu, kumbe wahusika wanapaswa kushughulikiwa kikamilifu, ili amani na utulivu viweze tena kurejeshwa. Itachukua muda mrefu kwa waathirika kuweza kupona kimwili na kisaikolojia, lakini wananchi wa Ufaransa kamwe wasitumbukie kwenye kishawishi cha mpasuko wa kitaifa, chuki na uhasama, bali waendelee kushikamana kama taifa moja ili kupambana kikamilifu na vitendo vya kigaidi.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.