2016-07-13 14:39:00

Yaliyojiri katika maisha na utume wa P. Lombardi!


Padre Federico Lombardi, S.J. anayeng’atuka kutoka madarakani rasmi hapo tarehe 31 Julai 2016 amekuwa ni msemaji mkuu wa Vatican kwa kipindi cha miaka kumi na kwamba, amekuwa ni gwiji katika tasnia ya habari duniani. Kuteuliwa kwa Dr. Greg Burke kuwa msemaji mkuu wa Vatican na Dr. Paloma Garcìa Ovejero kuwa msemaji mkuu msaidizi ni tukio ambalo limekuwa na mwangwi mkubwa kwenye vyombo vya mawasiliano ya jamii, ikikumbukwa kwamba, timu hii sasa inaongozwa na waamini walei ambao wamejipambanua katika huduma yao katika tasnia ya habari!

Padre Lombardi katika mahojiano maalum na Radio Vatican anakiri kwamba, uteuzi wa Baba Mtakatifu Francisko ni jambo la kawaida katika maisha na utume wa Kanisa kwani kila mtu anateuliwa kutekeleza dhamana na wajibu wake kwa muda uliopangwa na huduma inapofika ukomo,  kutokana na sababu mbali mbali, basi mtu anang’atuka na kuwaachia wengine kuendeleza utume wa Kanisa. Kwa muda wa miaka mitatu, anasema Padre Lombardi ameonesha kwa Baba Mtakatifu Francisko utayari wake wa kung’atuka kutoka madarakani lakini wakati huo huo, akijiachilia chini ya uamuzi wa Baba Mtakatifu Francisko.

Padre Lombardi anakiri kwamba, kuwa msemaji mkuu wa Vatican ni huduma nyeti kwa Khalifa wa Mtakatifu Petro na maisha ya Kanisa la Kristo. Wasi wasi na hofu kama alivyosema Dr. Burke ni jambo la kawaida sana, lakini wale wanaoteuliwa kutekeleza dhamana hii wanajiachilia mikononi mwa Mwenyezi Mungu, huku wakiwa na imani na matumaini. Wanatambua karama na mapungufu yao ya kibinadamu na kwamba, hii ni shule endelevu katika maisha na utume wa Kanisa.

Katika kipindi cha miaka 10 ya huduma yake kama msemaji mkuu wa Vatican amejifunza mengi, amekuwa na wasi wasi, hofu na mashaka, kumbe, hii ni hija ya maisha ya kila siku, hakuna mtu anayezaliwa akiwa na uhakika wa kuwa ni Msemaji mkuu wa Vatican, bali pale mtu anaposhikwa, hapo anashikamana kwa dhati pasi na utani! Kwa njia ya hija ya maisha ya kila siku, mtu anajipatia uzoefu na mang’amuzi mapya; anaimarisha utulivu na usalama wa ndani.

Padre Lombardi anawapongeza Dr. Greg Burke na DR. Paloma Garcìa Ovejero wanaoanza utume wao wakiwa vijana kabisa, kumbe wataweza kujipatia uzoefu na mang’amuzi, huku wakisaidiana na wadau mbali mbali katika tasnia ya habari ndani na nje ya Vatican. Kuna ushirikiano mkubwa katika tasnia ya mawasiliano ya jamii ndani ya Vatican anakiri Padre Lombardi bila kusahau kwamba, wadau mbali mbali wamekuwa tayari kutoa habari na ushauri kuhusiana na masuala mbali mbali ya maisha na utume wa Kanisa.

Ni matumaini yake kwamba, wasemaji wakuu wa Vatican watapata msaada mkubwa ndani ya Vatican ili kuwawezesha kutekeleza vyema dhamana na wito wao katika maisha na utume wa Kanisa, lakini wanapaswa kujiamini pamoja na kuwaamini wale wanaofanya nao kazi, ili kujenga amani na utulivu katika mazingira ya kazi.

Padre Lombardi ambaye amefanya utume wake chini ya Baba Mtakatifu mstaafu Benedikto XVI na baadaye Papa Francisko anasikitika kusema, kama kuna wakati mgumu aliokumbana nao katika utume wake kama Msemaji mkuu wa Vatican ni pale alipolazimika kushiriki katika masuala yaliyokuwa yanajadili kuhusu nyanyaso za kijinsia dhidi ya watoto wadogo ndani ya Kanisa. Alishiriki kikamilifu katika mijadala yote kwa kutambua kwamba, huu ulikuwa ni mchakato wa kulitakasa Kanisa dhidi ya vitendo hivi vichafu vinavyodhalilisha utu na heshima ya binadamu. Papa mstaafu Benedikto XVI alisimama kidete ili kuhakikisha kwamba, Kanisa linajitakasa zaidi na hivyo kuondokana na kashfa za nyanyaso za kijinsia.

Padre Lombardi anakiri kwamba, ameshirikiana na wadau mbali mbali pamoja na kutoa mchango wake katika mchakato wa mapambano dhidi ya nyanyaso za kijinsia kwa watoto wadogo ndani ya Kanisa katika: haki, ukweli na uwazi. Uvujaji wa nyaraka za siri na mipasuko ya kibinadamu ndani ya Vatican ni mambo ambayo yalikuwa yanatia uchungu na simanzi moyoni kwani ni rahisi sana kusema ukweli, lakini ukweli unaposemwa kwa kushiriki pia katika mahangaiko na mateso ya wahusika hapo “kiitikio” kinabadilika. Mchakato wa mawasiliano hauna budi kusaidia kufafanua haki na ukweli wa mambo, ili kuwa na mtazamo mpana zaidi kuhusu matatizo yaliyojitokeza.

Padre Federico Lombardi anakiri kwamba, hana mpango wa kwenda pensheni ifikapo tarehe 31 Julai 2016 kwani kama mtawa daima ataendelea kujitoa na kujisadaka kwa ajili ya maisha na utume wa Kanisa kwa watu watakaokuwa wanahitaji huduma na msaada wake. Anasema, wote hawa watapata majibu yatakayokuwa yanabubujika kutoka katika sakafu ya moyo wake.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.