2016-07-12 14:15:00

Vita imepamba moto Sudan ya Kusini!


Katika siku za hivi karibuni, Sudan ya Kusini imegeuka kuwa ni uwanja wa vita kiasi cha kusahau kwamba, kuna mkataba wa amani uliotiwa sahihi na viongozi wa kisiasa ili kuhakikisha kwamba, amani na utulivu vinarejeshwa tena nchini Sudan ya Kusini ili kusaidia mchakato wa kuharakisha maendeleo ya watu. Viongozi wamesahau wajibu na dhamana ya kulinda raia na mali za ona badala yake wameelemewa na uchu wa mali na madaraka.

Katika mapambano ya silaha kali yaliyofanyika katika kipindi siku chache zilizopita, taarifa zinaonesha kwamba,  zaidi ya watu 300 wamepoteza maisha huko Sudan ya Kusini, inayosherehekea kumbu kumbu ya miaka mitano ya uhuru wake kwa kumwaga damu ya watu wasiokuwa na hatia! Viongozi wa Serikali na chama cha upinzani baada ya kushuhudia madimbwi ya damu, wamewaagiza wanajeshi kusitisha mapigano mara moja na kuanza kuwalinda raia na mali zao.

Kinzani za kikabila hazina mashiko wala mvuto kwa ustawi na maendeleo ya wananchi wa Sudan ya Kusini ambao kwa sasa wamechoka kuishi kwa wasi wasi kutokana na vita ya wenyewe kwa wenyewe inayoendelea. Mapambano haya yamepelekea zaidi ya wananchi elfu saba kukimbilia kwenye kambi za Umoja wa Mataifa ili kutafuta hifadhi na usalama wa maisha yao.

Vikosi vya upinzani na Jeshi la Serikali vinatupia lawama za mashambulizi haya. Wachunguzi wa mambo wanasema wapinzani wanaungwa mkono na Serikali ya Sudan Kongwe na kwamba, Serikali ya Salva Kiir inaungwa mkono na Uganda. Mkataba wa amani uliotiwa sahihi mwezi Agosti 2015 bado haujafua dafu ili kuwaletea wananchi amani na utulivu na badala yake mtutu wa bunduki unaoendelea kusikika kila kukicha!

Takwimu zinaonesha kwamba, zaidi ya watu laki tano wamekwisha fariki dunia kutokana na vita ya wenyewe kwa wenyewe Sudan ya Kusini na watu zaidi ya millioni moja na nusu wamelazimika kuyakimbia makazi yao na kwa sasa wanaishi kwenye kambi za wakimbizi na watu wasiokuwa na makazi maalum. Kinzani ya kikabila na kisiasa pamoja na mapigano haya ni mambo yanayoendelea kukwamisha mchakato wa maendeleo endelevu Sudan ya Kusini.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.

 

 








All the contents on this site are copyrighted ©.