2016-07-15 09:34:00

Bolivia: Dumisheni umoja wa kitaifa!


Familia ya Mungu nchini Bolivia inaadhimisha kumbu kumbu ya mwaka mmoja tangu Baba Mtakatifu Francisko alipotembelea nchini humo kuanzia tarehe 8 - 10 Julai 2015. Askofu mkuu Giovanni Battista Diquattro, Balozi wa Vatican nchini Bolivia ameadhimisha Ibada ya Misa Takatifu kwa ajili ya kumbu kumbu hii kwa kuitaka familia ya Mungu nchini Bolivia kujenga na kudumisha umoja wa kitaifa, ustawi na maendeleo ya wengi.

Familia ya Mungu iwe na ujasiri wa kujikita katika maisha ya sala ili kuweza kumfungulia Mwenyezi Mungu malango ya maisha yake ili kuondokana na woga na simanzi zisizo na mashiko na badala yake, kukita maisha yao katika ujasiri ili kutoka kifua mbele kujenga na kudumisha umoja wa kitaifa unaowaambata wote bila ubaguzi! Ibada hii ya Misa Takatifu imehudhuriwa na umati mkubwa wa familia ya Mungu uliokuwa chini ya uongozi wa Askofu mkuu Sergio Alfredo Gualberti Calandrina wa Jimbo kuu Santa Cruz de la Sierra, huko Bolivia.

Itakumbukwa kwamba, Mwaka mmoja uliopita Baba Mtakatifu Francisko aliadhimisha Ibada ya Misa Takatifu katika eneo hili na kuhuduhuriwa na watu zaidi ya millioni mbili. Katika mahubiri yake, Askofu mkuu Sergio amewataka waamini kujenga utamaduni wa upendo na mshikamano; kwa kujikabidhi mikononi mwa Mwenyezi Mungu ili kuweza kupokea neema na baraka zake zinazofumbatwa katika imani, mapendo na matumaini. Hakuna sababu msingi kwa waamini kuelemewa na wasi wasi wala woga usiokuwa na mashiko katika maisha yao, kwani wakizidiwa na woga watadumaa hata katika maisha ya kiroho.

Katika ibada hii ya Misa Takatifu kwa namna ya pekee, wamemkumbuka Hatari Kardinali Julio Terrazas Sandoval aliyefariki dunia hapo tarehe 9 Desemba 2015. Baba Mtakatifu alipokuwa nchini Bolivia alipata nafasi ya kwenda kumsalimia Kardinali Sandoval alipokuwa amelazwa hospitalini. Mji mkuu wa La Paz, umefanya pia kumbu kumbu ya mwaka mmoja tangu Baba Mtakatifu Francisko alipotembelea Bolivia kwa kufanya onesho la picha na juma zima la katekesi makini kwa kuwataka waamini kuwa ni vyombo na mashuhuda wa huruma na upendo wa Mungu kwa waja wake.

Itakumbukwa kwamba, Baba Mtakatifu Francisko alipokuwa nchini Bolivia alipata nafasi ya kutembelea Gereza kuu la Palmasola ili kuonesha uwepo wake wa karibu na wafungwa, huku akiwataka kutumia kipindi cha adhabu yao gerezani kuwa ni muda muafaka wa toba na wongofu wa ndani, ili wanapotoka gerezani waweze kuanza kuandika ukurasa mpya wa maisha yao kwa njia ya wema na uadilifu wa maisha. Viongozi wa Kanisa wanasema, bado kuna haja ya kuendelea kufanya maboresho makubwa katika mfumo wa sheria na mahakama ili haki iweze kutendeka kwa haraka zaidi kwa kuzingatia usawa, kwani waswahili wanasema, “Mnyonge mnyongeni tu, lakini haki yake mpeni!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.