2016-07-13 15:55:00

CELAM: Utakatifu na ukuu wa maisha ya ndoa!


Shirikisho la Mabaraza ya Maaskofu Katoliki Amerika ya Kusini, CELAM linasema kuna haja kwa waamini pamoja na watu wenye mapenzi mema kujikita katika toba na wongofu wa ndani ili kusimama kidete kulinda, kutetea na kushuhudia Injili ya familia inayofumbatwa katika uhai na huruma ya Mungu. Kuna haja kwa waamini kushuhudia utakatifu, ukuu na umuhimu wa maisha ya ndoa na familia, kama sehemu ya ushuhuda wa mwelekeo mpya wa shughuli za kichungaji ndani ya Kanisa huko Amerika ya Kusini.

Haya ni kati ya mambo ambayo yamepewa kipaumbe cha pekee na Shirikisho la Mabaraza ya Maaskofu Amerika ya Kusini katika mkutano wake uliohitimishwa hivi karibuni huko Quito, Equador. “Tumelitambua na kuliamini pendo lake” ndiyo kauli mbiu iliyoongoza mkutano kuhusu familia ulioandaliwa na Idara ya familia, maisha na vijana ya Shirikisho la Mabaraza ya Maaskofu Katoliki Amerika ya Kusini. Wajumbe kutoka Mabaraza ya Maaskofu Katoliki Amerika ya Kusini walishiriki na kuchangia kikamilifu katika Wosia wa Kitume wa Baba Mtakatifu Francisko “Furaha ya Upendo ndani ya familia”

Askofu Ruben Gonzalèz Medina, Mwenyekiti wa Idara amewataka wajumbe kutafuta na kuibua mbinu mpya za mikakati na shughuli za kichungaji kwa ajili ya maisha na utume wa familia huko Amerika ya Kusini. Lengo ni kuliwezesha Kanisa kukutana na wanafamilia mbali mbali, tayari kusikiliza kilio, furaha, utakatifu na ukuu wa maisha ya ndoa na familia, ili wote waweze kujisikia kuwa kweli ni sehemu ya maisha na utume wa Kanisa.

Ili kuweza kuzifikia familia mbali mbali kuna haja ya kujikita katika toba na wongofu wa ndani; kwa kuangalia na kuguswa na shida na mahangaiko ya familia. Ni wajibu wa wazazi kusimama kidete katika malezi na makuzi ya watoto wao pamoja na kuwawezesha waamini kukuza na kudumisha tasaufi ya maisha ya ndoa na familia kama anavyohimiza Baba Mtakatifu Francisko katika Wosia wake wa kitume, “Amoris laetitia”.

Wosia huu wa kitume kutoka kwa Baba Mtakatifu Francisko ni matunda ya sala, tafakari na upembuzi yakinifu uliofanywa na Mababa wa Sinodi katika kipindi cha miaka miwili na baadaye kufuatiwa na Katekesi makini juu ya maisha na utume wa familia katika ulimwengu mamboleo. Ili kufikia malengo yaliyobainishwa na Baba Mtakatifu, kuna haja ya kuendelea kujikita katika toba na wongofu wa ndani kwa kuchuchumilia utakatifu wa maisha na kuondokana na mambo ambayo yanasababisha misigano na mipasuko na matokeo yake ndoa zinasambaratika.

Viongozi wa Kanisa wawe mstari wa mbele katika mchakato unaopania kuwasindikiza wanafamilia wanaoogelea katika shida, kinzani na mipasuko ya kifamilia, ili waweze kuonja uwepo wa Kanisa katika mahangaiko yao. Kwa njia hii, wanandoa wataweza kutafakari juu ya mapenzi ya Mungu katika maisha yao, tayari kutafuta na kutekeleza mapenzi ya Mungu katika maisha yao. Kanisa liwe ni shuhuda na chombo cha matumaini kwa familia ambazo zimekata tamaa na kutumbukia katika shida na mahangaiko mbali mbali.

Ukuu na utakatifu wa maisha ya ndoa na familia ni muhimu sana kwa ustawi na maendeleo ya Kanisa na ulimwengu katika ujumla wake. Waamini wanapaswa kujifunga kibwebwe kutangaza na kushuhudia Injili ya familia kwa kujibu kilio cha ndani kabisa cha matamanio ya binadamu licha ya changamoto zinazoendelea kujitokeza katika ulimwengu mamboleo na maendeleo ya sayansi na teknolojia. Wajumbe wamekaza kusema bila kigugumizi wala makunyanzi usoni kwamba ndoa na familia ni wito na hija ya maisha ya utakatifu ili kumwilisha mpango wa Mungu katika maisha ya mwanadamu!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.